Get Adobe Flash player

1. Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa iliyowasilishwa mapema leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu likubali kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012. 

2. Mheshimiwa Spika, kabla sijawasilisha hotuba yangu mbele ya Bunge lako tukufu, naomba kuchukua fursa hii kutoa rambirambi zangu kwa familia na wananchi wa Jimbo la Ukonga waliopoteza ndugu zao kutokana na milipuko ya mabomu iliyotokea tarehe 16 Februari 2011 kwenye kambi la Jeshi la Wananchi wa Tanzania Gongo la Mboto, Dar es Salaam. Aidha, nawapa pole ndugu na jamaa wa marehemu waliofariki kwa ajali mbalimbali za barabarani. Namwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, Amina. 

3. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Edward Lowassa, Mbunge wa Monduli kwa kuyachambua makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.  Naishukuru pia Kamati hiyo kwa ushauri wao.  Naamini ushauri huu utasaidia sana kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara yangu.

4. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii pia kuwapongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha kwa hotuba zao walizozitoa mapema katika mkutano huu wa Bunge ambazo  zimetoa mwelekeo wa bajeti ya Serikali  na hali ya uchumi kwa jumla kwa mwaka wa fedha 2011/2012. 

5. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao, kuhifadhi na kuwarekebisha wafungwa, kudhibiti uingiaji na utokaji nchini wa raia na wageni, kutoa huduma za zimamoto na uokoaji, kuwahudumia wakimbizi waliopo nchini, kutekeleza programu ya Huduma  kwa Jamii  na kutoa vitambulisho vya Taifa. Majukumu haya yanatekelezwa kupitia Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Wakimbizi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa. 

MALENGO YA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2010

6. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza malengo ya ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imepangiwa  kutekeleza majukumu 10. Ningependa kueleza utekelezaji wa majukumu hayo katika kipindi cha mwaka 2010/2011 kama ifuatavyo:- 

7. Mheshimiwa Spika, jukumu la kwanza ni kuendeleza mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya. Katika kipindi cha Julai 2010  hadi Aprili, 2011 Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, lilikamata watuhumiwa 557 wenye kilo 529 za dawa za kulevya za viwandani. Kwa upande wa dawa za kulevya za mashambani, watuhumiwa 507 walikamatwa na kilo 17,000 za bangi na kilo 5,316 za mirungi. Vile vile ekari 309 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika Mikoa ya Tanga, Tabora na Mkoa wa Kipolisi wa Tarime - Rorya.

8. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya Jeshi la Polisi limekuwa likichukua hatua zifuatazo:-(i) Kubaini mtandao unaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.(ii) Kuendelea kushirikiana na Shirika la Polisi la Kimataifa – Interpol kutafuta taarifa za kiintelijensia kuhusu wasafirishaji wa dawa za kulevya. (iii) Kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya kwenye Viwanja vya Ndege, bandarini na mipakani.(iv) Kuunda Kikosi Kazi cha pamoja kinachojumuisha Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, TAKUKURU, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ili kuwabaini wafanya biashara wa dawa za kulevya. 

9. Mheshimiwa Spika, jukumu la pili ni kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Magereza. Jeshi la Magereza linachukua hatua mbalimbali ili kupunguza msongamano magerezani ikiwemo kujenga mabweni ya wafungwa, kutumia huduma za Parole, programu ya huduma kwa jamii na misamaha ya Rais inayotolewa wakati wa maadhimisho ya sherehe za kitaifa.  Pamoja na hatua hizo zilizokwisha kuchukuliwa bado Magereza yetu yanakabiliwa na msongamano mkubwa. Magereza yetu yana uwezo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu 29,552 lakini mpaka kufikia tarehe 1 Aprili, 2011 kulikuwa na wahalifu 37,811 katika Magereza yote nchini.  Kati ya hao 18,267 walikuwa ni wafungwa, na 19,544 ni mahabusu.   

10. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2010 hadi Aprili, 2011 wafungwa   154 waliachiliwa huru kwa utaratibu wa Parole. Hata hivyo, idadi ya wafungwa wanaoachiliwa kwa kutumia Sheria ya Bodi za Parole ya mwaka 1994 ni ndogo kutokana na Sheria hii kutowaruhusu wafungwa waliofanya makosa makubwa kuachiliwa huru chini ya utaratibu huu. Jumla ya wafungwa 792 walikuwa wanatumikia kifungo cha nje kwa kutumia kanuni za kifungo cha nje za mwaka 1968. Vile vile wafungwa 1,026 waliachiliwa na Mahakama ili kutumikia kifungo cha nje chini ya Sheria ya Huduma kwa Jamii. Hivi sasa Programu ya Huduma kwa Jamii inatoa huduma katika Mikoa 12 ya Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Iringa, Mara, Kagera na Shinyanga. Halikadhalika  wafungwa 3,626 walifaidika na msamaha wa Rais uliotolewa tarehe 9 Desemba, 2010 wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 49 ya Uhuru na wafungwa 3,117  waliachiliwa  tarehe 26 Aprili, 2011 wakati wa kuadhimisha sherehe za miaka 47 ya Muungano.  Katika kipindi cha mwaka 2011/2012 Wizara yangu kupitia Jeshi la Magereza imepanga kupunguza msongamano wa wahalifu magerezani kwa asilimia 20. 

11. Mheshimiwa Spika, jukumu la tatu ni kuimarisha na kuboresha mfumo wa upelelezi wa makosa ya jinai ili kurahisisha uendelezaji wa kesi mahakamani.  Jeshi la Polisi limetoa mafunzo ya upelelezi kwa askari 2,370. Jeshi hili pia limepata vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa makosa katika maabara yaani ‘forensic laboratory’. 

