|
Mkakati wa utekelezaji wa Sheria mpya ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Namba 14 ya mwaka 2007, (The Fire and Rescue Force Act, 2007) unaofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoji , unatarajiwa kusaidia kuboresha huduma ya zimamoto na uokoaji hapa nchini, baada ya Jeshi hilo kupewa mamlaka kisheria ya kuwa chini ya Komandi Moja (Central Command ) na hivyo kutambulika kama Jeshi kamili litakalosimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kiutendaji katika majukumu yote ya Zimamoto na Uokoaji nchini. Zaidi Christina Mwangosi anaeleza. Sheria hii inalenga kuunda mfumo mpya wa kisheria na nidhamu kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wenye lengo la kuweka usimamizi wa shughuli zote za zimamoto na uokoaji chini ya kamandi moja ya Kamishna Generali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Bunge lilipitisha Sheria hiyo katika kikao chake cha mwezi Aprili mwaka huu baada ya kupitisha muswada wa sheria hiyo mpya ambayo itaanza kutumika rasmi katika kipindi cha mwaka huu wa fedha. Hatua ya kutungwa kwa sheria hiyo mpya imefikiwa kutokana na kuwepo kwa maendeleo na mabadiliko ya kiteknolojia yaliyotokea katika medani za udhibiti wa majanga, uzoefu na changamoto zilizojitokeza nchini katika eneo hilo. Sheria hiyo ya Zimamoto na Uokoaji ya Mwaka 2007 iliyopitishwa mwaka huu na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupigwa chapa na Mchapishaji wa serikali tarehe 22 mwezi Juni mwaka 2007 , itatumika kwa serikali ya Tanzania Bara. Naibu Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Kamishna Michael Shija, anasema kuwa Sheria ya zamani ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji haikubadilishwa ila Sheria hiyo Na.3 ya mwaka 1985 ilifutwa kimakosa na sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 katika kifungu cha 35 (b) cha sheria hiyo. Kuhusu sheria ya sasa, sheria hiyo mpya imegawanyika katika sehemu kuu nne, ambapo sehemu ya kwanza inajumuisha Masharti ya awali kama vile jina la Sheria, tarehe ya kuanza kutumika na tafsiri ya maeneo na misamiati muhimu iliyotumika ndani ya sheria hiyo. Sehemu ya pili ya sheria hiyo inahusu muundo, majukumu na madaraka ya Jeshi la Zimamoto na Uokoji katika shughuli zake za kuzima moto, kufanya ukaguzi wa tahadhari za moto kwenye maeneo mbalimbali , kutoa elimu ya moto kwa Umma. Sehemu hii imeainisha majukumu zaidi ya kumi na nane (18) ya Jeshi la Zimamoto pamoja na kuweka masharti yanayohusu uwekaji na upatikani wa maji kwa ajili ya kuzimia moto katika maeneo mbalimbali. Sehemu ya tatu ya Sheria hiyo imeweka masharti yanayohusu masuala ya utawala kama vile uteuzi wa Maafisa wa juu wa Jeshi, akiwemo Kamishna Jenerali na Wasaidizi wake ikiwemo Mikoa, Wilaya na Vituo, kadhalika mambo ya nidhamu kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoji yameainishwa katika sehemu hii ya tatu ya sheria hiyo ya mwaka 2007. Sehemu ya nne ya sheria hiyo inahusu masuala mchanganyiko ambapo kuna masharti mbalimbali yanayohusu wajibu juu ya tahadhari za moto kwa Wadau mbalimbali hususani wenye majengo marefu, uwekaji wa maeneo ya kutokea wakati wa dharura, mameneja wa kudhibiti moto kwenye majengo marefu, mashuleni, Viwandani na sehemu zenye watu wengi, iwe kazini au sehemu ya kuishi, fidia kwa wazimamoto wa kujitolea nayo imeainishwa ndani ya sheria hii. Aidha sheria imeweka mfuko kwa ajili ya Jeshi, Mafunzo, baadhi ya makosa chini ya sheria hii na uwezo wa Waziri kutengeneza Kanuni. Kwa mujibu wa sheria hiyo mpya Namba 14 ya mwaka 2007, Jeshi litaongozwa na Kamishna Jenerali akisaidiwa na Makamishna, Manaibu Kamishna kwa ngazi ya Makao Makuu na kwamba ofisi za Mikoa na Wilaya zitaanzishwa kwa mujibu wa sheria hii mpya, hii ikimaanisha kuwa wigo wa Jeshi umepanuka hadi kufikia Wilayani ambako watateuliwa viongozi wa kuendesha mikoa na wilaya. Bwana Shija anasema kuwa katika kukabiliana na maafa ya zimamoto sheria hii mpya