Ministry of Home Affairs Website

MOHA in Focus
Serikali imefunga jumla ya Kambi nane za Wakimbizi
Tuesday, 10 October 2006 23:16

SERIKALI ya Tanzania imefunga jumla ya Kambi nane za Wakimbizi, hapa nchini, ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya zoezi la kuwarejesha wakimbizi nchini kwao kwa hiari, baada ya hali ya amani na utulivu kuimarishwa na kuwa endelevu katika nchi zao za asili. Zoezi la kuwarejesha wakimbizi kwao kwa hiari linashirikisha Serikali ya Tanzania, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumiwa Wakimbizi (UNHCR) pamoja na nchi zenye wakimbizi husika. Zoezi hili lilianza mwezi Machi mwaka 2002, kwa wakimbizi kutoka Burundi na Oktoba, 2005 kwa wakimbizi kutoka Congo (DRC).

Kadhalika hatua ya kufungwa kwa baadhi ya kambi hizo ni sehemu ya matokeo ya mafanikio ya utekelezaji wa maamuzi ya Mkataba wa Kamisheni ya Pande Tatu (Tripartite Commission), inayojumuisha Serikali ya Tanzania, Shirika la Umoja wa Maitafa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR) pamoja na serikali za nchi wanakotoka wakimbizi hao (Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo).

Serikali imefikia uamuzi wa kufunga kambi hizo za wakimbizi kutokana na wakimbizi wengi kuamua kurudi katika nchi zao kwa hiari baada ya amani na utulivu kupatikana katika nchi hizo.

Sambamba na hilo uzoefu wa Serikali ya Tanzania katika kuhifadhi wakimbizi, umeonyesha kuwa pale ambapo amani na utulivu katika nchi za asili za wakimbizi inapopatikana na kuwa endelevu, basi huwa rahisi kwa wakimbizi hao kurejea nchini kwao kwa hiari, mara nyingi kabla hata hawajaanza kusaidiwa kurejea nchini mwao chini ya utaratibu wa Kamisheni ya Pande Tatu.

Kurejea makwao kunaipunguzia Serikali ya Tanzania mzigo mkubwa wa kuwahudumia wakimbizi Serikali inayo shauku kubwa, kuona kuwa tatizo la wakimbizi linamalizika, si katika nchi za Maziwa Makuu tu, bali Afrika nzima ili Afrika ipate kuondokana na aibu hii ya kuwa na wakimbizi.

Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bi. Judith Mtawali, anasema kuwa, tangu kuanza kwa mchakato wa wakimbizi kurejea nchini mwao kwa hiari Mwezi Machi mwaka 2002 hadi Juni mwaka 2007, jumla ya Kambi nane za wakimbizi zimekwisha kufungwa na kwamba zoezi hilo bado linaendelea.

Kambi zilizofungwa ni Kitali katika wilaya ya Biharamulo, Karago, Mtendeli na Mkugwa wilayani Kibondo, Lukole ‘B’ wilayani Ngara, Muyovosi wilayani Kasulu, Lugufu II wilayani Kigoma Vijijini na Mwisa wilayani Karagwe.

Bi Mtawali anasema, kambi ya utenganisho ya Mwisa haikuwa Kambi ya kawaida kama zilivyo kambi zingine za wakimbizi, bali imekuwa ikitumika kuhifadhi wakimbizi wakorofi k.m. waliokuwa wanashawishi wenzao kutorudi makwao na waliokuwa wanajihusisha katika masuala ya siasa. Ni marufuku kujihusisha na siasa katika makambi ya wakimbizi.

Kambi ya Mkugwa nayo ilikuwa ni tofauti kidogo kwa vile ilikuwa ikihudumia wakimbizi mchanganyiko wakiwemo wa kutoka Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Uganda, Ethiopia, Madagascar pamoja na Zimbabwe. Kwa wale waliokuwa katika kambi ya Mkugwa na ambao hawakuwa tayari kurejea makwao, walihamia katika Kambi ya Nduta Kibondo, baada ya Kambi ya Mkugwa kufungwa.

Anasema, zoezi la kufunga Kambi ya Lugufu II ilianza tangu mwezi Julai mwaka 2007, ambapo wakati huo ilikuwa na jumla ya wakimbizi 14,000. Zoezi la kufunga Kambi hiyo ya Lugufu II limekamilika Mwezi Septemba, 2007. Kambi ya Karago ilifungwa katika kipindi cha mwaka 2005. Kambi ya Lukole ‘B’ ilifungwa mwaka 2006 na Kambi ya Kitali ilifungwa mwaka 2003, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuanza kwa zoezi la wakimbizi kurejea kwa hiari nchini Burundi.

Kambi za Mtendeli, Mkugwa, Muyovosi na Kambi ya Utenganisho ya Mwisa zilifungwa katika kipindi cha kati ya Januari na Juni 2007.

Kuhusu idadi ya Kambi ambazo hazijafungwa na bado zinahudumia wakimbizi Bi. Mtawali anasema Serikali imesalia na Kambi sita (6) na Makazi manne ya wakimbizi ambazo zinaendelea kuhudumia wakimbizi. Kambi zilizosalia hapa nchini huku Wilaya na idadi ya wakimbizi zikiwa kwenye mabano ni Mtabila (Kasulu – 60,363), Nduta (Kibondo - 37,711), Kanembwa (Kibondo - 11,772) Lugufu I (Kigoma vijijini – 69,826) Nyarugusu (Kasulu – 51,151) na Lukole (Ngara – 37,343 Kambi za Mtabila, Kanembwa na Lukole zinahifadhi wakimbizi kutoka Burundi na zile za Lugufu I na Nyarugusu zinahifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ( DRC). Kambi ya Nduta ina wakimbizi wengi wa Burundi na wachache wa mataifa mengine kama vile Ethiopia, Madagascar, Zimbabwe, Kenya na wengineo waliohamia Nduta baada ya kambi ya Mkugwa kufungwa.

