|
|
|
|
HOTUBA YA MHESHIMIWA LAWRENCE KEGO MASHA (MB.), WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KWA MWAKA 2009/2011 UTANGULIZI Hoja 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu, baada ya kuzingatia taarifa iliyowasilishwa mapema leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, likubali kupokea, kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha wa 2009/2010. Rambirambi 2. Mheshimiwa Spika, naomba kuungana na Wabunge wenzangu katika kutoa rambirambi zangu kwa familia na wananchi wa majimbo matatu ambayo yaliwapoteza Wabunge wao katika mwaka wa fedha wa 2008/2009. Majimbo hayo ni ya Tarime, Mbeya Vijijini na Busanda kwa kuwapoteza waliokuwa Wabunge wenzetu Waheshimiwa marehemu Chacha Wangwe, Richard Said Nyaulawa na Kabuzi Faustine Rwilomba. Namwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi. Amina. Pole 3. Mheshimiwa Spika, nawapa pole wananchi wa Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam kwa tukio la kusikitisha lililotokea tarehe 29 Aprili, 2009 la milipuko ya mabomu yaliyokuwa yamehifadhiwa katika ghala la silaha katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 20 na zaidi ya kaya 7,000 kukosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuharibiwa na mabomu hayo. 4. Mheshimiwa Spika, maafa mengi yametokea zikiwemo ajali za barabarani, migodini, meli na treni ambazo zimeendelea kupoteza maisha ya wananchi. Nachukua nafasi hii kuwapa pole ndugu na jamaa wa marehemu na waathirika wote wa maafa hayo. Pongezi 5. Mheshimiwa Spika, nakupongeza wewe binafsi, Naibu wako, Wenyeviti wetu ndani ya Bunge na wale wa Kamati za Bunge pamoja na wasaidizi wao chini ya uongozi wa Katibu wa Bunge kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kusimamia uendeshaji wa shughuli za Bunge. Nawapongeza pia Wabunge wenzangu wote kwa michango yao ndani na nje ya Bunge ambayo imelenga kulinufaisha taifa letu. 6. Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha na Uchumi kwa hotuba zao walizozitoa mapema katika mkutano huu wa 16 wa Bunge ambazo pamoja na mambo mengine zimetoa mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2009/2010 na mwelekeo wa bajeti na hali ya uchumi kwa jumla kwa mwaka 2009/2010. Dira 7. Mheshimiwa Spika, dira ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kutoa huduma bora katika kudumisha amani, utulivu na umoja nchini. Dhima 8. Mheshimiwa Spika, dhima ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, kuhifadhi na kuwarekebisha wafungwa, kudhibiti uingiaji na utokaji nchini wa raia na wageni, kutoa huduma za zimamoto na uokoaji na kuwahudumia wakimbizi waliopo nchini. MAELEKEZO YA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2005 NA UTEKELEZAJI WAKE 9. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina majukumu 13. Ningependa kueleza majukumu hayo pamoja na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wake kama ifuatavyo:- 10. Mheshimiwa Spika, jukumu la kwanza ni kuimarisha usalama migodini. Jeshi la Polisi limeendelea kutoa ulinzi kwa kufanya operesheni, misako na doria kwenye maeneo ya uwekezaji ikiwemo migodi hususan katika Mikoa ambayo imekuwa na migogoro mingi. Hadi sasa askari wetu bado wanalinda mgodi wa Buhemba Mkoani Mara. 11. Mheshimiwa Spika, jukumu la pili ni kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa kuliongezea utaalam na zana ili upelelezi wa kesi ukamilike haraka hivyo kupunguza muda wa mahabusu kukaa magerezani. Kama hatua ya utekelezaji wa jukumu hilo maofisa na askari 480 walishiriki katika mafunzo mbalimbali kuhusu taaluma ya upelelezi. Mafunzo hayo yalitolewa kwa lengo la kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika upelelezi. Aidha, askari wapya 205 walipata mafunzo ya msingi kuhusu upelelezi. 12. Mheshimiwa Spika, jukumu la tatu ni kuendelea kupunguza msongamano magerezani. Hivi sasa magereza yetu yana uwezo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu 27,653. Kwa kukarabati na kupanua magereza yaliyopo na kujenga magereza mapya na mabweni ya wafungwa katika vituo mbalimbali, Serikali imeongeza uwezo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu kwa asilimia 22 kutoka wafungwa na mahabusu 22,669 mwaka 2006 hadi kufikia 27,653 hivi sasa. Hata hivyo, bado msongamano upo, na juhudi za kupunguza zaidi msongamano zinaendelea kupitia taratibu za Parole na kifungo cha nje. Tarehe 1 Aprili, 2009 kulikuwa na wafungwa na mahabusu 41,109 katika magereza yote nchini. Kati ya hao 20,360 walikuwa ni wafungwa, na 20,749 ni mahabusu. 13. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2008 wafungwa 78 waliachiliwa kwa utaratibu wa Parole. Hata hivyo, idadi ya wafungwa wanaoachiliwa kwa utaratibu huu imeendelea kuwa ndogo kutokana na kwamba Sheria ya Bodi za Parole ya mwaka 1994 haiwaruhusu wafungwa wanaofanya makosa makubwa kuachiliwa. Wizara ipo katika mchakato wa kuwasilisha Serikalini mapendekezo ya kuifanyia marekebisho sheria hii kwa lengo la kupanua wigo wake. 14. Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Desemba, 2008 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa msamaha kwa wafungwa 7,553 wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 47 ya Uhuru. Rais pia alitoa msamaha kwa wafungwa 3,247 tarehe 26 Aprili, 2009 wakati wa kuadhimisha sherehe za miaka 45 ya Muungano. 15. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2008 hadi Aprili, 2009 jumla ya wafungwa 664 walitolewa gerezani ili watumikie kifungo cha nje chini ya usimamizi wa Halmashauri za Wilaya kwa mujibu wa Sheria ya Magereza. 16. Mheshimiwa Spika, jukumu la nne ni kushughulikia kwa ufanisi malalamiko ya wananchi ya kero ya rushwa ndani ya Jeshi la Polisi. Hatua mbalimbali zimechukuliwa dhidi ya askari waliobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa. Askari 15 wamefukuzwa kazi na baadhi kesi zao zinaendelea katika Mahakama ya kijeshi na Mahakama za Jinai. Aidha, Wizara imeunda idara maalum inayoshughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya vyombo vyake likiwemo Jeshi la Polisi. Katika mwaka huu wa fedha, idara inatarajia kuwa na sheria kwa lengo la kuipa nguvu ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. 