12. Mheshimiwa Spika, jukumu la nne ni kuanzisha mpango wa kuwapatia askari nyumba bora za kuishi.  Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) kwa udhamini wa Serikali umekamilisha ujenzi wa nyumba za makazi katika Kambi ya Polisi, Barabara ya Kilwa. Jumla ya nyumba 30 za ghorofa zimejengwa zitakazozinufaisha familia 120.  Aidha, kupitia bajeti ya maendeleo  ujenzi wa nyumba 82 za askari Polisi umeanza katika  Kambi za Polisi  Mabatini (Mwanza), Buyekera (Kagera),  Musoma  (Mara), Ludewa  (Iringa), Uwanja wa ndege (Arusha) na Finya (Kaskazini Pemba).  Utaratibu huu wa kuwajengea askari nyumba bora utawapunguzia tatizo la kuishi uraiani ili hatimaye waweze kulinda maadili ya Jeshi la Polisi.  

13. Mheshimiwa Spika, jukumu la tano ni kujenga vituo vya Polisi katika kila Tarafa nchini.  Ili kujenga vituo vya Polisi katika kila Tarafa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika mwaka 2011/2012 itashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI kwa ajili ya kujenga vituo vya daraja “C”.  Hivi sasa zipo Tarafa 215 zenye vituo vidogo na tarafa 286 bado hazina vituo hivyo. Jeshi la Polisi litatoa Askari Wakaguzi 700 ambao watapangiwa kuongoza vituo vya Polisi katika tarafa. 

14. Mheshimiwa Spika, jukumu la sita ni kuwapatia wananchi mafunzo ya Ulinzi Shirikishi ili wawe tayari kujilinda katika maeneo yao. Katika kutekeleza jukumu hili, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dhana ya Polisi Jamii. Kitengo cha Polisi Jamii Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kimesambaza vitabu vya Mpango wa Ulinzi Jirani kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kushiriki katika ulinzi huo.  Vile vile wananchi wanahamasishwa kushiriki katika ulinzi wa Polisi Jamii kwa kupitia vyombo vya habari.  Mpaka sasa vikundi 2,832 vya ulinzi shirikishi vimeanzishwa tangu mwaka 2005.  

15. Mheshimiwa Spika, jukumu la saba ni kuimarisha mafunzo ya askari wa vyombo vya ulinzi na usalama. Katika kipindi cha Julai 2010 hadi Aprili 2011 askari 14,690 kutoka Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji wamepatiwa Mafunzo.  Jumla ya askari Polisi 11,251 wamepatiwa mafunzo ya upelelezi, usimamizi wa kumbukumbu za uhalifu, uchunguzi wa makosa ya fedha haramu, na usalama barabarani.  Halikadhalika, askari 3,122 wa Magereza, 202 wa Zimamoto na Uokoaji na 115 wa Uhamiaji wamepatiwa mafunzo.

16. Mheshimiwa Spika, jukumu la nane ni kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora katika Magereza. Katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (Agricultural Seed Agency) lililima hekta 796 na kupanda mbegu bora za mahindi, mpunga, mtama, maharage, mbaazi, alizeti, ufuta, karanga, nyanya na vitunguu katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Manyara, Lindi, Mbeya, Kilimanjaro na Morogoro. Jeshi la Magereza lilivuna tani 1,618 za mbegu bora. Kwa kushirikiana na Kampuni ya ‘Highland Seed Growers Ltd’ Jeshi la Magereza pia lilizalisha mbegu bora za mahindi tani 600 katika Mikoa ya Rukwa na Ruvuma. Katika mwaka 2011/2012 Jeshi la Magereza litalima hekta 2,736 za mazao mbalimbali ili kuvuna tani 7,195 za mazao hayo. 

17. Mheshimiwa Spika, jukumu la tisa ni kutoa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi na wageni wanaoishi nchini. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa imeshapata Mkandarasi wa kutekeleza mradi huo. Kampuni iliyoshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa kutoa vitambulisho vya Taifa inaitwa ‘IRIS Corporation Behard’ kutoka Malaysia. Serikali ilitiliana saini na Kampuni hiyo mnamo tarehe 21 Aprili, 2011. Hivi sasa Mkandarasi anafanya maandalizi ya awali ya kutekeleza mkataba huo.  Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inatarajia kutoa vitambulisho vya Taifa kwa awamu ya kwanza itakapofika mwishoni mwa mwaka 2011. 

18. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa itatoa vitambulisho vya Taifa kwa Watanzania waliofikia umri wa miaka 18 na wageni wanaoishi nchini.  Jumla ya watu kati ya milioni 25 na 26 wanatarajiwa kupatiwa vitambulisho hivyo. Hivi sasa Mamlaka ya Vitambulisho imeshakamilisha taratibu za kupata viwanja vya kujenga ofisi katika Wilaya zote za Tanzania Bara isipokuwa Wilaya za Ilala na Kinondoni.  Mradi huu utagharimu shilingi bilioni 355 mpaka kumalizika kwake katika kipindi cha miaka mitano.  Mradi wa vitambulisho vya Taifa utakapomalizika utasaidia kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutoka walipa kodi 1,570,000 hadi 12,000,000, kukabiliana na tatizo la watumishi hewa Serikalini, kuwatambua wanafunzi wanaostahiki kupewa mikopo ya elimu ya juu na vyombo vya fedha,  kuimarisha usalama na kuwatambua wapiga kura halali katika daftari la kudumu la wapiga kura.  

19. Mheshimiwa Spika, jukumu la kumi ni kuimarisha vikosi vya Zimamoto na Uokoaji vyenye wataalam na zana za kisasa ili kukabiliana na majanga ya moto. Katika mwaka 2010/2011 Askari wa Zimamoto na Uokoaji 202 wamepatiwa mafunzo katika Chuo cha Magereza Kiwira, Mbeya.  Jeshi la Zimamoto limenunua magari mawili ya kuzima moto kwa ajili ya mafunzo katika Chuo cha Zimamoto na Uokoaji kilichopo Uwanja wa Ndege wa zamani wa Dar es Salaam.  