Aidha anasema jumla ya Makazi ya wakimbizi manne yanaendelea kuhudumia wakimbizi ambayo (Wilaya zake na idadi ya wakimbizi ziko katika mabano), ni pamoja na Makazi ya Katumba (Mpanda – 108,948), Mishamo (Mpanda - 51,017), Ulyankulu (Urambo - 50,708) zinazohudumia wakimbizi kutoka nchini Burundi na Chogo (Handeni – 2044) inayohudumia wakimbizi kutoka nchini Somalia.

Akizungumzia hali ya wakimbizi kwa ujumla Bi. Mtawali anasema hadi kufikia June mwaka 2007, kulikuwa na wakimbizi 481,075 na wengi wa wakimbizi hao ni kutoka katika nchi za Burundi (357,862) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (120,997). Anasema chini ya Mkataba wa Pande Tatu uliosainiwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania pamoja na (Serikali ya Burundi) na UNHCR, zaidi ya wakimbizi 319,583 walirejea kwa hiari nchini kwao Burundi tokea kuanza kwa zoezi hilo mwaka 2002. Kati ya hao zaidi ya wakimbizi 22,651 walirejea nchini Burundi wenyewe, yaani kwa maandalizi binafsi.

Chini ya mkataba uliofufuliwa kati ya Serikali ya Tanzania, Serikali ya Congo – DRC na UNHCR mwaka 2005, zaidi ya wakimbizi 34,348 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walirejea nchini mwao Kongo, ambapo zaidi ya wakimbizi 7,209 kutoka Kongo walirejea nchini kwao wenyewe, kwa maandalizi binafsi. (Mkataba wa kwanza kati ya Serikali ya Tanzania, Serikali ya Congo – DRC na UNHCR ulisainiwa mwaka 1997 ambapo wakimbizi wa DRC walianza kurejea kwao mpaka zoezi hilo lilipositishwa mnamo mwaka 1998 baada ya mapigano kuzuka upya nchini DRC).

Wakati huo huo tarehe 20 Mwezi Juni mwaka 2007, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Joseph Mungai aliwakabidhi Hati za Uraia wa Tanzania takribani wakimbizi 500 kutoka nchini Somalia wanaojulikana kama Wasomali wa Kibantu wanaoishi katika Makazi ya Chogo wilayani Handeni. Makazi hayo yana wakimbizi 2,044.

Anasema kutokana na zoezi la wakimbizi kurejea nchini kwao kwa hiari katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuendelea vizuri katika Mikoa ya Kigoma na Kagera, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2007 idadi kubwa ya wakimbizi watakuwa wamerejea nchini kwao hasa iwapo amani na utulivu vitaendelea kuwepo katika nchi hizo. Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo, bado kasi ya urejeshaji wakimbizi inaathiriwa na mambo mbali mbali ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa meli kubwa za kubeba abiria kwenye ziwa Tanganyika kutokana na uwezo mdogo wa MV Mwongozo inayotumika sasa wa kubeba abiria 500 tu. Kwa sasa Meli hiyo inafanya safari tatu kwa wiki kwenda DRC ili kufanikisha wakimbizi wanaotaka kurejea kwao kufanya hivyo.

Kwa upande wa Burundi kasi ya zoezi hilo ilipungua mwaka 2006 kutokana na ukame na njaa vilivyoikumba nchi hiyo ambapo baadhi ya wakimbizi waliogopa kurejea kwa kuhofia janga hilo na kwamba kasi ya zoezi hilo imeongezeka na inatarajiwa kuongezeka zaidi hususani baada ya mavuno. UNHCR kwa upande wao wameongeza msaada wa chakula kutoka miezi minne hadi sita kwa wanaorudi ikiwemo malipo ya fedha taslimu ya Dola za Kimarekani (USD) 50 mara wafikapo nchini kwao ili kuwawezesha kumudu maisha nchini mwao kabla ya kuanza kujitegemea.

Kuhusu wakimbizi walioko kwenye Makazi ya Ulyankulu, Katumba na Mishamo, Bi. Mtawali alisema utaratibu rasmi wa urejeaji wao Burundi bado haujaanza kwa vile uko tofauti na ule wa wakimbizi walio katika makambi ya mikoa ya Kigoma na Kagera. Kundi hili la kwenye Makazi limekaa nchini hapa kwa miaka mingi. Kwa sasa zoezi linaloendelea ni la uandikishaji wa wakimbizi hao ili kuweza kufikia suluhisho muafaka. Hata hivyo wapo wakimbizi wachache katika makazi hayo ambao wanaamua kurudi kwao katika kipindi hiki. Wakimbizi hao huunganishwa na wale waliopo mkoani Kigoma katika misafara ya kurejea Burundi.

Chini ya Mkataba wa Pande Tatu Serikali ya Tanzania inatarajia kufunga rasmi Kambi na Makazi yote ya wakimbizi hapa nchini katika kipindi cha mwaka wa fedha 2007/2008.

By Christina Mwangosi (Afisa Habari Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi) .

 


Page 4 of 4

Download Centre

Polls

Wananchi kuvamia vituo vya Polisi. Je wavamizi wanastahili kuchukuliwa hatua kali?
 
You are here  : Home