katika kifungu cha 12(5) imempa madaraka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuamrisha vikosi binafsi na wadau wote wanaoshughulika na masuala ya moto , kushiriki katika kukabiliana na maafa ya moto kwa maslahi ya Umma na Taifa kwa ujumla iwapo janga litatokea. Sheria hiyo pia katika kifungu cha 22 (1) na (2) inawataka pia wenye majengo marefu kuweka vifaa maalumu vya kuashiria moto na vifaa vya kuzima moto vinavyojiendesha vyenyewe. Anasema kuwa historia ya Zimamoto na Uokoaji nchini Tanzania ilianza mwaka 1945, mara baada ya vita ya Pili ya Dunia, baada ya vita kumalizika kikosi rasmi kilichojumuisha Maaskari waliokuwa vitani kilianzishwa kikiwa chini ya Jeshi la Polisi. Kikosi hicho kiliendelea kufanya kazi mjini Dar es salaam mpaka killipovunjwa na kuundwa vikosi viwili vipya ambavyo vilikuwa vyenye taratibu za kisayansi zaidi. Anafafanua kuwa Vikosi vilivyoundwa vilikuwa ni vya Zimamoto na Uokoaji Mijini na Zimamoto na Uokoaji Viwanja vya Ndege katika miaka ya 1950 na kwamba Zimamoto na Uokoaji Mijini zilikuwa chini ya Halmashauri za Miji na vilevile za Viwanja vya Ndege vilikuwa chini ya Idara ya Ujenzi. Kwa mujibu wa Kamishna Shija baada ya vikosi hivyo kuimarishwa umuhimu wa kuanzisha vikosi vya Bandari ulionekana na hivyo kikosi cha Bandari kilianzishwa kikiwa chini ya Mamlaka ya Bandari. “Mara baada ya Uhuru Serikali iliendelea kutambua shughuli za Idara ya Zimamoto na Uokoaji na kuiweka katika Serikali Kuu mwaka 1961 chini ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi,”’ anaeleza Kamishna Shija na kuongeza kuwa kati ya mwaka 1979 – 1981 Serikali iliamua kufanya utafiti juu ya hali ya shughuli za Zimamoto na Uokoaji nchini, utafiti ambao uligundua mambo kadhaa. Utafiti uligundua kuwa hakukuwa na mamlaka kuu iliyokuwa ikisimamia shughuli zote za Zimamoto na Uokoaji nchini, hivyo kukosa kuwajibika na pia kukosa Sera na miongozo mbalimbali ya huduma ya Zimamoto na Uokoaji kwa ujumla. Anafafanua kuwa mwaka 1982 shughuli za Zimamoto na Uokoaji zilihamishiwa Wizara ya Mambo ya Nchi ikiwa nia kuu ni kuondoa misingi ya kiraia katika utendaji kazi, hata hivyo vikosi vingine viliendelea kufanya kazi chini ya mamlaka wanazozitumikia ambazo ni pamoja na mamlaka ya Bandari, Serikali za Mitaa, Mashirika na Makampuni. Anasema kuwa mwaka 1985 hatua za kisheria zilichukuliwa na kutunga sheria ya kuanzisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Na.3 ya mwaka 1985 na kwa kuanzia utekelezaji wa Sheria hiyo, askari waliokuwepo kwenye kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Viwanja vya Ndege ndio waliounda Jeshi la Zimamoto na Uokoaji chini ya Kamishna wa Zimamoto. Askari wa vikosi vingine kama Miji, Bandari, Misitu hawakujiunga na Jeshi hilo mara moja na hali hii iliendelea kuwa hivyo kwa sababu ya urasimu wa kiutendaji. Kadhalika mwaka 1996 Serikali iliamua kurejesha tena shughuli za Zimamoto Viwanja vya Ndege chini ya Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi kiutendaji. Ofisi ya Kamishna wa Zimamoto na Uokoaji chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ilibakiwa na majukumu ya Kuandaa na kusimamia sera, Kuandaa na kuendesha mafunzo ya Zimamoto wote nchini sambamba na kufuatilia shughuli za vikosi vya Zimamoto na Uokoaji Nchini Mwaka 2002 sheria Na. 3 ya mwaka 1985 ya Zimamoto na Uokoaji ilifutwa kimakosa na sheria Na. 8 ya mwaka 2002 ya Utumishi wa Umma na kusababisha mabadiliko ya kiutumishi na kiutendaji ambapo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji liliingizwa tena kwenye mfumo wa kiraia chini ya Programu ya Kuboresha huduma za Serikali. Kwa mujibu wa Naibu Kamishna Shija, Vikosi mbalimbali vilianzishwa chini ya Asasi mbalimbali hali iliyochangia kutokuwa na mfumo mmoja wenye mtiririko. Kila Idara au Asasi ilikuwa na utaratibu wake. Kutokana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ilipendekezwa mambo mbalimbali ambayo yanaweza kuleta ufanisi katika