|
Serikali nchini Tanzania imeanza kuchukua hatua kadhaa za utekelezaji wa mikakati mbalimbali inayolenga kupunguza tatizo la Msongamano wa Wafungwa na Mahabusu katika Magereza yake hapa nchini, miongoni mwa mikakati hiyo ni Uimarishaji na Upanuzi wa Magereza, Ujenzi wa Magereza Mapya ya Mahabusu ya Wilaya, Ukamilishaji wa Magereza yanayoendelea Kujengwa sambamba na Ukarabati wa Magereza ya Mahabusu. Tatizo la Msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye Magereza hapa nchini limekuwa ni mojawapo ya matatizo makuu yanayoathiri utekelezaji wa majukumu ya mbalimbali ya Jeshi la Magereza linalolenga kuleta, kuendeleza na kudumisha usalama wa jamii hapa nchini. Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Magereza imesema kuwa kwa upande wa ujenzi wa Magereza mapya ya Mahabusu ya wilaya, serikali ina mpango wa kujenga magereza ya wilaya mapya ya mahabusu kwa awamu katika wilaya zisizokuwa na magereza hayo na kwamba ujenzi huo utazingatia idadi ya mahabusu katika wilaya husika, umbali kutoka gereza la karibu pamoja na kiwango cha uhalifu katika wilaya husika. Aidha magereza hayo 36 yatajengwa kwa kutumia ramani maalumu za kisasa ambazo zitazingatia viwango vyote vya utenganisho wa wahalifu na kwamba kiasi cha shilingi za Kitanzania 18,000,000,000 kimekadiriwa kutosheleza ujenzi wa magereza hayo kwa gharama ya TShs 500,000,000/= kwa kila gereza. Hata hivyo kuanzia mwaka wa fedha wa 2003/2004 ujenzi wa mabweni ya wafungwa ulianza kwenye wilaya za Mbarali, Mbinga na Igunga ambazo hazikuwa na magereza ya mahabusu. Kwa upande wa ukamilishaji wa Magereza yanayoendelea kujengwa kati ya magereza 66 ya mahabusu yaliyopo hivi sasa yapo magereza 17 ambayo ujenzi wake haujakamilika na kwamba magereza hayo yapo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Kukamilika kwa magereza hayo kutasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu uliopo hivi sasa magerezani ambapo ukamilishaji huo unakadiriwa kugharimu Tshs 12,920,000,000/=. Kuhusu mkakati wa ukarabati wa upanuzi wa Magereza ya Mahabusu magereza mengi yaliyopo yamejengwa zamani ni ni machakavu ambapo baadhi ya magereza hayo uwezo wake wa kuhifadhi wahalifu kisheria ni mdogo kulingana na idadi ya kuhifadhi wahalifu waliopo hivi sasa ambayo ni zaidi ya mara mbili ya uwezo huo hivyo kumekuwepo na mpango wa kukarabati na kupanua magereza yaliyopo ili yaendelee kuwa mahali salama pa kuhifadhi wahalifu, ukarabati na upanuzi wa magereza hayo utagharimu jumla ya TShs 8,449,00,000/=. Hata hivyo shughuli za upanuzi na ukarabati wa magereza zilisimama kwa muda mrefu kutokana na fedha za Maendeleo (Development Budget ) ziliachwa kutolewa tangu mwaka wa fedha 1992/1993 hata hivyo kuanzia mwaka wa fedha wa 2002/2003, Serikali ilianza tena kutoa fedha hizo, hivyo kazi ya ukarabati na upanuzi wa magereza makubwa, ukamilishaji wa mabweni ya wafungwa, nyumba za askari zimeanza kufanyika tena sambamba na kazi hizo kuaznia mwaka wa fedha wa 2003/2004 ujenzi wa mabweni ya wafungwa ulianza kwenye wilaya za Mbarali, Mbinga na Igunga ambazo hazikuwa na Magereza na mahabusu. Kadhalika ujenzi wa Magereza mapya na upanuzi way ale ya zamani ni njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani, katika kipinci cha mwaka 1985 hadi na 1990 juhudi zimefanyika kupanua na kukarabati Magereza mapya kama vile Mwanga, Magu, Handeni, Mpwapwa, Magumu, Bariadi, Kahama, Muleba, Sumbawanga, Liwale,Bagamoyo, Rombo, Makete na Segerea. Aidha upo mpango wa kabambe uliokwishaidhinishwa na Serikali kujenga Magereza makubwa sita (6) ya Kanda nchini ambayo yatakuwa na uwezo wa kuchukua wafungwa wengi wa vifungo virefu kwa wakati mmoja na kwamba tatizo linalokabili uanzishaji wa mpango huo ni fedha za utekelezaji. Tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu Magerezani ni la muda mrefu, tatizo hili limeongezeka hivi karibuni baada ya seriklai kuanzisha Sheria ya vifungo vya muda mrefu na kuanza kuwapokea wafungwa hao magereani kwani wanaoingia ni wengi lakini wanaotoka ni wachache, wakati ambapo Magereza yana nafasi ya watu 