17. Mheshimiwa Spika, jukumu la tano ni kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuviongezea uwezo kitaaluma na zana za kisasa. Wizara imeweza kutoa mafunzo katika taaluma za upelelezi, intelijensia, usimamizi wa kumbukumbu za uhalifu, uchunguzi wa makosa yahusuyo fedha haramu, na uendeshaji wa magereza, na shughuli za zimamoto, uokoaji na uhamiaji. Mafunzo hayo yametolewa kwa watumishi wa Polisi 8,651, Magereza 1,671, Zimamoto na Uokoaji 60 na Uhamiaji 374. Wizara imekamilisha ukarabati wa majengo na ufungaji wa kompyuta katika Chuo cha Mafunzo ya Uhamiaji Mjini Moshi, na imekamilisha maabara ya uchunguzi wa nyaraka ambayo imepatiwa msaada wa vifaa maalum toka Uholanzi. Chuo hicho kilizinduliwa rasmi tarehe 12 Desemba 2008 na mafunzo ya uhamiaji yameanza kutolewa kwa askari. Wizara itaendelea kuimarisha vyombo vyake vya ulinzi na usalama kwa kuvipatia zana na vifaa vya kisasa. itdelea kuiarisha ombo ke vya zi na usalama kwa kuvipatia zana na vifaa vya kisasa zikiwemo boti za 18. Mheshimiwa Spika, jukumu la sita ni kuwahamasisha wananchi kushiriki katika ulinzi wa maeneo yao na kuhakikisha usalama wao na mali zao. Katika kutekeleza jukumu hili, Makamanda wa Polisi Mikoa na Wakuu wa Polisi Wilaya na vituo wameendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dhana ya Polisi Jamii katika maeneo yao. Aidha, Kitengo cha Polisi Jamii Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kimesambaza machapisho mbalimbali kama vile vitabu vya Mpango wa Ulinzi Jirani na Safiri Salama Tanzania na kitabu cha Falsafa ya Polisi Jamii/Ulinzi Shirikishi, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki katika ulinzi. Vikundi 1,888 vya ulinzi shirikishi vimeanzishwa tangu mwaka 2005. Aidha, elimu ya kuhamasisha wananchi inaendelea kutolewa kupitia vipindi vya redio na runinga. Nashukuru kwa ushirikiano na moyo unaotolewa na wananchi katika kuanzisha vikundi vya kujilinda katika maeneo mbalimbali nchini. 19. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa askari wake. Katika taarifa ya programu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ya Research and Education for Democracy in Tanzania - REDET ya mwezi Aprili, 2009 Jeshi la Polisi limetajwa kuwa ni mojawapo ya taasisi za Serikali ambazo wananchi kwa ujumla wanaridhika na utendaji wake wa kazi. Kituo cha Haki za Binadamu katika taarifa yake ya mwaka 2008 pia kilielezea kwamba utendaji wa Jeshi la Polisi unaendelea kuboreshwa kwa kuanza kufanya kazi kwa kuzingatia miiko ya kitaaluma. 20. Mheshimiwa Spika, jukumu la saba la Wizara katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni kuvijengea mazingira mazuri vyombo vya ulinzi na usalama, na kutatua matatizo ya makazi na maslahi ya watumishi wake. Katika mwaka 2008/2009 Wizara imeendelea na ujenzi wa ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, upanuzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Wizara pamoja na Ofisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar. Wizara imeendelea pia na ukarabati wa nyumba, vituo, ofisi na mabweni ya wafungwa katika vituo mbalimbali. Kupitia udhamini wa Serikali, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) unatekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba za askari Polisi Dar es Salaam na Zanzibar ambapo ujenzi upo katika hatua za mwisho. 21. Mheshimiwa Spika, ninayo furaha kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeamua kuongeza posho mbalimbali za askari wa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kiwango cha kuridhisha. Lengo la nyongeza hii ni kuongeza mori wa utendaji. Ni matarajio yangu kuwa nyongeza ya posho hizi na maboresho ya makazi yanayoendelea yatawapa askari nafasi nzuri zaidi ya kuongeza ufanisi katika utendaji. 22. Mheshimiwa Spika, jukumu la nane ni kuongeza uwezo wa taifa wa kupambana na ujambazi na kuzagaa kwa silaha ndogondogo. Katika kukabiliana na uhalifu ukiwemo ujambazi, Jeshi la Polisi limeendelea kuimarisha Kitengo cha Intelijensia kwa kukipatia mafunzo na vitendea kazi. Doria za kutambua maficho ya wahalifu zimefanyika, ulinzi katika maeneo ya mipakani umeimarishwa kwa kuongeza idadi ya askari na kufanya operesheni za kudumu, na mafunzo ya utayari wa kukabiliana na matukio ya uhalifu yametolewa kwa askari. Kupitia mpango wa Polisi Jamii, Jeshi la Polisi limeweza kupata taarifa sahihi kutoka kwa raia wema ambazo ziliwezesha kuzima uhalifu na pale ulipotokea watuhumiwa kuweza kukamatwa. Kikosi Kazi cha Taifa kilichoundwa mwaka 2006 kukabiliana na hali ya kutisha ya ujambazi iliyokuwa wakati huo, kimeendelea kukabiliana na uhalifu kwa kuendesha upelelezi wa matukio makubwa ya uhalifu na kufuatilia mwenendo wa uhalifu nchini na kuchukua hatua. 23. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kuhakiki umiliki wa silaha ndogondogo ambapo katika kipindi cha Julai, 2008 hadi Mei, 2009 kumbukumbu za silaha 10,643 zimeingizwa kwenye database ya silaha. Aidha, Jeshi la Polisi liliendesha misako na operesheni za kusaka silaha, na silaha 424 na risasi 4,026 zilibainika kumilikiwa kinyume cha sheria na kukamatwa. Wizara imeandaa mapendekezo ya kuwasilishwa Serikalini ya kutunga sheria ambayo itasimamia na kudhibiti umiliki na matumizi ya silaha ndogondogo hapa nchini. 24. Mheshimiwa Spika, jukumu la tisa ni kuandaa Sera ya Uhamiaji yenye kubainisha masuala ya uraia na ukaazi katika mazingira ya kuelekea ushirikiano katika SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mchakato wa kuandaa sera hii ulikwishaanza mwaka 2007 na rasimu yake kujadiliwa na wadau mbalimbali. Wadau walishauri kuwa ni vyema majadiliano yanayoendelea katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu free movement of persons na majadiliano ya UNIVISA katika Jumuiya ya SADC yazingatiwe katika sera hiyo. Majadiliano hayo bado yanaendelea. Hivyo, sera hii itakamilishwa baada ya majadiliano hayo kukamilika. 