HALI YA USALAMA NA MATUKIO YA UHALIFU

20. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya nchi yetu imeendelea kuwa ya amani na utulivu.  Hata hivyo mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010 zimeanza kujitokeza dalili za uvunjifu wa amani.  Baadhi ya Viongozi wa Kisiasa wanaandaa maandamano na mikutano ya mara kwa mara. Pamoja na wanasiasa kutumia haki yao ya kidemokrasia hali hii inawanyima wananchi fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo na miradi ya kuwapunguzia umaskini. Kwa bahati mbaya viongozi wanaoamini kuwa Watanzania ni maskini sana ni hao hao wanaowatia shime watu maskini washiriki katika maandamano yasiyokuwa na tija. Hapana shaka muda unaotumika  katika  kuandaa na kushiriki maandamano haya ungetumika katika shughuli za maendeleo bila shaka Tanzania ingeweza kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa. 

21. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2010 makosa ya jinai 543,358 yaliripotiwa katika vituo vya Polisi ikilinganishwa na makosa  567,288 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hiki mwaka 2009. Makosa yanayoongoza ni wizi, uvunjaji wa majengo, unyang’anyi wa kutumia nguvu, kubaka na kupatikana na bangi. Makosa haya yanachangiwa sana na ukosefu wa ajira kwa vijana, kumomonyoka kwa maadili na tamaa ya kupata fedha haraka. Idadi ya makosa imepungua kwa asilimia 4.2.  Jeshi la Polisi linaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na uhalifu zikiwemo kuongeza idadi ya askari katika Mikoa yenye upungufu wa askari kama vile Kagera, Mara, Kigoma, Rukwa na Tabora ili kufanya doria. Jeshi la Polisi pia linashirikiana na wadau mbalimbali kukabiliana na vitendo vya uhalifu kupitia Polisi Jamii, kuimarisha utendaji kazi wa Makamanda, wakaguzi na askari na kubadilishana taarifa za kiintelijensia. 

22. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni ajali za barabarani zimekuwa zikiongezeka kwa kasi na kusababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali za wananchi.  Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2010 makosa ya usalama barabarani 384,676 yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi ikilinganishwa na makosa 359,305 yaliyoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2009. Idadi ya makosa imeongezeka kwa asilimia 7.1.  

23. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi imekusudia kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 10 katika kipindi cha mwaka 2011/2012. Ili kudhibiti ajali za barabarani Kikosi cha Usalama Barabarani kimeendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo kukamata magari mabovu na kuyaondoa barabarani, kutoa elimu ya usalama barabarani kwenye mashule na ukaguzi wa leseni za udereva. Aidha, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi imeandaa mwongozo wa madereva wanafunzi na kuusambaza kwenye vyuo vya udereva.  

24. Mheshimiwa Spika, uzoefu unaonyesha kuwa asilimia 75 ya ajali za barabarani zinasababishwa na makosa ya kibinaadam ikiwemo uzembe, ulevi, na mwendo wa kasi.  Ili kudhibiti makosa haya Jeshi la Polisi limekuwa likiwahimiza wamiliki wa mabasi ya abiria yanayokwenda Mikoani kufunga mitambo ya kutoa taarifa za mwendo (Car tracking), kuwataka madereva kuendesha magari kwa mwendo wa usalama na kukata leseni mpya. Pamoja na juhudi hizi bado ajali za barabarani zinaendelea kuwaangamiza wananchi.  Nimeliagiza Jeshi la Polisi lisisite kuwanyang’anya leseni madereva wazembe na wanaosababisha ajali.  Vile vile nimeliagiza Jeshi hilo kuwataka wamiliki na madereva wa mabasi ya abiria waweke namba za simu kwenye mabasi yao ili abiria waweze kutoa taarifa za uzembe unaofanywa na madereva kwa Jeshi la Polisi.   

25. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania lilianza kutoa leseni za elektroniki awamu ya kwanza katika vituo tisa vya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Mbeya, Dodoma, Mwanza, Ilala, Temeke na Kinondoni mwezi Oktoba, 2010. Zoezi hili kwa sasa linafanyika katika Mikoa yote ya Tanzania Bara isipokuwa katika Mkoa wa Rukwa ambako Mamlaka ya Mapato Tanzania bado haijafunga mitambo yake na Mkoa wa Manyara ambako benki ya CRDB bado haijafungua tawi. Taratibu zinafanywa ili kuwaruhusu wananchi kutumia Benki ya Posta Tanzania. Hadi tarehe 24 Mei 2011 jumla ya leseni 105,518 zimetolewa kwa madaraja mbalimbali. Hata hivyo mpaka sasa zoezi la kubadilisha leseni mpya linakwenda pole pole. Kwa hiyo nimeamua kuongeza muda wa kubadilisha leseni mpaka tarehe 31 Desemba, 2011 ili madereva ambao hawajabadilisha leseni zao wafanye hivyo haraka.  

MAPITIO YA UTEKELEZAJI  WA BAJETI YA MWAKA 2010/2011 NA MALENGO YA MWAKA 2011/2012

26. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilipangiwa kukusanya mapato ya shilingi 56,343,700,000. Hadi tarehe 30 Aprili, 2011 Wizara ilikuwa imekusanya shilingi 36,289,744,299 sawa na asilimia 64 ya lengo la mwaka.Tunatarajia kuwa baada ya hesabu za mwaka kufungwa kiwango cha makusanyo kitafikia asilimia 77. Kwa mwaka 2011/2012 Wizara imejiwekea lengo la kukusanya mapato ya shilingi bilioni 79. Ili wizara yangu iweze kufikia malengo ya ukusanyaji mapato itachukua hatua za kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji mapato katika taasisi zake na kusisitiza malipo ya huduma yafanywe kwa kutumia mabenki ili kudhibiti upotevu wa fedha. 

27. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Wizara iliidhinishiwa kutumia shilingi 446,347,481,000 kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili 2011, jumla ya shilingi 352,756,892,775 zimetumika sawa na asilimia 79 ya bajeti. Mishahara shilingi 177,689,774,286, matumizi mengineyo shilingi 161, 432,989,313 na fedha za maendeleo ni shilingi 13,634,129,176. Katika mwaka 2011/2012, Wizara imetengewa shilingi 482,394,883,000 kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. 

JESHI LA POLISI

28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Polisi limeendelea kupambana na vitendo vya uhalifu ili kuimarisha usalama wa raia na mali zao.  Jeshi hili linajitahidi kuzuia makosa, kupeleleza makosa ya jinai yaliyoripotiwa katika Vituo vya Polisi, kuwakamata  na kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wa makosa ya jinai na makosa ya usalama barabarani. 

29. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza sera ya Ulinzi Shirikishi /Polisi Jamii ili kuwawezesha wananchi kujilinda katika maeneo yao. Naziomba Mamlaka za Serikali za Mitaa  kuanzisha vikundi  vya ulinzi shirikishi katika maeneo yao.  Jeshi la Polisi linaratibu  uanzishwaji wa vikundi hivyo  na kutoa mafunzo ya Ulinzi Shirikishi kwa wananchi kupitia Halmashauri za Wilaya, Majiji, Manispaa, Miji, mitaa, vijiji na vitongoji.  

30. Mheshimiwa Spika, katika siku za hivi karibuni baadhi ya wananchi wameanza kujenga tabia ya kujichukulia sheria mikononi mwao.  Vitendo hivi vinahatarisha maisha na mali za wananchi  wasio na hatia na hata askari polisi wanaotekeleza majukumu yao. Wizara yangu inalaani vitendo hivi. Kwa kuwa Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa misingi ya utawala wa sheria, nawaomba wananchi wazingatie na kuheshimu sheria. Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo hivi.  

31.  Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na Shirikisho la Polisi la Kimataifa - Interpol, Shirikisho la Polisi la nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika  na Shirikisho la Polisi la nchi za Kusini mwa AfrikaUshirikiano huu unafanikisha ubadilishanaji taarifa za uhalifu, mafunzo, operesheni na mikutano ya Wakuu wa Majeshi na Wakuu wa Upelelezi wa nchi wanachama.  Katika mwaka 2010/11 operesheni za pamoja zilihusisha nchi za Mauritius, Zambia, Malawi,  DRC na Zimbabwe. Operesheni hizi zililenga kudhibiti wizi wa magari, biashara ya dawa za kulevya, silaha haramu na wahamiaji haramu.  Hapa nchini operesheni hizi zilifanyika katika Mikoa ya Arusha, Mbeya, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Mara, Dar es Salaam, Zanzibar na Mkoa wa Kipolisi wa Tarime-Rorya.  

Ununuzi wa Magari

32. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 jumla ya magari 281 yamenunuliwa kwa ajili ya Jeshi la Polisi. Magari hayo yalitumiwa katika kupambana na vitendo vya uhalifu na zoezi la Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2010. 

Ujenzi wa Nyumba za Makazi

33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011Jeshi la Polisi limeendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa maghorofa 30 kwenye Kambi ya Polisi Barabara ya Kilwa, maghorofa sita Kambi ya Mabatini (Mwanza), sita Musoma (Mara) na matatu Buyekera  (Kagera), nyumba 12 Ludewa (Iringa), nane Kiwanja cha Ndege Arusha na mbili Finya (Kaskazini Pemba). Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, Jeshi la Polisi litaendelea kukamilisha ujenzi wa nyumba hizi.   

Ujenzi wa Ofisi na Vituo vya Polisi

34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Polisi  liliendelea na ujenzi wa jengo la   Ofisi ya  Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai,  Dar es Salaam, majengo ya Ofisi za Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Kusini Pemba, Mara na Manyara,  Vituo vya Polisi vya Ludewa na Newala. Ujenzi wa vituo   vya  daraja “C” vya Horohoro (Tanga) na Mtambaswala (Mtwara) uko katika hatua za umaliziaji. Katika mwaka 2011/2012 Jeshi la Polisi litaendelea na ujenzi wa ofisi  hizi na kuanza ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Mkokotoni. 

Ujenzi na Ukarabati wa Vyuo

35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012 Jeshi la Polisi litaendelea na ujenzi wa Chuo cha Upelelezi Dodoma na Chuo cha Polisi Wanamaji Butimba (Mwanza). Chuo cha Polisi Wanamaji, Mwanza kinajengwa kwa gharama za Serikali ya Tanzania na vifaa pamoja na mafunzo yanatolewa kwa ushirikiano na Serikali ya Marekani. Lengo la Chuo hiki ni kuimarisha uwezo wa Polisi Wanamaji pamoja na taasisi zingine zinazosimamia sheria nchini na nchi jirani ili kukabiliana na changamoto za uhalifu katika mito, maziwa na baharini. Naishukuru Serikali  ya  Tanzania kwa kukubali kudhamini ujenzi wa chuo hiki na Serikali ya Marekani kwa kuahidi kutoa vifaa mbalimbali vya mafunzo zikiwemo boti za doria 12. Hivi sasa tayari mafunzo awamu ya kwanza yameanza na boti mbili zimeshawasili na zinafanya kazi katika Ziwa Victoria. 

Mafunzo na Ajira

36. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Polisi limetoa mafunzo mbalimbali kwa askari 11,251 na kuajiri askari wapya 2,732 kati yao 660 ni wanawake. Katika mwaka 2011/2012 Jeshi la Polisi linatarajia kutoa mafunzo kwa askari 15,000, kati yake askari 680 watapata mafunzo ya upelelezi wa makosa ya kimtandao (cyber crimes). 