22,669, mafungulio ya kila siku siyo chini ya wahalifu 45,000. Uharakishaji wa Kesi Mahakamani kwa kusikiliza kesi kwa zamu mbili (shift system) pamoja na kuanzishwa kwa kamati za kusukuma kesi mahakamani (Case Flow Management Committees) ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na serikali kupambana na tatizo la msongamano magerezani. Mfumo wa Kifungo cha Nje kinatumika kwa lengo la kutatua tatizo hilo, kwa mujibu wa kifungu cha 72 cha sheria ya Magereza ya mwaka 1967 (Prisons Act,1967) wafungwa wanaostahili kutolewa kifungo cha nje ni wale wanaotumikia kifungo kisichozidi miezi kumi na mbili, Hata hivyo utaratibu wa kuwatoa wafungwa kutumia kifungo cha nje hautekelezwi ipasavyo sehemu nyingi kutokana na Halmashauri za Miji kukosa fedha za kuwahudumia. Mpango wa Parole ni utaratibu ambao wafungwa wenye tabia nzuri wanaotumikia vifungo magerezani kuanzia miaka minne na kuendelea ambao makosa yao hayana hisia kali katika jamii wanaweza kuachiliwa kwa masharti ili wamalizie vifungo vyao nje kwa kuishi na familia zao. Hadi mwezi Machi mwaka 2007 wafungwa wapatao 2,530 wameachiliwa kwa utaratibu huu tangu uanze , tatizo kubwa la utaratibu huu ni lile la kuacha nje ya wigo wafungwa wengi wa vifungo virefu na makosa makubwa waliopaswa kufaidika na mpango huo. Kadhalika Sheria ya Huduma Kwa Jamii (Community Service) huu ni utaratibu ambao wahalifu wanatiwa haiani kwa makosa ambayo kifungo chake kwa mujibu wa sheria hakizidi miaka miatatu hupewa nafasi ya kwenda kufanya kazi ya huduma za kijamii bila malipo kwa faida ya jamii yenyewe badala ya kutumikia kifungo gerezani, lengo la kutungwa kwa sheria hii pamoja na mambo mengine ilikusudiwa kupunguza msongamano ndani ya magereza kwa sababu watakaokuwa wanahukumiwa chini ya sheria hii wengi hawatakuwa wanaingia magerezani bali watakuwa wanatoka mahakamani moja kwa moja kwenda kwenye maeneo waliyopangiwa kufanya kazi. Magereza yote nchini yanahifadhi wastani wa wafungwa 3,000 kwa siku ambao wangeweza kwenda kufanya kazi za huduma kwa jamii kama utaratibu huu ungekuwa umesambaa nchi nzima na vyombo vingine vinavyohusika bna utekelezaji wa sheria hii kama Mahakama vingekuwa vimeanza kutekeleza sheria hii ipasavyo. Msamaha wa Rais kwa wafungwa pia ni miongoni mwa mikakati ya kupungunza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani, Kisheria Jeshi la Magereza kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi humshauri Mheshimiwa Rais kutoa msamaha kwa baadhi ya wafungwa kwa kuzingatia vigezo vitakavyowekwa kwa wakati huo ambapo kwa utaratibu huo zaidi ya wafungwa 7,000 waliachiliwa huru mwaka 2006. Hata hivyo kukua kwa uhalifu sambamba na ongezeko la idadi ya watu na ongezeko la umasikini kwa ujumla ni miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia kuwepo kwa tatizo la Msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza hapa nchini.Takwimu za mwaka 2003 kwa mfano zinaonesha kwamba kati ya wahalifu 18,079 waliokuwa na vifungo vya hadi miaka kumi (10), idadi ya 10,687 kati yao walikuwa na makosa ya kuwania mali (offences against property) ambao ni wizi, kuvunja nyumba na unyang’anyi. Hii ni asilimia 59% ya wahalifu wote hao, tafsiri iliyopo hapa ni kwamba wengi wa wahalifu wanaotumikia vifungo vya hadi miaka kumi (10) ni wale walioshindwa kujipatia vipato halali kwa sababu ama za ukosefu wa ajira na ujuzi, utaalamu wa kuwawezesha kujiajiri. Sababu nyingine za msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani ni uchache wa magereza kwa sababu magereza mapya hayajengwi kulingana na kasi ya kukua kwa mahitaji, hivi sasa zipo wilaya 36 nchini ambazo hazina magereza, nyingi kati ya hizo zikiwa mpya zilianzishwa kwa lengo la kurahishisha utawala wa serikali. Suala hili pia ni chanzo cha uvunjifu wa Haki za Binadamu kwa watuhumiwa wanaolazimika kupelekwa kuhifadhiwa mbali na mamlaka za mahakama zinazoshughulikia kesi zao na hivyo mara nyingi kushindikana kufikishwa mahakamani kwa muda unaotakiwa na pia kutopata fursa za kutembelewa na ndugu, jamaa zao au hata mawakili wao. Mwisho . |