25. Mheshimiwa Spika, jukumu la kumi ni kuanzisha na kutoa vitambulisho vya taifa. Mamlaka ya kusimamia na kuratibu utoaji wa vitambulisho - NIDA iliundwa na Mheshimiwa Rais kupitia hati maalum iliyotolewa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watendaji wa Mamlaka hiyo wameajiriwa, na Kamati ya Uongozi imeshateuliwa na kuanza kazi. Wizara imekamilisha hatua ya kwanza ya kumpata mkandarasi ambaye ataweka mfumo wa kutunza taarifa za watu watakaopewa vitambulisho. Hivi sasa maandalizi kwa ajili ya utoaji zabuni ya vitambulisho vya taifa yanaendelea sambamba na maandalizi ya miradi ya majaribio (pilot projects) ambayo itaanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha wa 2009/2010. 26. Mheshimiwa Spika, naomba kuwathibitishia Watanzania kupitia Bunge lako Tukufu kwamba mradi wa vitambulisho utakamilika kwa kufuata sheria na taratibu, bila mizengwe, kwa uwazi unaostahili na bila upendeleo. 27. Mheshimiwa Spika, jukumu la kumi na moja ni kuongeza kasi ya kuwarejesha wakimbizi kwao. Utekelezaji wa jukumu hilo umekuwa na mafanikio. Kati ya tarehe 1 Julai, 2008 na tarehe 30 Aprili, 2009 wakimbizi 69,687 walirejea kwao kwa hiari. Kati yao, wakimbizi 55,399 wamerejea nchini Burundi, na 14,288 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC ). 28. Mheshimiwa Spika, tangu zoezi la kuwarejesha wakimbizi katika nchi zao za asili lilipozinduliwa mwezi Machi, 2002 hadi kufikia mwezi Aprili, 2009 jumla ya wakimbizi 390,599 walirejea nchini Burundi. Aidha, hadi kufikia mwezi Machi, 2009 wakimbizi 65,418 toka DRC waliokuwepo nchini walirejea kwao. 29. Mheshimiwa Spika, jukumu la kumi na mbili ni kuendeleza kampeni ya upandaji miti. Katika mwaka wa fedha wa 2008/2009, Jeshi la Magereza liliendelea kuboresha mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yake kote nchini. Siku ya upandaji miti kitaifa, tarehe 1 Januari, 2009, jumla ya miti 41,610 ilipandwa katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa yamepata mvua. Mradi wa kupanda miti kwenye eneo la jumla ya ekari 3,000 katika Magereza ya Idete-Morogoro, Isupilo-Iringa na Msalato- Dodoma, ambao unafadhiliwa na NORAD kwa ushirikiano na Wizara ya Maliasili na Utalii, unaendelea vizuri. Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2009 jumla ya miti 742,092 ilikuwa imepandwa kwenye eneo la ekari 1,029. Mashamba mengine ya miti yalianzishwa katika magereza 10 katika Mikoa ya Mwanza, Singida, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Kilimanjaro, Rukwa na Mbeya. Hadi sasa idadi ya miti yote iliyopandwa ni zaidi ya 3.8 milioni. 30. Mheshimiwa Spika, jukumu la kumi na tatu na la mwisho la Wizara katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ni kuendeleza vita dhidi ya dawa za kulevya ili kuwakinga watoto wasiathirike na dawa hizo. Tatizo la dawa za kulevya limeendelea kuwa changamoto siyo kwa nchi yetu tu, bali kwa nchi nyingi duniani. Utandawazi, kukua kwa sayansi na teknolojia, kuongezeka kwa maingiliano ya watu duniani na upana wa mipaka ya nchi yetu vyote vimechangia hali hii. Kati ya Julai, 2008 hadi Aprili, 2009 Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola lilikamata watuhumiwa 514 na kilo 5 na gramu 331 za dawa za kulevya za viwandani. Kilo 67,624 za bhangi na kilo 8,606 za mirungi vilevile zilikamatwa, na watuhumiwa 6,501 walikamatwa na kufikishwa Mahakamani. HALI YA USALAMA NCHINI NA CHANGAMOTO ZILIZOPO 31. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ulinzi na usalama. Aidha, ushauri uliotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama umesaidia sana katika kuimarisha utendaji wa shughuli za Wizara. 32. Mheshimiwa Spika, tathmini ya hali ya usalama nchini inatokana na takwimu zinazotokana na taarifa za vyombo vya Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto na Uokoaji. Kwa ujumla hali ya amani na utulivu nchini imeendelea kuwa ya kuridhisha licha ya kuwepo kwa baadhi ya makosa kama vile mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliyoonekana kutishia usalama wa raia na mali zao. 33. Mheshimiwa Spika, napenda kuvishukuru vyombo vilivyo chini ya Wizara vya Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto na Uokoaji kwa ushirikiano wao na vyombo vingine vya dola kwa kutoa mchango mkubwa katika kudumisha amani na utulivu nchini katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2008/2009 pamoja na changamoto zinazowakabili zikiwemo ufinyu wa bajeti, kuongezeka kwa mbinu za uhalifu, upungufu wa askari, uhaba wa vitendea kazi, uhaba na uduni wa makazi na ofisi, msongamano magerezani, majanga mbalimbali na uhamiaji haramu. 34. Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo zinaonyesha makosa ya jinai 506,030 yaliripotiwa katika vituo vya Polisi nchini katika mwaka 2008 ikilinganishwa na makosa 509,462 yaliyoripotiwa mwaka 2007. Idadi ya makosa ilipungua kwa kiasi cha makosa 3,432 sawa na asilimia 0.7. Jeshi la Polisi limeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na uhalifu zikiwemo kuendesha mafunzo ya utayari kwa maofisa na askari, kuongeza nguvu ya rasilimali watu katika Mikoa yenye upungufu wa askari mfano Kagera, Mara, Kigoma, Rukwa na Tabora, kufanya doria za kutambua maficho ya wahalifu na kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kukabiliana na uhalifu. 35. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi lina upungufu mkubwa wa nguvu kazi kwani idadi inayokubalika kimataifa ni askari mmoja kwa watu 450 (1:450), wenzetu wa Kenya wana uwiano wa askari mmoja kwa watu 821 (1:821), Tanzania ni askari mmoja kwa watu 1,300 (1:1,300). Hali hii inafanya maeneo mengine kutofikiwa na huduma ya Polisi. 36. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa makosa ya usalama barabarani, mwaka 2008 makosa yaliyoripotiwa Polisi ni 229,451 ikilinganishwa na makosa 230,751 yaliyoripotiwa mwaka 2007. Idadi ya makosa ilipungua kwa kiasi cha makosa 1,300 sawa na asilimia 0.6. Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na wadau wengine kimeendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo operesheni za kukamata magari mabovu na kuyaondoa barabarani, kubaini mtandao wa kundi linalotoa leseni za udereva za bandia, kutoa elimu ya usalama barabarani kwenye mashule, ukaguzi wa leseni za udereva, magari na shule za udereva. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2008/2009 NA MALENGO YA MWAKA 2009/2010 Mapato 37. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika mwaka 2008/09 ilipangiwa kukusanya maduhuli ya Serikali ya jumla ya shilingi 30 bilioni. Hadi tarehe 30 Aprili, 2009 Wizara ilikuwa imekusanya shilingi 28.8 bilioni sawa na asilimia 96 ya lengo la mwaka. Matumizi 38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009 Wizara iliidhinishiwa shilingi 273 bilioni kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili, 2009, shilingi 248 bilioni zilikuwa zimetolewa na HAZINA na shilingi 231 bilioni zilikuwa zimetumika ambazo ni sawa na asilimia 93 ya fedha zote zilizotolewa. 39. Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka 2008/2009, nililieleza Bunge lako Tukufu kuwa kutokana na ufinyu wa bajeti, Wizara ingetumia fursa na rasilimali zilizopo ndani ya Wizara kwa lengo la kutekeleza baadhi ya kazi badala ya kutumia wakandarasi. Katika kutekeleza ahadi hiyo Kikosi cha Ujenzi cha Jeshi la Magereza kimekarabati Chuo cha Polisi Kidatu - Morogoro na Kiwanda cha ushonaji cha Magereza kilichopo Ukonga Dar es Salaam kimeshona sare za askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Wizara itaendelea kuzifanya fursa hizi kuwa endelevu. 40. Mheshimiwa Spika, pia nilieleza kuwa Wizara itazingatia suala la jinsia katika maeneo yetu mbalimbali ya kazi ili kuona idadi ya watumishi wanawake katika utumishi wa Wizara inaongezeka kila wakati kulingana na majukumu na kazi zilizopo. Katika kipindi cha mwaka 2008/2009 Wizara ilitoa mafunzo kwa askari/watumishi 10,859 ambapo wanawake ni 1,069 sawa na asilimia 10. Pia Wizara iliwapandisha vyeo jumla ya askari/watumishi 3,875 ambapo wanawake ni 629 sawa na asilimia 16. Suala hili litaendelea kuzingatiwa katika mipango ya Wizara. 41. Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa ya kiutendaji iliyotukabili katika utekelezaji wa bajeti ya 2008/2009 ni kuchelewa kupatikana kwa magari kutokana na mchakato wa manunuzi unaofanyika kitaifa kupitia Wizara ya Miundombinu. Hali hii imeathiri kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa ahadi ya Wizara ya kupeleka magari kwenye baadhi ya vituo vilivyoahidiwa. Huduma ya Polisi 42. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kushirikiana na vyombo vingine vya dola pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo majeshi mengine ya Shirikisho la Polisi la kimataifa - Interpol, Shirikisho la Polisi la nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika – EAPCCO na Shirikisho la Polisi la nchi za Kusini mwa Afrika - SARPCCO kupitia ubadilishanaji taarifa za uhalifu na wahalifu, mafunzo, operesheni mbalimbali za pamoja na mikutano ya Wakuu wa Majeshi na Wakuu wa Upelelezi wa nchi wanachama. Operesheni ya pamoja ilifanyika iliyohusisha nchi za Tanzania, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi na Mauritius kwa lengo la kukamata magari ya wizi, dawa za kulevya, dawa bandia, silaha haramu na wahamiaji haramu. 43. Mheshimiwa Spika, katika dhana hiyo hiyo, mwezi Agosti, 2008 nchini Ethiopia, Tanzania iliweka saini Itifaki ya kuzuia na kupambana na wizi wa mifugo ambayo inahusisha nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika. Lengo la Itifaki hiyo ni kuziwezesha nchi wanachama kushirikiana katika kuzuia na kupambana na wizi wa mifugo. Wizara imeanza mchakato ili Itifaki hiyo iridhiwe na Bunge. 4. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa ulinzi kwenye maeneo yenye migogoro baina ya wafugaji na wakulima, na mapigano ya koo. Serikali imeunda Kikosi Kazi kinachoongozwa na Jeshi la Polisi kinachojumuisha wataalam kutoka Wizara za Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Katiba na Sheria na Ofisi ya Rais, Utawala Bora ili kufuatilia tatizo la migogoro ya mara kwa mara inayotokea kati ya wafugaji na wakulima Mkoani Morogoro. Kikosi Kazi tayari kimekamilisha taarifa yake na kuiwasilisha Serikalini. Mikakati ya Kukabiliana na Uhalifu 45. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau wengine limeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu na tatizo la usalama barabarani. Kwa upande wa ajali za barabarani, tatizo bado ni kubwa na linahitaji nguvu za pamoja za wadau wote. Makosa ya mauaji ya Albino yameendelea kudhibitiwa. Katika kipindi cha Julai, 2008 hadi Aprlili, 2009 watuhumiwa 86 wa makosa ya mauaji ya Albino wamefikishwa Mahakamani na kesi zao zinaendelea kusikilizwa. Mwaka 2009/2010 Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza mikakati ya kukabiliana na uhalifu na ajali za barabarani, mapigano baina ya koo, migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro katika maeneo ya migodi, ajali za majini na mauaji yanayotokana na imani za kishirikina. Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 46. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2008/2009 Jeshi la Polisi limeanza utekelezaji wa mkakati wa kuimarisha ulinzi wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2009 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Maandalizi haya yanalenga kuongeza askari 7000 na vitendea kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na magari na vifaa vya kutuliza ghasia. Programu ya Maboresho ya Jeshi la Polisi 47. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeifanyia mapitio programu yake ya awali ya maboresho na kupanga programu ya miaka mitano (2009/2010 -2013/2014) yenye mihimili mitatu ya Usasa, Weledi na Polisi Jamii. Programu hiyo ina maeneo makuu sita ambayo ni, mifumo ya kazi za Polisi, sheria, kanuni na muundo wa kitaasisi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA), menejimenti ya rasilimali watu, miundombinu na vitendea kazi na Polisi Jamii/Ulinzi Shirikishi. Ujenzi wa Nyumba za Makazi 48. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa nyumba mbili katika Wilaya ya Bahi na nne katika kikosi cha FFU Finya umekamilika. Mradi wa ujenzi wa nyumba 54 Dar es Salaam na sita Zanzibar upo katika hatua za mwisho, ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa moja kila moja Wilaya ya Mwanga unaendelea. Katika mwaka 2009/10 ujenzi wa nyumba utaanza katika kambi za Mabatini – Mwanza, Musoma, Kegonga na Nyamwaga Mkoani Mara, Ludewa - Iringa, Mtambaswala – Mtwara, Horohoro – Tanga, Muhukuru - Ruvuma na Byekera - Kagera. Pia ujenzi wa nyumba za askari utaendelea katika kambi za Finya – Kusini Pemba, Tunguu na Unguja Ukuu – Kusini Unguja. Ujenzi wa Ofisi 49. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa ofisi za Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Tabora, Kilimanjaro, Dodoma, Morogoro na Mbeya, na vituo vya Polisi vya Makambako na Chato upo katika hatua za mwisho. Miradi inayoendelea ni vituo vya Polisi vya Wilaya za Mpanda, Ludewa, Newala, Bukombe na Meatu. Katika mwaka 2009/2010 ujenzi utaanza wa ofisi ya Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Jijini Dar es Salaam, ofisi za Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Mara na Manyara, ofisi za Wakuu wa Polisi Wilaya za Bahi, Bagamoyo na Njombe na ofisi za Wilaya za Kipolisi za Mbagala na Rorya. Vilevile ujenzi wa vituo vya Daraja “C” katika kata za Kegonga Mkoani Mara, Muhukuru Mkoani Ruvuma, Horohoro Mkoani Tanga na Mtambaswala Mkoani Mtwara na ofisi za Makao Makuu ya Kikosi cha Ujenzi. Ujenzi na Ukarabati wa Vyuo 50. Mheshimiwa Spika, ukarabati wa vyuo vya Polisi uliendelea katika vyuo vya Dar es Salaam, Moshi, Zanzibar na Kidatu. Mwaka 2009/2010 ujenzi utaanza wa Chuo cha Upelelezi Dodoma. Upembuzi yakinifu utaendelea kwa ajili ya upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi. Ukarabati wa Vituo vya Polisi na Kambi 51. Mheshimiwa Spika, ukarabati utaendelea wa kituo cha Polisi cha Wilaya ya Nkasi, ofisi za Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Rukwa na Pwani, kituo cha Polisi Kati –Tabora, jengo la karakana ya vifaa vya mawasiliano, ghala kuu la Polisi Dar es Salaam, zahanati ya kambi ya Polisi Kunduchi na ofisi ya Polisi Makao Makuu ya kutuliza ghasia. Ununuzi 52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 Jeshi la Polisi limelipia magari 13 aina ya Toyota L/Cruiser Pick –Up, lori moja la maji taka, gari moja la kubebea wagonjwa na mabasi mawili. Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya kutokana na utaratibu mpya wa ununuzi, Wizara yangu haikufanikiwa kupeleka magari katika Wilaya zilizoahidiwa katika mwaka wa fedha uliopita. Naomba kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba Wilaya zote zilizopangiwa kupata magari watapata kama ilivyoahidiwa. Mwaka wa fedha wa 2009/2010 yatanunuliwa magari 22 aina ya Toyota Land Cruiser Pick Up, lengo likiwa kuhakikisha kwamba Wilaya zote za Tanzania ziwe na magari ya Polisi. Huduma za Magereza 53. Mheshimiwa Spika, jukumu la Jeshi la Magereza ni kuhifadhi wafungwa wa aina zote pamoja na kurekebisha tabia za wale waliohukumiwa vifungo. Urekebishaji wa tabia za wafungwa hufanywa kupitia programu za mafunzo kwa njia ya vitendo na nadharia, ili wamalizapo vifungo vyao wawe raia wema katika jamii. Programu hizo huendeshwa kupitia miradi ya ujenzi, kilimo na viwanda vidogovidogo. Mafunzo ya nadharia huendeshwa katika Chuo cha Ufundi cha Magereza Ruanda - Mbeya, Gereza la Wami Vijana na utoaji ushauri nasaha kwa kutumia walimu wa dini na Maafisa Ustawi wa Jamii. Usafirishaji wa Mahabusu Kwenda Mahakamani na Kurudi Magerezani 54. Mheshimiwa Spika, ili kuboresha usafirishaji wa mahabusu kwenda mahakamani na kurudi magerezani, katika mwaka 2008/2009 yamelipiwa magari matano ambayo ni mabasi makubwa matatu na madogo mawili. Jukumu hili limeanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya za Kisarawe, Mkuranga na Kibaha Mkoani Pwani na litaendelezwa kwa awamu kwenye mikoa mingine kadri bajeti itakavyoruhusu. Katika mwaka 2009/2010, Jeshi la Magereza linatarajia kununua mabasi makubwa mawili, madogo matano na Pick-Up tano kwa ajili ya Mkoa wa Pwani na Arusha. Programu za Urekebishaji wa Wafungwa 55. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009 Jeshi la Magereza lilianza kutekeleza mradi wa uendeshaji wa shughuli za wafungwa nchini kote kwa kutumia mtandao wa kompyuta wa Offenders Management Information System. Utekelezaji wa mradi huu utaendelezwa katika mikoa yote nchini kwa awamu kadri fedha zitakavyopatikana. Ajira 56. Mheshimiwa Spika, askari wapya 1,081 wameajiriwa baada ya kuhitimu mafunzo ya awali ya uaskari katika Chuo cha Magereza Kiwira Mkoani Mbeya. Mwaka 2009/2010 Jeshi la Magereza linatarajia kuajiri askari wapya 598. Uimarishaji wa Magereza Makongwe Yenye Ulinzi Mkali 57. Mheshimiwa Spika, ukarabati na uboreshaji wa majengo na miundombinu ya magereza yenye ulinzi mkali umefanyika na unaendelea katika magereza ya Karanga - Kilimanjaro, Lilungu – Mtwara, Gereza Maalum Isanga – Dodoma na Ukonga – Dar es Salaam. Lengo la mwaka 2009/2010 ni kuendelea na ukarabati katika magereza ya Maweni – Tanga, Uyui – Tabora, Karanga – Kilimanjaro, Butimba – Mwanza na Ukonga – Dar es Salaam. Upanuzi, Ukarabati na Ujenzi wa Mabweni ya Wafungwa na Nyumba za Askari 58. Mheshimiwa Spika, kazi ya upanuzi, ujenzi na ukamilishaji wa mabweni ya wafungwa ulifanyika katika magereza ya Korogwe, Kahama, Isupilo, Mahabusu Tabora, Mafia, Kilosa, Bukoba, Ubena, Kigongoni, Mahenge, Mahabusu Songea, Singida, Ileje, Ludewa, Muleba, Geita, Kilwa, Njombe na Kingolwira. Katika mwaka 2009/2010 kazi hiyo itafanyika kwa mabweni ya wafungwa na ofisi za magereza 19 yaliyopo katika Mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Manyara, Pwani, Dar