Mapambano Dhidi ya UKIMWI

37. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linashirikiana na Marie Stopes (T) Ltd, ili kuandaa Sera ya UKIMWI.  Vile vile Jeshi la Polisi limeshirikiana na taasisi ya ‘Pharm Access Foundation’ ili kukarabati majengo ya zahanati katika Mikoa ya Pwani, Tanga, Lindi, Kigoma, Iringa na Hospitali ya Polisi, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam. Kutokana na juhudi hizi kiwango cha maambukizi mapya ndani ya Jeshi la Polisi kimedhibitiwa na kubaki asilimia 4.7. 

JESHI LA MAGEREZA

38. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza lina jukumu la kuwahifadhi wafungwa na mahabusu ili kuwarekebisha kitabia. Urekebishaji wa wafungwa kitabia hufanywa kwa kupitia programu za mafunzo kwa njia ya vitendo katika miradi ya kilimo, viwanda vidogovidogo, ujenzi na mafunzo ya ufundi katika Chuo cha Ufundi Magereza Ruanda (Mbeya) Gereza la Vijana Wami pamoja na utoaji ushauri nasaha kwa kuwatumia walimu wa dini na Maafisa Ustawi wa Jamii.  Lengo la programu hizi ni kuwafanya wafungwa wawe raia wema ili watakaporudi katika jamii waweze kutoa mchango katika kukuza maendeleo ya nchi yetu. 

Usafirishaji wa Mahabusu Kwenda Mahakamani

39. Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa kazi ya kuwapeleka mahabusu Mahakamani na kuwarudisha magerezani ilikuwa ikifanywa na Jeshi la Polisi siku za nyuma.  Kwa kuwa utaratibu huu ulikuwa ukiwachelewesha mahabusu kufika mahakamani, Serikali iliamua kulikabidhi jukumu hili kwa Jeshi la Magereza.  Kwa hiyo Jeshi la Magereza lilianza kutekeleza jukumu hili kuanzia Mei, 2008 kwa Mahakama zote za Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya ya Kisarawe na Mkuranga Mkoa wa Pwani. Utaratibu huu umeleta mafanikio makubwa kwa sababu mahabusu sasa hufikishwa Mahakamani kwa tarehe walizopangiwa na Mahakama.  Hali hii inasaidia kuendesha kesi haraka na hatimaye kupunguza msongamano magerezani. Katika mwaka 2011/2012 Jeshi la Magereza litaendelea kutekeleza jukumu hilo katika Wilaya zilizosalia za Mkoa wa Pwani na kuanza katika Mkoa wa Arusha. 

Programu ya Kuhifadhi Taarifa za Wafungwa

40. Mheshimiwa Spika, awamu ya kwanza ya mradi wa kuhifadhi taarifa za wafungwa nchini kwa kutumia mtandao wa kompyuta uliozinduliwa tarehe 17 Desemba, 2010 umekamilika. Awamu hii ilihusisha kufunga mitambo katika Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Ofisi ya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Chuo cha Maafisa Ukonga  na magereza ya Segerea, Ukonga na Keko. Mtandao huu umesaidia kujenga uwezo wa Jeshi la Magereza katika kutoa taarifa sahihi za wahalifu. Mradi huu umegharimu jumla ya shilingi bilioni 2.5.  

41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, Jeshi la Magereza linatarajia kuanza awamu ya pili ya mradi huu katika Mikoa tisa yenye magereza ya Ulinzi mkali kwa kuanzia na vituo vya Magereza ya  Butimba (Mwanza), Uyui (Tabora) na Isanga (Dodoma) na Ofisi za Magereza katika Mikoa hiyo. 

Kuajiri Askari

42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Magereza limeaajiri askari wapya 959 baada ya kuhitimu mafunzo ya awali ya uaskari katika Chuo cha Magereza Kiwira (Mbeya). Katika mwaka 2011/2012 Jeshi la Magereza litaajiri askari 954. 

Uimarishaji wa Magereza Yenye Ulinzi Mkali

43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Magereza limekarabati majengo na miundombinu ya Gereza lenye ulinzi mkali  Lilungu (Mtwara).  Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, ukarabati wa majengo na miundombinu utaendelea katika Magereza ya Butimba (Mwanza), Lilungu (Mtwara), Maweni (Tanga) na Isanga (Dodoma).  

Ukarabati na Ujenzi wa Mabweni ya Wafungwa

44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Magereza limefanya ukarabati wa mabweni ya wafungwa katika Magereza ya Rombo, Kambi Mkoka (Dodoma) na Meatu. Vile vile Jeshi la Magereza liliendelea na ujenzi wa  Gereza  Karatu na upanuzi wa Gereza Masasi. Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 Jeshi la Magereza litakamilisha ujenzi wa mabweni ya wafungwa katika Gereza  Karatu na  kuanza ujenzi wa  mabweni ya wafungwa katika Magereza ya Muleba na Isupilo na ujenzi wa Ofisi ya Utawala  Mbarali.  Halikadhalika, Jeshi la Magereza litakarabati Magereza ya Korogwe, Same, Kilwa, Kingurungundwa na Mahabusu Tabora. 

Ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Magereza wa Mikoa

45. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Magereza limeendelea na ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Magereza katika Mikoa ya Singida na Dar es Salaam. Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, Jeshi la Magereza  litaendelea na ujenzi huu.  

Matumizi ya Nishati Mbadala Magerezani 

46. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza linaendelea na juhudi za kutafuta nishati mbadala ya kupikia chakula cha wafungwa badala ya kuni. Mradi wa ‘biogas’ umefikia hatua nzuri ambapo mtambo wa kuzalisha ‘biogas’ katika gereza la Ukonga umekamilika kwa asilimia 100 na uzalishaji wa malighafi umefikia asilimia 60.  Mradi huu umegharimu  shilingi  827,422,380. Matumizi ya ‘biogas’ na nishati nyingine mbadala zitasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa lengo la kuhifadhi mazingira.