uendelezaji huduma ya Zimamoto na Uokoaji. Hii ndio sababu, katika jitihada za kuendeleza huduma ya Zimamoto na Uokoaji, Serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepitisha sheria Na 14 ya 2007 ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji yenye lengo la kuimarisha nidhamu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na shughuli za kiutawala na kiutendaji. na pia kujenga kamandi kuu katika shughuli za Zimamoto na Uokoaji Kuhusu mahusiano ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Vikosi vya Makampuni Binafisi Naibu Kamishna Shija anafafanua kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji hutoa leseni za uendeshaji wa huduma za Zimamoto na Uokoaji kwa vikosi vya Makampuni binafsi ili kupanua wigo wa huduma ya Zimamoto na Uokoaji. Aidha Idara inaandaa Kanuni zitakazoainisha masharti ya kuanzisha vikosi binafsi na utoaji wa huduma hiyo kwa umma. Katika hotuba yake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Joseph Mungai alipokuwa akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2007/2008 alisema kuwa hatua kadhaa zitachukuliwa kuunda Jeshi la Zimamoto na Uokoji la kisasa lenye ufanisi bora zaidi katika kukabiliana na majanga mbalimbali. Mheshimiwa Mungai alisema kwa dhana hiyo na ili kuleta ufanisi unaotakiwa zitaanzishwa Ofisi za Mikoa na Wilaya kama ilivyo kwa majeshi ya Polisi na Magereza ambapo mwaka mpya wa fedha wa 2007/2008 utatumika kwa ajili ya kujipanga upya, ambapo mwaka wa fedha wa 2008/2009, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji litaanza kazi kwa nguvu mpya, Kadhalika Wizara itahakikisha suala la mafunzo kwa askari wa Zimamoto na Uokoji linapewa kipaumbele sambamba na upatikanaji wa Chuo cha kitaifa cha Zimamoto na Uokoaji. Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Sotery Ntamuturano hivi karibuni aliiambia kamati ya Bunge ya ulinzi na Usalama iliyotembelea vituo vya zimamoto na Uokoaji Jijini Dar es salaam kuwa miongoni mwa majukumu ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo ni pamoja na kuhakiki mali zote za vikosi vya zimamoto na uokoaji wa ili ziweze kuwa chini ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Kwa mujibu wa Kamishna Ntamuturano ili kuimarisha huduma za zimamoto na uokoaji upo uwezekano wa mafunzo ya zimamoto kutolewa kwa mgambo hususani maeneo ya vijijini, hali ambayo itasaidia kuongeza nguvu katika kupambana na kasi ya majanga ya moto na kwamba elimu ya moto itatolewa pia kwa watoto wadogo.na watanzania wote kwa ujumla. Amesema kupitishwa kwa sheria hiyo kunalipa mamlaka kisheria Jeshi la Zimamoto kuweza kutekeleza majukumu yake kisheria tofauti na ilivyokuwa awali na kwamba matatizo mengi yanatarajiwa kutatuliwa mara baada ya utekeleaji wa sheria hiyo mpya. Aidha matatizo mengi ambayo yamekuwa yakitokea kwenye iliyokuwa Idara ya Jeshi la Zimamoto imetokana na kutokuwepo kwa sheria ambayo ingeipa mamlaka ya kuwa katika Komandi Moja(Central Command). Kwa upande wake ujumbe wa kamati ya Bunge ya Ulinzi na usalama ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wake Kaptain George Mkuchika iliyotembelea vituo vya Zimamoto na Uokoaji imesema kuwa chini ya sheria hiyo mpya Idara ya Zimamoto na Uokoji imekuwa sasa Jeshi kamili la Zimamoto na Uokoaji na litastahili kupata haki zote zinazopaswa kupatiwa kwa mujibu wa sheria, kama ilivyo kwa majeshi mengine. Ujumbe wa kamati hiyo jukumu la kupambana na majanga ya mot ni ya kila mtanzania hivyo kila mtanzania anapaswa kuona ana wajibu huo kwa kuzingatia hasa tahadhari za kutokea kwa majanga ya moto kutokana na baadhi ya matukio kutokea kutokana na uzembe wa watu. Aidha kamati hiyo imesema itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kusaidia utekelezaji wa sheria hiyo ya Jeshi la Zimamoto na Uokoajina hivyo kuliweka taifa katika hali ya ulinzi na usalama zaidi. Na Christina Mwangosi – (Afisa Habari , Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi) |