es Salaam, Kagera, Morogoro, Mara, Arusha, Mbeya, Iringa, Shinyanga, Ruvuma, Singida, Tanga na Tabora. Uimarishaji wa Mifumo ya Maji Safi na Maji Taka 59. Mheshimiwa Spika, kazi ya uimarishaji wa mifumo ya maji safi na maji taka iliendelea katika magereza ya Mwanga, Kibiti, Segerea, Nachingwea, Mafia, Kahama na Kikosi Maalum Ukonga. Mwaka 2009/2010 kazi hiyo itaendelea katika magereza ya Mwanga, Meatu, Mbinga, Kalilankulukulu, Kingurungundwa, Majimaji, Mkwaya, Kibondo, Hanang, Butundwe, Kiteto, Chuo Ukonga na Gereza Kiabakari. Fidia na Upimaji wa Maeneo ya Magereza 60. Mheshimiwa Spika, fidia ya mazao na majengo imefanyika katika eneo la upanuzi wa Gereza la Mahabusu Segerea na eneo litakapojengwa Gereza la Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi. Upimaji wa maeneo umefanyika katika vituo vya Nzega, Mbinga na eneo litakalojengwa Gereza la Wilaya ya Chato. Maeneo ya magereza yataendelea kupimwa katika magereza kumi ya Ubena, Mkuza, Mwanga, Kibiti, Matongo, Ngwala, Kalilankulukulu, Rwamurumba, Kondoa na Hanang. Ununuzi wa Magari na Zana za Kilimo 61. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Jeshi la Magereza limelipia fedha za ununuzi wa magari ya aina mbalimbali 49 kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa magereza. Uboreshaji wa mashamba umeendelezwa kwa kununua majembe 64 ya kukokotwa na wanyamakazi, power tillers nane pamoja na mashine nne za kunyunyizia dawa kwenye mikorosho. Lengo la mwaka 2009/2010 ni kununua matrekta manane, power tillers nne, magari 22 na mashine moja ya kuvuna mpunga (combine harvester). Shirika la Magereza 62. Mheshimiwa Spika, Shirika la Magereza lilianzishwa chini ya kifungu Na. 3 (1) cha Sheria Na. 23/1974 (The Corporations Sole Establishment Act, 1974). Madhumuni ya Shirika hili ni kuendesha programu za urekebishaji wa wafungwa kwa njia ya uzalishaji kupitia miradi ya kilimo, mifugo na utengenezaji wa vifaa toka viwanda vidogovidogo. Shirika lina jumla ya miradi 15 ya kilimo na mifugo na nane ya viwanda vidogovidogo. 63. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2008/2009, shirika liliendelea kuimarisha viwanda kwa kufunga mashine mpya Kiwanda cha Viatu Karanga - Moshi na Uhunzi katika Gereza Ukonga. Ununuzi wa pembejeo umefanyika na Serikali imetoa ruzuku ya zana za kilimo kwenye mashamba ya magereza ya Mollo - Sumbawanga na Songwe – Mbeya. Ekari 1000 za mahindi zililimwa katika magereza hayo na magunia 6,678 ya mahindi yalipatikana. Ekari 450 za mpunga zililimwa katika shamba la Gereza Idete lililoko Ifakara – Morogoro na kupata magunia 2,846. Matarajio ya mwaka 2009/2010 ni kuweka nguvu zaidi katika shamba la Kitengule Kagera ili kutumia fursa ya kilimo cha umwagiliaji. Jeshi la Magereza Kuzalisha Mbegu Bora za Kilimo 64. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza limeanza kuchukua hatua ya kuzalisha mbegu bora za kilimo katika Mikoa sita ya Morogoro, Arusha, Dodoma, Lindi, Manyara na Kilimanjaro, ambazo zitasambazwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini. Matumizi ya Nishati Mbadala Magerezani 65. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza limeanza kutumia makaa ya mawe katika Magereza ya Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kupikia chakula cha wafungwa badala ya kuni. Utaratibu huu unatarajiwa kuendelezwa katika Mikoa ya Iringa, Ruvuma na Rukwa. Mradi wa kutumia gesi itokanayo na tungamotaka (biogas) unaendelea vizuri katika Gereza la Ukonga. Katika Gereza la Keko upo mradi wa kutumia gesi asilia kwa ajili ya kupikia chakula cha wafungwa. Miradi hii inatarajiwa kuenezwa katika magereza yote makubwa nchini. Juhudi za Kupambana na Janga la UKIMWI Magerezani 66. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza limejikita katika utoaji wa ushauri nasaha, elimu ya kujikinga na maambukizi mapya kupitia waelimishaji rika, uhamasishaji wa kupima virusi vya ukimwi kwa hiari ili kujitambua, na utoaji wa dawa. Ufuatiliaji wa watumishi na wafungwa wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi na UKIMWI umefanyika na wanaendelea kupatiwa virutubisho na dawa za kupunguza makali ya VVU. Huduma kwa Jamii 67. Mheshimiwa Spika, Programu ya Huduma kwa Jamii ambayo ni mojawapo ya adhabu mbadala wa kifungo gerezani inaendelea kutekelezwa katika Mikoa 12 ya Tanzania Bara. Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Iringa, Kagera, Mara na Shinyanga. Hadi kufikia mwezi Mei, 2009 wafungwa wanaume 831 na wanawake 158 wamefaidika na programu hii. Wafungwa hao wamekuwa wakifanya kazi kwenye taasisi za umma. 68. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Wizara itajikita katika kuimarisha muundo wa Idara ya Huduma kwa Jamii kwa kuajiri Maafisa Majaribio (Probation Officers) ambao watasimamia utekelezaji wa sheria zinazohusu adhabu mbadala za Huduma kwa Jamii, Huduma za Majaribio, Sheria ya Bodi za Parole na utaratibu wa kifungo cha nje. Watumishi 100 wanatarajiwa kuajiriwa na kupewa mafunzo maalumu na ununuzi wa vitendea kazi, zikiwemo pikipiki. Huduma za Zimamoto na Uokoaji 69. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009 nchi yetu imeshuhudia majanga makubwa ya moto, ajali mbalimbali zikiwemo za barabarani, treni, vyombo vya usafiri majini na tukio la kulipuka kwa mabomu kwenye ghala la kuhifadhia silaha katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania iliyoko Mbagala Jijini Dar es Salaam. Ukaguzi wa Tahadhari na Kinga ya Moto 70. Mheshimwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea na zoezi la ukaguzi wa tahadhari na kinga dhidi ya moto katika maeneo mbalimbali nchini. Ukaguzi huu umeenda sambamba na utoaji wa elimu ya kinga dhidi ya moto, majanga mengine au moto unapotokea na jinsi ya kutumia vifaa vya kuzimia moto. Katika kipindi cha Julai 2008 hadi Aprili 2009 jumla ya nyumba 582 ziliteketea kwa moto. Tukio kubwa la ajali ya moto ni lile lililotokea tarehe 23 Machi, 2009 kwenye hoteli za kitalii za Paradise, Oceanic na Malaika katika Wilaya ya Bagamoyo. Katika tukio hilo madhara makubwa yalitokea hasa kwenye hoteli ya Paradise ambapo mali nyingi ziliteketea na watumishi watatu walijeruhiwa. 71. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 zoezi la ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto lilifanyika kwenye maeneo 3,576. Ukaguzi huo pia ulilenga kutoa elimu ya moto kwa jamii na namna ya kutumia vizimamoto vinavyobebeka (Portable Fire Extinguishers) ambavyo vinawekwa katika maeneo ya kufanyia kazi au makazi. Zoezi la ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto ni endelevu. 72. Mheshimiwa Spika, mchakato wa utekelezaji wa usimamizi wa Vikosi vya Zimamoto na Uokoaji wa komandi moja na kuanzisha ofisi za Mikoa za Zimamoto na Uokoaji unaenda sanjari na ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dar es Salaam ambao umeanza katika bajeti ya mwaka 2008/2009. Mafunzo na Ajira 73. Mheshimwa Spika, katika mwaka 2008/2009 askari 60 walipatiwa mafunzo ambapo askari 59 walihitimu mafunzo hayo. Mafunzo ya muda mfupi yalitolewa kwa watumishi 13 kwa lengo la kuwajengea uwezo kiutendaji. Askari wapya watano waliajiriwa. Katika mwaka 2009/2010 mafunzo yatatolewa kwa askari 300 na askari 42 wataajiriwa. Huduma za Uhamiaji 74. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2008 hadi Mei, 2009, jumla ya wageni 680,168 waliingia nchini, ikilinganishwa na wageni 732,328 walioingia nchini katika kipindi kama hicho mwaka uliopita. Wageni 652,720 walitoka nchini ikilinganishwa na wageni 681,750 waliotoka nchini katika kipindi kama hiki mwaka uliopita. Kwa ujumla idadi ya wageni walioingia na kutoka nchini imepungua. Kushuka kwa idadi hii kunaweza kuelezwa pamoja na mambo mengine ni kutokana na mtikisiko wa uchumi duniani. 75. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2008 hadi Mei, 2009 wageni 10,682 walipewa vibali vya kuishi nchini ikilinganishwa na wageni 11,356 waliopewa vibali mwaka 2007/2008. Idadi ya vibali vilivyotolewa imeshuka kwa asilimia 6. Hii inatokana na baadhi ya makampuni au mashirika kupunguza nafasi za ajira au idadi ya watumishi katika maeneo yao. Uratibu wa Maombi ya Wageni Wanaoomba Uraia wa Tanzania 76. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2008/2009, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa uraia kwa wageni 146 waliotimiza masharti na kuyakataa maombi 41. Mchakato wa Kuratibu Maombi ya Uraia ya Wakimbizi wa Burundi 77. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) inaendelea kushughulikia maombi ya uraia ya Wakimbizi wa Burundi walioingia nchini mwaka 1972 na kuishi katika makazi ya Mishamo na Katumba Mkoani Rukwa, na Ulyankulu Mkoani Tabora. Katika kipindi cha mwezi Machi, 2008 hadi mwezi Mei, 2009 Wizara imekwishapokea maombi ya Wakimbizi wakaazi 51,876 toka Mkoani Rukwa na 20,523 toka Mkoani Tabora, ambayo yameshughulikiwa katika ngazi za Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mkoa. Wizara inaendelea na zoezi la kuyapitia na hatimaye kutoa maamuzi. 78. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2008/2009, Watanzania 32 walipatiwa uraia wa nchi nyingine na hivyo kupoteza haki ya kuwa raia wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995. Watanzania wengi wanaoukana uraia wetu ni wanawake. Kati ya idadi hiyo wanawake ni 21 ambao ni sawa na asilimia 66 kutokana na wengi wao kuolewa na wageni wa mataifa mengine. Wanaume ni 11 waliopata uraia wa mataifa mengine kutokana na ama kupata ajira ughaibuni au kutegemea kupata mafao yatolewayo kwa raia wa nchi husika. Uraia wa Nchi Mbili 79. Mheshimiwa Spika, hoja ya nchi yetu kuruhusu uraia wa nchi mbili imekuwa ikijadiliwa ndani na nje ya Bunge lako Tukufu kwa miaka kadhaa, bila shaka kutokana na ukweli kwamba Tanzania ipo katika mageuzi ya kisiasa na kiuchumi, na katika mageuzi hayo kila njia inatafutwa ili kuharakisha maendeleo ya nchi. Serikali imekuwa ikilifanyia kazi suala hili la uraia wa nchi mbili. Kwa kuzingatia kuwa uraia ni suala la muungano, Serikali iliwasiliana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ( SMZ ) ili kupata maoni yake. Baada ya kupata maoni ya awali ya SMZ, Wizara yangu imeendelea kulifanyia kazi kwa lengo la kufikia muafaka juu ya namna ya kulishughulikia. Pasipoti na Hati za Kusafiria 80. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009 Idara ya Uhamiaji ilitoa jumla ya pasipoti 46,622. Kati ya hizo 44,586 ni za kawaida, 1,677 ni za Afrika Mashariki, 297 za kibalozi na 62 za kitumishi, ikilinganishwa na jumla ya pasipoti 69,521, ambapo pasipoti 66,339 za kawaida, 2,691 za Afrika Mashariki, 392 za kibalozi na 99 za kiutumishi zilizotolewa mwaka 2007/2008. 81. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2008/2009, vijana 372 walirudishwa nchini toka nchi mbalimbali baada ya kubainika kwamba wapo kwenye nchi hizo kinyume cha sheria ikilinganishwa na vijana 382 waliorudishwa mwaka 2007/08. Misako na Doria 82. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2008 hadi Mei, 2009 Idara iliendesha doria na misako yenye lengo la kudhibiti wageni haramu nchini ambapo jumla ya wageni 3,109 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria ikilinganishwa na wageni 3,252 waliokamatwa katika kipindi cha mwaka 2007/08. Miongoni mwa idadi ya wahamiaji haramu waliokamatwa, 1,162 walitokea nchi za Pembe ya Afrika (Somalia 37 na Ethiopia 1,125). Kati yao 1,089 wamekwisharejeshwa kwao na 73 wapo katika magereza mbalimbali hapa nchini. Ujenzi /Ukarabati wa Nyumba na Ofisi 83. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, ujenzi umekamilika wa nyumba ya makazi ya Afisa Uhamiaji Mkoa wa Manyara na ofisi ya kituo cha kuingilia nchini cha Mkenda Nakawale mpakani mwa Tanzania na Msumbiji Mkoani Ruvuma. Awamu ya kwanza ya ukarabati wa majengo ya Chuo cha Uhamiaji Moshi imekamilika na ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, upanuzi wa Ofisi Kuu Zanzibar na ukarabati wa nyumba katika kituo cha mpakani cha Uhamiaji - Rusumo unaendelea. Miradi hii itaendelea kutekelezwa katika mwaka 2009/2010 Ajira na Mafunzo 84. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, askari wapya 192 wameajiriwa, na askari/watumishi 374 wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ndani na nje ya nchi. Katika mwaka 2009/2010, askari 150 wataajiriwa na mafunzo yatatolewa kwa watumishi 36. Ununuzi 85. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Idara imelipia magari tisa na mwaka huu zitanunuliwa pikipiki 20. Huduma za Wakimbizi 86. Mheshimiwa Spika, tarehe 1 Mei, 2009 walikuwepo wakimbizi 301,644 nchini. Wakimbizi 234,672 ni Warundi, 63,116 Wakongo (DRC), 1,529 ni Wasomali na 2,327 ni wakimbizi wa mataifa mbalimbali. Warundi wapatao 194,986 wanaishi kwenye makazi ya wakimbizi yaliyoko Katumba na Mishamo Wilayani Mpanda Mkoani Rukwa na Ulyankulu na Urambo Mkoani Tabora na wengine 39,686 wanaishi katika makambi Mkoani Kigoma. Katika kipindi 2008/2009, kambi moja ya Nduta iliyopo Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma ilifungwa. 87. Mheshimiwa Spika, kufuatia tathmini iliyofanywa mwaka 2007 kwa wakimbizi 218,234 waishio kwenye makazi ya Ulyankulu (Tabora), Katumba na Mishamo (Rukwa) wakimbizi 172,000 sawa na asilimia 79 walionyesha nia ya kutaka kubaki nchini. Mchakato wa kuwatafutia suluhisho la kudumu unaendelea. Huduma ya Kushughulikia Malalamiko 88. Mheshimiwa Spika, ili kuratibu ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi dhidi ya vyombo vya Wizara na pia malalamiko ya askari na watumishi wengine wa Wizara, ipo idara maalum kwa ajili ya kazi hiyo. Katika mwaka 2008/2009, idara ilipokea na kushughulikia jumla ya malalamiko 104 mengi yakihusu Jeshi la Polisi kuhusiana na ubambikizaji wa kesi na askari wa vyeo vya chini kulalamika kutotendewa haki katika suala zima la kufukuzwa kazi kwa askari hao. Katika mwaka 2009/2010, Wizara imeazimia kuanza mchakato wa kutunga sheria ambayo itaipa nguvu ya kisheria idara hii katika kutekeleza majukumu yake. Usajili wa Vyama vya Kijamii na Huduma ya Sheria 89. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 jumla ya vyama 296 viliandikishwa na hii inafanya jumla ya vyama vilivyoandikishwa hadi sasa kuwa 5,722. Pia idara iliendelea kutatua migogoro ya vyama mbalimbali vikiwemo sita vya kidini na vingine saba vya kiraia. Hata hivyo, migogoro hiyo bado inaendelea na chanzo kikubwa cha migogoro ndani ya vyama hivyo ni uchu wa madaraka na tamaa ya fedha miongoni mwa wanachama. 90. Mheshimiwa Spika, ili kufuatilia uhai wa vyama, zoezi la uhakiki limefanyika katika Mikoa 12 ya Mtwara, Lindi, Mbeya, Iringa, Mara, Mwanza, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Pwani na Morogoro na kubaini kuwa vyama vingi vinashindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na kuwepo migogoro ya mara kwa mara. 91. Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha utendaji katika Idara ya Huduma ya Sheria inayosimamia pia usajili wa vyama vya kijamii, katika mwaka 2009/2010 inatarajia kuwa na database ya usajili wa vyama, kuendelea kushughulikia migogoro ya vyama, kuhakiki utendaji na uhai wa vyama na kuelimisha vyama vilivyoandikishwa juu ya wajibu wao wa kulipa ada ya mwaka. SHUKURANI 92. Mheshimiwa Spika, natoa shukurani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Wilson Mutagaywa Masilingi Mbunge wa Muleba Kusini kwa kupitia na kuchambua makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2009/2010 pamoja na ushauri wao katika masuala mbalimbali yahusuyo Wizara yangu. 93. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukurani za pekee kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Balozi Khamis Suedi Kagasheki, Mbunge wa Bukoba Mjini, Katibu Mkuu Ndugu Patrick Rutabanzibwa, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Elizabeth Nyambibo, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Inspekta Jenerali wa Polisi Ndugu Saidi Mwema, Kamishna Mkuu wa Magereza Ndugu Augustino Nanyaro, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Ndugu Kinemo Kihomano na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Ndugu Matwani Kapamba, wakuu wote wa Idara na vitengo, Makamanda wote, askari pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambao kwa ushirikiano wao hotuba hii imeweza kuandaliwa na kukamilika katika wakati unaotakiwa. 94. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukurani kwa nchi wahisani za Denmark, Canada, Sweden, Belgium, Libya na Uholanzi. Vile vile kwa nchi za China, UAE na Marekani. Aidha, shukurani zangu iziendee taasisi za kimataifa za INTERPOL, UNHCR, IOM, NORAD, WFP na Benki ya Dunia kwa misaada yao ambayo imeongeza uwezo wa kiutendaji wa Wizara yangu. MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2009/2010 95. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naliomba Bunge lako Tukufu lipitishe Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2009/2010 ya shilingi 395,345,819,200 kama ifuatavyo: Fungu 14: Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Matumizi Mengineyo shilingi 3,080,000,000 Mishahara shilingi 1,246,343,000 Maendeleo shilingi 3,000,000,000 Jumla shilingi 7,326,343,000 Fungu 28: Jeshi la Polisi Matumizi Mengineyo shilingi 99,058,982,000 Mishahara shilingi 92,612,438,000 Maendeleo shilingi 22,870,815,000 Jumla shilingi 214,542,235,000 Fungu 29: Jeshi la Magereza Matumizi Mengineyo shilingi 52,000,000,000 Mishahara shilingi 48,238,639,000 Maendeleo shilingi 12,988,927,000 Jumla shilingi 113,227,566,000 Fungu 51: Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Matumizi Mengineyo shilingi 4,500,000,000 Mishahara shilingi 1,629,483,000 Maendeleo shilingi 6,440,980,200 Jumla shilingi 12,570,463,200 Fungu 93: Idara ya Uhamiaji Matumizi Mengineyo shilingi 15,374,996,524 Mishahara shilingi 13,309,107,476 Maendeleo shilingi 18,995,108,000 Jumla shilingi 47,679,212,000 96. Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. 97. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
|
||||