generica viagra

Hotuba ya Mgeni Rasmi

Friday, February 19, 2016

HOTUBA YA MGENI RASMI, WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. CHARLES M. KITWANGA, MB AKIFUNGUA KIKAO CHA KAZI CHA  MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI UKUMBI WA JULIUS NYERERE INTERNATIONAL CONVENTION CENTRE, DAR ES SALAAM  TAREHE 18 – 19 FEBRUARI 2016

  • Inspekta Jenerali wa Polisi, Ndugu Ernest Jumbe MANGU,
  • Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdurahman KANIKI,
  • Makamishna wa Polisi,
  • Naibu Makamishna wa Polisi,
  • Wajumbe wa Mkutano,
  • Waandishi wa Habari,
  • Wageni waalikwa,
  • Mabibi na Mabwana.

 
Habari za asubuhi!
Heri ya Mwaka Mpya!
Napenda kutumia fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo hii. Pili, natumia nafasi hii kumshukuru Inspekta Jenerali wa Polisi ndugu Ernest Mangu kwa kunipa heshima hii ya kuwa Mgeni Rasmi katika Kikao hiki muhimu. Kupitia hafla hii ninapata fursa ya kuzungumza na na viongozi wote waandamizi wa Jeshi la Polisi na makamanda wa mikoa na vikosi ambao ni wasimamizi wakuu wa kazi za Polisi. Ninawapongeza sana kwa utaratibu huu mliojiwekea wa kukutana kila mwaka kwa ajili ya kufanya tathimini lakini pia kuweka mikakati ya namna ya kuboresha huduma zenu kwa jamii pamoja na jinsi ya kuzidi kuboresha Jeshi la Polisi nchini.
Ndugu Wajumbe,
Nimatumaini yangu kuwa kikao hiki kitakuwa tofauti na vikao vilivyopita kutokana na kasi kubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Falsafa yake ya ‘HAPA KAZI TU’. Ni lazima mbadilishe mtazamo na kufanya kazi kwa kasi inayoendana na Serikali hii. Fanyeni tathimini ya tulikotoka, mapungufu, changamoto na fursa zilizopo ili kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi. Ni muhimu kupanga mikakati mipya ya kupambana na uhalifu kwa kuzingatia changamoto zilizopo na mapungufu mliyoyaona kwa mustakabali wa amani na usalama wa taifa letu. Kukiwa na usalama, shughuli za kiuchumi zitafanyika kikamilifu na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Aidha, usalama wa nchi yetu utazidi kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali nchini na kuongeza ajira nchini.
Ndugu Wajumbe,
Kwa kuangalia tu aina ya wajumbe wa kikao hiki, nimeridhika kuwa Kikao Kazi hiki ni muhimu sana kwa kuwa ninyi ndiyo msingi na dira ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini. Maamuzi yenu mtakayoyafanya kwenye kikao hiki na mkiamua kuyatekeleza kwa dhati taifa litakuwa limepiga hatua kubwa katika kukabiliana na wimbi la uhalifu nchini. Nimeambiwa kuwa kaulimbiu ya kikao hiki ni Badilika kifikra, acha kufanya kazi kwa mazoea. Kaulimbiu hii ni nzuri na ya maana kama  mtaamua kuitekeleza kwa vitendo. Malalamiko ya Wananchi dhidi ya utendaji kazi wa Askari Polisi yatapungua kwa kiasi kikubwa sana.
Ndugu Wajumbe,
Kwa kuwa hiki ni kikao changu cha kwanza kukutana na viongozi wote wa Jeshi la Polisi wa nchi nzima, nitumie fursa hii kutoa pongezi za dhati kwenu kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya katika kipindi chote cha Uchaguzi Mkuu. Mlisimamia kwa weledi wa hali ya juu sana Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani katika muda wote wa mchakato. Mlisimama imara kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu na kudumisha amani, utulivu, umoja na mshikamano kwa watanzania wote. Hongereni sana kwa kazi nzuri.
Ndugu Wajumbe,
Pamoja na pongezi hizo, nafahamu kuwa zipo changamoto kadhaa za kiuhalifu ambazo ziliripotiwa katika kipindi kilichopita. Takwimu zinaonesha kuwa kwa kipindi cha mwaka 2015 makosa makubwa yaliyoripotiwa yalikuwa 68,814 ukilinganisha na makosa 70,153 yaliyoripotiwa mwaka 2014 ambayo ni pungufu ya makosa 1,339  sawa na asilimia 1.9 %. Kwa upande wa makosa madogo mwaka 2015 yaliripotiwa  makosa 450,389  ukilinganisha na makosa 458,422 yaliyoripotiwa mwaka 2014 ambayo ni upungufu wa makosa 8,033 sawa na asilimia 1.8%.