Ujenzi na Ukarabati wa Nyumba za Askari

47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Magereza limejenga nyumba za askari katika Magereza ya Karatu na Chato. Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, Jeshi la Magereza litakamilisha ujenzi wa jengo la ghorofa la kuishi askari Mkoani Iringa pamoja na ukarabati wa nyumba za askari katika Magereza ya Mang’ola na Wami Kuu.  

Uimarishaji wa Mifumo ya Majisafi na Majitaka

48. Mheshimiwa Spika, hivi sasa Jeshi la Magereza linaendelea kuboresha miundombinu ya majisafi na majitaka. Katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Magereza lilikarabati miundombinu ya majitaka katika magereza ya King’ang’a, Msalato, Kihonda, Tunduru, Ngwala na Handeni. Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 Jeshi la Magereza litakarabati  mifumo ya majisafi na majitaka katika magereza ya King’ang’a, Ukonga, Same, Kambi ya Chumvi (Mtwara), Mkwaya, Mbinga na Mang’ola. 

Upimaji wa Maeneo ya Magereza

49. Mheshimiwa Spika, mpaka sasa maeneo mengi ya Jeshi la Magereza bado hayajapimwa. Katika mwaka wa fedha wa 2010/2011, Jeshi la Magereza lilianza mchakato wa kupima Gereza la Ubena. Katika mwaka 2011/2012, Jeshi la Magereza litapima maeneo ya magereza ya Muleba, Urambo, Kibondo, Mkuza, Bunda, Newala, Mbinga, Ngudu na Kambi Kizwite.  

Shirika la Magereza

50. Mheshimiwa Spika, Shirika la Magereza limeendelea na shughuli za uzalishaji mali katika viwanda vidogo vidogo. Katika mwaka 2010/2011, Shirika limeendelea kutengeneza samani za aina mbalimbali. Shirika pia lilitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi kupitia Kikosi cha Ujenzi cha Jeshi la Magereza kwa kujenga nyumba za askari Polisi katika Kambi ya Polisi, Barabara ya Kilwa, ukarabati wa Chuo cha Polisi Kidatu na jengo la Wizara ya Katiba na Sheria.  Katika mwaka 2011/2012 Jeshi la Magereza linatarajia kuongeza shughuli za uzalishaji mali. 

Kilimo cha Umwagiliaji

51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Jeshi la Magereza liliandaa taratibu za ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji katika Magereza ya Idete (Morogoro) na Kitengule (Kagera). Hivi sasa miradi hiyo inafanyiwa tathmini ya kimazingira na usanifu wa michoro. Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, Jeshi la Magereza litaanza rasmi ujenzi wa miundombinu hiyo ya umwagiliaji katika magereza ya Idete na Kitengule. 

HUDUMA KWA JAMII

52. Mheshimiwa Spika, Programu ya Huduma kwa Jamii ilianza rasmi mwaka 2005 kama njia mojawapo ya adhabu mbadala ya kifungo gerezani.  Programu hii inatekelezwa katika Mikoa 12 ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Iringa, Kagera, Mara na Shinyanga. Katika kipindi cha Julai, 2010 hadi Aprili, 2011 jumla ya wafungwa 1,026 wamefaidika na programu hii ambapo wanaume ni 863 na wanawake 163. Wafungwa hao hutumikia vifungo vyao nje ya magereza kwa kufanya kazi bila ya malipo katika taasisi za umma.  

JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

53. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea kutoa huduma za kuzima moto na uokoaji. Huduma hizo zimetolewa na Vikosi vya Zimamoto na Uokoaji vya Serikali, Makampuni Binafsi na Halmashauri za Wilaya. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea na zoezi la ukaguzi wa tahadhari na kinga dhidi ya moto katika maeneo mbalimbali na kwenye vyombo vya usafiri. Katika kipindi cha Julai 2010 hadi Aprili 2011 jumla ya maeneo 9,051 yalifanyiwa ukaguzi.  Katika mwaka 2011/2012 Jeshi la Zimamoto litafanya ukaguzi katika maeneo 35,000. 

54. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, limewapatia mafunzo askari 202 katika Chuo cha Magereza Kiwira (Mbeya).  Aidha, katika kuimarisha mafunzo kwenye Chuo cha Zimamoto na Uokoaji kilichopo Uwanja wa Ndege wa zamani wa Dar es Salaam, Jeshi la Zimamoto limenunua magari mawili ya kuzimia moto ambayo yatatumika katika mafunzo hayo.   

IDARA YA UHAMIAJI55. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2010 hadi Aprili, 2011, jumla ya wageni 625,308 waliingia nchini, ikilinganishwa na wageni 664,037 walioingia nchini katika kipindi kama hiki mwaka jana. Wageni 627,884 walitoka nje ya nchi ikilinganishwa na wageni 638,376 waliotoka nchini katika kipindi kama hiki mwaka uliopita. Idadi ya wageni walioingia imepungua kwa wastani wa watu 38,729 sawa na asilimia 5.8. Kushuka kwa idadi hiii kulisababishwa na kudorora kwa uchumi duniani.  

Wageni Waliopatiwa Hati za Ukaazi

56. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 wageni 12,563 walipewa hati za ukaazi nchini ikilinganishwa na wageni 10,890 waliopewa hati hizo katika kipindi kama hiki mwaka jana. Idadi ya hati zilizotolewa imeongezeka kwa hati 1,673 sawa na asilimia 15.4. Hali hii inatokana na kuimarika kwa hali ya uchumi duniani pamoja na kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji nchini.  