Kutokanana takwimu hizo niwapongeze sana kwa kazi nzuri mliyoifanya kwa kipindi cha mwaka jana, na niwasihi muongeze nguvu zaidi katika kupambana na uhalifu huku tukijikita katika kuzuia zaidi kuliko kusubiri uhalifu utokee.
Aidha, nawakumbusha kuwa katika kuhakikisha kuwa hili linafanikiwa ni lazima kujenga mahusiano mazuri na jamii kwani wao ndio hasa wahusika na waathirika wa uhalifu na wanawafahamu wahalifu kwa kuwa ni sehemu ya jamii. Mahusiano mazuri na jamii yatasaidia upatikanaji wa taarifa kwa wakati na hivyo kuwezesha askari wetu kushughulikia matukio ya kihalifu kwa wakati, weledi na ufanisi.
Ndugu Wajumbe,
Naelewa changamoto zinazotokana na upungufu wa vitendea kazi, nyumba, maslahi yasiyotosheleza kwa maafisa na askari, uhaba wa taaluma katika mafunzo na askari kuishi nje ya . Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia kwamba Serikali itaongeza jitihada ya kuliwezesha Jeshi la Polisi na askari kwa vitendea kazi vya kisasa kwa kadri uwezo wa bajeti utakavyoruhusu. Tutaendelea kuwajengea uwezo na maarifa ya kiutendaji kwa kuwaelimisha watendaji ili waendane na wakati wa sasa wa sayansi na teknolojia. Ni matarajio yangu kwamba mtatumia fursa zilizopo katika kutatua matatizo yanayolikabili Jeshi letu la Polisi, wakati jitihada kama nilivyoeleza hapo juu zinafanyiwa kazi kulingana na uwezo wa kifedha wa serikali. Aidha, napenda kusisitiza kwamba hatuna budi kutunza vizuri vifaa vilivyopo ili hivi vichache tulivyonavyo tuvitumie kwa muda mrefu zaidi. Hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha matumizi bora ya magari, nyumba, vifaa vya ofisini, matumizi ya umeme na maji katika makazi na ofisi. Ni muhimu sana kulisimamia hili ili kuepusha gharama zisizo za lazima. Kwa hiyo nawataka makamanda wote msimamie hili kwa dhati na kwa nguvu zenu zote.
Pia lipo suala la ajali za barabarani ambalo limekuwa likikua siku hadi siku hasa ajali zinazohusisha pikipiki maarufu kama boda boda. Ninaunga mkono harakati zinazofanywa na kitengo cha usalama barabarani katika kutoa elimu ya usalama barabarani, lakini  nawataka nguvu kubwa pia ielekezwe huko kama mlivyoelekeza nguvu kubwa kukabiliana na ajali za barabara kwa mabasi na malori yaendayo mikoani. Kwa mfano kwa Jiji la Dar es Salaam pekee, karibu kila siku kumekuwa kukiripotiwa ajali zinazohusisha bodaboda na nyingi zinasababisha vifo au ulemavu kwa madereva na hata abiria wao na wakati mwingine hata kwa watumiaji wengine wa barabara. Ajali hizi zidhibitiwe.
Mbali na kuhusika katika ajali za barabarani, bodaboda pia zimekuwa zikihusika sana katika matukio ya kihalifu hasa unyang’anyi wa kutumia silaha. Ni rai yangu kwenu kuwa baada ya mkutano huu mtoke na suluhisho kwa tatizo hili hasa uhalifu wa kutumia silaha kwa kutumia pikipiki jijini Dar es salaam. 
Ndugu Wajumbe,
Yapo malalamiko kadhaa juu ya baadhi ya askari na maafisa wachache wanaotumia beji ya polisi vibaya kwa kuwabambikia kesi wananchi, kuomba na kupokea rushwa, kuchelewa kufika eneo la tukio hata kama ni umbali mfupi tu, kula njama na watuhumiwa na hivyo kuharibu vielelezo vya kesi, kuchelewesha upelelezi wa kesi, kutokuwajali wateja (huduma bora kwa mteja) na mengi mengineyo ambayo yamekuwa ni kero kubwa sana kwa jamii. Natambua kuwa mmekuwa mkiwashughulikia askari na maofisa waliotuhumiwa kujihusisha na tabia hizi kwa mujibu wa sheria, lakini nitoe rai kwenu viongozi kuongeza jitihada zaidi katika kushughulikia matatizo haya kwa kuwasimamia ipasavyo askari wenu kuanzia ngazi ya chini kabisa. Nawahakikishia kuwa Serikali haitafumbia macho askari au Afisa yeyote atakayefanya mambo haya ya hovyo bila kujali cheo chake. Tutachukua hatua kwa faida ya Watanzania.
Ninaimani kuwa kila kiongozi akijiepusha katika kulinda na uendekeza mambo ya hovyo na akiwasimamia anaowaongoza ipasavyo  na kuhakikisha kuwa wanawajibika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi na za nchi, malalamiko ya aina hiyo yatapungua sana kama si kumalizika kabisa.
 
Ndugu Wajumbe,
Mapambano dhidi ya uhalifu na wahalifu ndiyo jjukumu la msingi la Jeshi la Polisi. Ninawataka makamanda wote wa mikoa kuweka mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu na wahalifu katika himaya zenu ili kupunguza uwezekano wa wahalifu kukimbilia maeneo mengine pindi wanapofanya uhalifu. Aidha mafunzo kazini yaimarishwe ili kuwajengea askari uwezo wa kukabiliana nauhalifu.
Mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja wenu, tunasikia taarifa za kukamatwa mirungi na bangi kwa wingi lakini dawa za kulevya za viwandani hatuzikii zikikamatwa. Nawakumbusha kudhibiti mitandao ya madawa ya kulevya ya viwandani. Tutapima ufanisi wenu kwa kuangalia uhalifu wa aina zote hasa eneo hili la madawa ya kulevya. Ni wazi kuwa hii ni vita kubwa na inahitaji umakini wa hali ya juu katika kukabiliana nayo kutokana na namna biashara hii inavyoendeshwa.  Ninawasihi katika mkutano huu mtoke na mkakati wa namna ya kushughulika na wote wanaojihusisha na biashara hii haramu ili kuikomesha kabisa.
Ndugu wajumbe ,
Kwa kumalizia niseme tena kuwa ni matumaini yangu kikao hiki kitaleta tija kwa taifa zima na maazimio mtakayotoka nayo ndiyo yatakuwa dira katika njia mtakayopita mwaka huu katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku na kuhakikisha kuwa amani tuliyonayo inadumishwa.
Ndugu IGP, Makamanda na Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi,
Mwisho ingawa si mwisho kwa umuhimu, natumia nafasi hii kuwapongeza Makamishna Albert Nyamhanga, Nsato Marijani na Simon Sirro kwa kupandishwa vyeo na kuwa kupewa nafasi za juu za kuwatumikia Watanzania mkiwa Makamishna wa Polisi. Nafasi hizo ni mzigo mzito kwenu. Nawatakia kila la kheri katika utumishi wetu. Nitoe tena shukrani za dhati kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kwa kunialika kusema nanyi na kufungua Kikao hiki muhimu.
 
Baada ya kusema hayo sasa  natamka kuwa kikao kazi cha  Maafisa Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa polisi wa Mikoa na Vikosi cha Mwaka 2016 kimefunguliwa rasmi.
 
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
 

Back to Top