Wageni Waliopatiwa Uraia wa Tanzania

57. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa uraia wa Tanzania kwa wageni 90 waliotimiza masharti. Wageni waliopata uraia wa Tanzania wanatoka katika nchi za India, Somalia, Rwanda, Kenya, Uingereza, Uganda, Burundi, Lebanon, Finland, Yemen, Pakistan, Nigeria, Italia, Sudan, Zambia, Bangladesh na China.  Hivi sasa Wizara yangu inaandaa Sera ya uraia ili iweze kudhibiti kiwango cha watu wanaopewa uraia wa Tanzania.  Wizara itaweka masharti na idadi ya watu wanaoweza kupewa uraia wa Tanzania katika kila mwaka. 

Watanzania Waliopatiwa Uraia wa Mataifa Mengine

58.  Mheshimiwa Spika, Watanzania 32 walipata uraia wa mataifa mengine ya Kenya, Ujerumani, Norway, Denmark, Zambia, Uingereza, Australia, Namibia, Sweden, China  na Singapore.  Kwa kuwa Tanzania haina utaratibu wa kuwa na uraia wa nchi mbili, watu hawa wamepoteza uraia wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995.  

Pasipoti Zilizotolewa

59. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji ilitoa jumla ya pasipoti 36,818 katika kipindi cha 2010/2011. Kati ya hizo 35,546 ni za kawaida, 813  za Afrika Mashariki, 360 za kibalozi na 99 za kiutumishi, ikilinganishwa na pasipoti 39,241, ambapo pasipoti 37,664 za kawaida, 1,269 za Afrika Mashariki, 209 za kibalozi na 99 za kiutumishi zilizotolewa katika kipindi kama hiki mwaka jana.   

Misako na Doria

60. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2010 hadi Aprili, 2011 Idara iliendesha doria na misako yenye lengo la kudhibiti wageni haramu nchini. Jumla ya wageni 3,339 walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ikilinganishwa na wageni 2,272 waliokamatwa katika kipindi kama hiki mwaka jana. Miongoni mwa idadi ya wahamiaji haramu waliokamatwa 1,371 walitokea Somalia na Ethiopia.  Wahamiaji haramu 551 wamekwisharejeshwa kwao na 820 wapo katika magereza mbalimbali hapa nchini. Kwa kuwa tatizo la wahamiaji haramu limekithiri, Idara ya Uhamiaji  itaongeza juhudi katika kukabiliana na tatizo hili kwa kuongeza vitendea kazi, kutoa elimu kwa umma na mafunzo ya weledi kwa watumishi, kushirikiana na vyombo vingine vya  ulinzi na usalama pamoja na kuwashirikisha wananchi katika maeneo yao, kwani jukumu la ulinzi na usalama wa Taifa letu ni la kila mwananchi. 

Ujenzi na Ukarabati wa Nyumba na Ofisi

61. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, ujenzi wa nyumba za makazi katika Kituo cha Mkenda Nakawale mpakani mwa Tanzania na Msumbiji umekamilika. Ujenzi wa Afisi ya Uhamiaji Zanzibar upo katika hatua za mwisho na ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga umeanza. Ukarabati wa nyumba ulifanyika katika vituo vya Uhamiaji vya Kyela, Sirari, Manyovu na Mabamba.  Ukarabati wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Rukwa nao umekamilika na ukarabati wa nyumba za watumishi wa Uhamiaji Kibaha bado unaendelea.  Katika mwaka 2011/2012, Idara ya Uhamiaji itakamilisha ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga na kuanza ujenzi wa Ofisi za Uhamiaji katika Mikoa ya Ruvuma, Manyara na Morogoro. Idara pia itafanya ukarabati wa majengo ya Ofisi na nyumba za kuishi Igoma (Mwanza), Horohoro (Tanga) na mabweni ya Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda, Moshi. 

Ajira na Mafunzo

62. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, watumishi wapya 115 wameajiriwa na watumishi 105 wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu ndani na nje ya nchi. Katika mwaka 2011/2012, Idara itatoa mafunzo kwa watumishi 148. Mafunzo haya yatawasaidia wafanyakazi kuongeza ujuzi na utaalamu ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi. 

Ununuzi wa Vyombo vya Usafiri

63. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Idara imenunua pikipiki 42 ili kuwapatia wafanyakazi vyombo vya usafiri.  Katika mwaka 2011/2012 Idara ya Uhamiaji itanunua magari 9 na pikipiki 5 kwa lengo la kuwaondolea watumishi matatizo ya usafiri. 

Mapambano Dhidi ya KIMWI

64. Mheshimiwa Spika, katika kupambana na maambukizi ya UKIMWI mahali pa kazi Idara inaendelea kutoa elimu kwa watumishi na familia zao katika Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Rukwa na Mbeya. Pia Idara iliendesha zoezi la kuhamasisha kupima afya ambapo watumishi 318 pamoja na familia zao walipima virusi vya UKIMWI katika Mikoa hiyo. Vipeperushi vimesambazwa katika vituo vya kuingilia nchini kwa lengo la kutoa elimu juu ya janga la ukimwi kwa wasafiri wanaoingia na kutoka nchini.  

MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA

65. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa iliajiri wafanyakazi 105. Katika mwaka 2011/2012 Mamlaka itawapatia vitambulisho wafanyakazi wa Serikali, wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu pamoja na wafanyabiashara katika awamu ya kwanza. Mradi huu utakapomalizika utagharimu shilingi bilioni 355 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wilaya, malipo ya mkandarasi na mshauri.   

IDARA YA WAKIMBIZI

66. Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Aprili, 2011 walikuwepo wakimbizi 107,513 nchini.  Kati ya idadi hiyo kuna Warundi 45,017, Wakongo 60,735, Wasomali 1,500 na 261 wakimbizi wa mataifa mbalimbali.  Katika kipindi cha Julai, 2010 hadi Aprili, 2011 jumla ya wakimbizi 690 walirejea kwao ambapo Warundi ni 669 na Wakongo 21. Katika mwaka 2011/2012 Idara inatarajia kuwarudisha wakimbizi 38,800 walioko katika kambi ya Mtabila, na hatimaye kuifunga kambi hiyo.  Kufuatia mkutano wa Pande Tatu, uliojumuisha nchi za Tanzania, Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) uliofanyika hapa Dar es Salaam tarehe 25 Mei, 2011, pande zote tatu zilikubaliana kuweka ratiba ya kuwarudisha wakimbizi 10,000 kila mwezi, kuanzia mwezi Septemba, 2011.Wizara yangu inatarajia kuifunga Kambi hiyo mwaka 2012.  Kwa upande wa Wakimbizi wa Kongo (DRC), jitihada za kuhimiza urejeaji pia zinaendelea.  Wizara yangu inaendelea na mazungumzo na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) kuhusu utekelezaji wa mpango wa kuwarudisha wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwa hali ya usalama imeimarika katika eneo la Kivu. Wizara yangu inatarajia kuwa mazungumzo hayo yatasaidia kufikia mwafaka wa kuwarudisha wakimbizi wa DRC makwao mwaka 2012. 

IDARA YA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO

67. Mheshimiwa Spika, idara hii inaratibu malalamiko ya wananchi na askari dhidi ya Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji ili kuboresha utendaji wa vyombo hivyo. Katika mwaka 2010/2011, Idara ilipokea jumla ya malalamiko 300 yakiwemo 150 yanayohusu Jeshi la Polisi dhidi ya raia hususan ubambikizaji wa kesi na ucheleweshaji wa upelelezi wa makosa ya jinai. Aidha, yapo malalamiko ya kutotendewa haki ya askari wa vyeo vya chini wa Jeshi la Polisi na Magereza wanaolalamika kuwa walifukuzwa kazi kinyume na taratibu.  

68. Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu idara hii imekuwa ikifanya kazi bila ya kuwa na sheria maalum. Kutokana na sababu hiyo maamuzi yanayofanywa na idara hukosa nguvu ya kisheria. Katika mwaka 2010/2011 Wizara iliendelea na mchakato wa kutunga sheria itakayosimamia utendaji kazi wa idara hii. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2011/2012. 

USAJILI WA VYAMA VYA KIJAMII

69. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011 idara ya usajili wa vyama vya kijamii ilisajili vyama 257. Hivi sasa kuna vyama vilivyosajiliwa 6,266. Idara pia imekamilisha uwekaji mfumo wa kutunza kumbukumbu za usajili wa vyama. Kazi hii ilifanywa kwa ushirikiano na Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Katika mwaka 2011/2012, Idara itaendelea kuhakiki utendaji wa vyama hivyo, kutoa elimu kwa vyama juu ya wajibu wao wa kutoa taarifa mbalimbali za vyama na kulipa ada ya kila mwaka kwa mujibu wa Sheria ya Vyama Sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Vile vile idara itatafuta suluhu ya migogoro ya vyama kadri itakavyojitokeza.  

SHUKURANI

70. Mheshimiwa Spika, natoa shukurani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Edward Lowassa, Mbunge wa Monduli kwa kuyapitia na kuyachambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2011/2012. Ushauri wa Kamati hiyo utaisaidia wizara yangu kuimarisha utendaji wa majukumu yake. 71.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukurani za pekee kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Balozi Khamis Suedi Kagasheki, Mbunge wa Bukoba Mjini, Katibu Mkuu Ndugu Mbarak Abdulwakil, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Mwamini Malemi, Inspekta Jenerali wa Polisi Ndugu Saidi Mwema, Kamishna Mkuu wa Magereza Ndugu Augustino Nanyaro, Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Ndugu MatwaniKapamba, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Ndugu Magnus Ulungi na wakuu wote wa Idara na Vitengo, Makamanda, askari pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambao wamefanikisha maandalizi ya hotuba yangu.  

72. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukurani kwa nchi wahisani ikiwemo China, Marekani, Misri na  Saudi Arabia, taasisi za INTERPOL, IOM, Pharm Acces, Marie Stopes, UNHCR, UNDP, UNICEF na  WFP kwa misaada yao ambayo imeongeza uwezo wa kiutendaji katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 

73. Mheshimiwa Spika, mwisho ingawa sio mwisho kwa umuhimu ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa maelekezo mbalimbali anayoyatoa kwa Wizara yangu. Halikadhalika namshukuru Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu kwa kuhimiza utekelezaji wa majukumu ya Wizara yangu. 

MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2011/2012

74. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naliomba Bunge lako Tukufu lipitishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2011/2012 ya shilingi 482,394,883,000 kama ifuatavyo:- 

Fungu 14: Jeshi la Zimamoto na Uokoaji

Matumizi Mengineyo shilingi                        1,950,152,000

Mishahara shilingi                                       1,075,840,000

Maendeleo shilingi                                                    0.00

Jumla shilingi                                          3,025,992,000 

Fungu 28: Jeshi la Polisi

Matumizi Mengineyo shilingi                    126,749,350,000

Mishahara shilingi                                   149,395,114,000

Maendeleo shilingi                                      7,494,169,000

Jumla shilingi                                      283,638,633,000 

Fungu 29: Jeshi la Magereza

Matumizi Mengineyo shilingi                         44,277,003,000

Mishahara shilingi                                        60,010,016,000

Maendeleo shilingi                                         4,563,212,000

Jumla shilingi                                          108,850,231,000  

Fungu 51: Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Matumizi Mengineyo shilingi                           2,793,916,000

Mishahara shilingi                                           1,871,114,000

Maendeleo shilingi                                          2,199,400,000

Jumla shilingi                                               6,864,430,000     

Fungu 93: Idara ya Uhamiaj

Matumizi Mengineyo shilingi                           35,073,444,000

Mishahara shilingi                                          18,133,486,000

Maendeleo shilingi                                         26,808,667,000

Jumla shilingi                                              80,015,597,000 

75. Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. 

76. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja