generica viagra

HOTUBA YA MGENI RASMI, WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU, MB. WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA MWAKA WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA MAGEREZA BWALO KUU LA MAAFISA MAGEREZA - UKONGA, D’SALAAM, TAREHE 17 MACHI, 2017

Friday, March 17, 2017

HOTUBA YA MGENI RASMI, WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
MHE. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU, MB. WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA MWAKA WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI
LA MAGEREZA BWALO KUU LA MAAFISA MAGEREZA - UKONGA, D’SALAAM, TAREHE 17 MACHI, 2017
 

 • Kamishna Jenerali wa Magereza Dkt. Juma A. Malewa,
 • Kamishna wa Fedha na Utawala,
 • Maafisa Waandamizi kutoka Makao Makuu ya Magereza,
 • Wakuu wa Magereza wa Mikoa Tanzania Bara,
 • Wakuu wa Vyuo vya Magereza,
 • Mkuu wa Kikosi Maalum,
 •  Mkuu wa Bwawani Sekondari,
 • Viongozi mbalimbali mliopo,
 • Wageni Waalikwa,
 • Waandishi wa Habari,
 • Mabibi na Mabwana.

 
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika siku hii ya leo tukiwa na afya njema. Nashukuru pia kwa kupata fursa ya kuwa Mgeni Rasmi katika hafla hii ya ufunguzi wa Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara.
 
Ndugu Kamishna Jenerali,
Kwa kuwa huu ni mkutano wangu wa kwanza wa aina hii kwa uongozi mpya wa Jeshi, nitumie fursa hii kumpongeza Kamishna Jenerali wa Magereza Dkt. Juma A. Malewa kwa kuteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza.  Hii ni ishara imani kubwa ambayo Mheshimiwa Rais anayo kwako. Hongera sana.
 
Nimeelezwa kwamba Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Magereza ndicho kikao cha juu cha uongozi ambacho huwakutanisha Maafisa Waandamizi kutoka Makao Makuu, Wakuu wa Magereza wa Mikoa, Wakuu wa Vyuo, Mkuu wa Kikosi maalum na Mkuu wa Sekondari Bwawani. Aina ya wajumbe wa mkutano inadhihirisha kwamba mkutano huu ni muhimu sana katika uendeshaji wa Jeshi kwani ni mahali ambapo viongozi wa juu mnakutana kujadiliana mambo mbalimbali na kuweka mikakati ya namna ya kuboresha utendaji kazi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mliyokabidhiwa. Ni mahali ambapo mtapitia malengo yenu mliyojiwekea kama mmeweza kuyatekeleza kwa kiwango mlichokusudia, kuangalia sababu zilizofanya kutofikia malengo na kupanga mikakati ya kuweza kufanikisha malengo yenu.
 
Ndugu Kamishna Jenerali,
Ninafahamu jitihada zako katika kufanya maboresho ya Jeshi la Magereza ambayo yanahusisha uandaaji wa Rasimu ya Sera ya Taifa ya Magereza. Niwahakikishie kwamba kwa kushirikiana na Kamishna Jenerali wa Magereza tutafuatilia kwa karibu ukamilishwaji wa será hiyo ili kuliwezesha Jeshi kutekeleza Mpango Mkakati katika kuboresha maeneo mbalimbali na kuongeza tija na ufanisi.
 
Nitoe rai kwenu kwamba pamoja na kusubiri ukamilishwaji wa será hiyo, tumieni kikao hiki kujadili kwa kina namna Jeshi la Magereza linavyoweza kufanya mageuzi ya kiutendaji.  Utekelezaji wa maboresho katika maeneo mengine ya kiutendaji unaweza kuendelea wakati tunasubiri kupatikana kwa Sera ya Taifa ya Magereza. 
 
Ndugu Wajumbe,
Baada ya maelezo hayo ya utangulizi nitumie fursa hii kusisitiza mambo machache ambayo yana maslahi mapana katika mustakabali wa chombo hiki. Suala la kwanza ni matumizi mazuri ya fursa zilizopo ndani ya Jeshi la Magereza. Kwa upande wa ardhí, Jeshi la Magereza lina eneo lenye ukubwa wa takribani hekta 130,482 ambazo zinafaa kwa shughuli za kilimo, mifugo na hifadhi ya mazingira. Aidha, mna nguvu kazi ya wafungwa wakiwemo wale wa vifungo virefu wanaoweza kutumika katika shughuli za uzalishaji.
 
Tumieni mkutano huu kujitathmini, kujadiliana na kupanga mikakati ya kutumia ipasavyo fursa mlizonazo katika kuongeza uzalishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali ikiwemo chakula, mifugo na bidhaa za viwandani ili kuongeza mapato kwa manufaa ya Jeshi na taifa kwa ujumla.
Nimefurahi kusikia kwamba andiko la mkakati wa Jeshi la Magereza kujitosheleza kwa chakula limewekwa kwenye mipango ya utekelezaji na Serikali. Nitoe rai tena kwenu kwamba ni vyema mkaanza maandalizi ya utekelezaji wa mpango huo kwa yale yanayowahusu ili Serikali itakapoanza kutekeleza mpango huo, pasiwepo na kikwazo chochote kwa kuwa kila upande utakuwa umejiandaa ipasavyo. Haya ni maelekezo rasmi ya Serikali. Maelekezo haya nimekuwa nikiyatoa katika mikoa yote nilikofanya ziara. Aidha, sote tunakumbuka maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu jambo hili katika kikao chake Dodoma.
Ndugu Wajumbe,
Suala la pili ni kuhusu migogoro ya ardhí baina ya Jeshi na wananchi wanaowazunguka. Sababu moja kubwa ya kuwepo kwa migogoro hii ni kutopimwa na kukosa hati kwa maeneo mengi ya magereza. Migogoro mingine imekuwa ni ya muda mrefu na ufumbuzi wake ni mgumu. Hali ya kuwepo na migogoro kumesababisha kutokuwepo na maelewano na mahusiano mazuri baina ya Jeshi na wananchi majirani. Ni wakati sasa wa kuchukuwa hatua dhabiti za kumaliza migogoro ya ardhi kwa kushirikiana na pande zote husika zikiwemo mamlaka zinazoshughulikia mambo ya ardhi.
 
Chukueni hatua kuhakikisha kuwa maeneo yote ya magereza yanapimwa na kuwa na hati ili kuondokana kabisa na suala la migogoro ya ardhi. 
 
Kwa hatua za awali iwekwe mipaka kwa kupanda miti na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuzuia uvamizi zaidi. Gereza Ilagala kule Uvinza nimekuta mgogoro wa aina hiyo na nimetoa maelekezo ya hatua za kuchukua kumaliza jambo hilo. Gereza Bagamoyo kuna mgogoro wa aina hiyo pia. Kamishna Jenerali, tafadhali simamia upatikanaji wa suluhu ya mgogoro wa eneo la Gereza Bagamoyo. Si sawa askari wetu kutumia nguvu kwa wananchi ambao hawana silaha na kufungua kesi kila uchao wakati tunaweza kutumia mamlaka zilizopo kumaliza matatizo yanayotukabili. Nitafurahi kupata tarifa ya utatuzi wa mgogoro huu kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti ili tujue hatua zaidi za kuchukua.
 
Ndugu Wajumbe,
Eneo lingine muhimu ni uwajibikaji na kufanya kazi kwa weledi. Natumia fursa hii kuwakumbusha kufanya kazi zenu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazoongoza Jeshi. Ukiharibikiwa ukiwa unafuata Sheria utakuwa salama na sisi kama viongozi wako tutakuwa mstari wa mbele kukutetea. Ukifanya kinyume chake, tengeneza na mazingira ya gereza yawe mazuri kwa maana ni hakika maisha yako utayamalizia huko.
 
Vilevile, napenda nichukue nafasi kukumbushia umuhimu wa kukusanya maduhuli ya Serikali. Kumbukumbu zinaonesha kwamba Jeshi la Magereza kwa miaka kadhaa halijawahi kufikia malengo ya ukusanyaji wa maduhuli. 
 
Kwa mfano, mwaka wa fedha 2016/2017 Jeshi la Magereza lilijiwekea malengo ya kukusanya Tshs. 2,619,386,503.00, lakini hadi kufikia mwezi Februari, 2017 jumla Tshs. 840,617,933.70 zimekusanywa. Takwimu hizo zinaonesha kwamba uwezekano wa kufikia malengo ni mdogo sana.  Tumieni mkutano huu kujadili changamoto zinazowakwamisha kufikia malengo na kuja na mikakati ya kukabiliana nazo ili muweze kufikia malengo yenu. Serikali inafahamu changamoto nyingi mlizokuwa nazo ikiwemo uhaba na uduni wa vitendea kazi, madeni makubwa, miundombinu chakavu, uhaba na uchakavu wa nyumba za askari.  Wakati Serikali inafanyia kazi changamoto hizi, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu eneo hilo zifanyiwe kazi kwa umakini na pale ambapo Serikali inatakiwa iweke nguvu msisite kusema. Lakini lazima tubadili fikra zetu na kuacha kufanya kazi kwa utaratibu wa zamani wa kutegemea Serikali katika kila jambo wakati tumekalia rasilimali. Tutumie rasilimali zilizopo kutatua changamoto hizo na kile kidogo kinacholetwa na serikali kisaidie kukamilisha pale mnapokwama.
 
Kwa upande wa makazi mkoa wa Dar es salaam Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuguswa na changamoto hiyo aliahidi Tshs.10 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 320 eneo la Ukonga na hadi sasa tayari Tshs.5 bilioni zimetolewa tayari kwa kuanza mradi huo.  Naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais.
 
Wajumbe wa Mkutano,
Nitumie fursa hii kuwatia moyo katika utekelezaji wa maelekezo ya Serikali katika kuifanya Tanzania kuwa ya nchi ya Viwanda.  Ninazo taarifa kuhusu makubaliano ya Ubia na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF kufufua kilimo cha miwa na Kiwanda cha Sukari cha Gereza Mbigiri, Morogoro ambapo tayari matrekta yameanza kulima na ujenzi wa Kiwanda unategemea kuanza mwezi Mei, 2017 kazi ambayo inategemea kuchukua miezi nane.  Mradi huu utakapokamilika utaweza kuzalisha tani 30,000 kwa mwaka.  Ni matumaini yangu kwamba mradi huu utakapokamilika utakuwa umepunguza changamoto ya uhaba wa sukari nchini.  Vilevile, uwekezaji katika kiwanda cha Viatu Karanga, utakiongezea uwezo wa uzalishaji na kuwezesha kujenga Kiwanda kingine cha kuchakata ngozi.  Mradi huu pia utawezesha Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Taasisi zingine kuagiza viatu kutoka Kiwanda hicho badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.
 
Tumieni mkutano huu kuwa na majadiliano mapana ya namna gani ya kuweza kuwa wabunifu na kuongeza uzalishaji kwa kutumia fursa zilizopo na hivyo kusaidia kutatua matatizo mengine bila kutegemea Serikali Kuu.
 
Ndugu Kamishna Jenerali,
Ni matarajio yangu kuwa mara baada ya mkutano huu mtakuwa katika nafasi nzuri ya kuwa na mikakati thabiti ya kutatua changamoto zinazokwamisha utendaji kazi. Nitoe rai kwamba wekeni mikakati inayotekelezeka ambayo itawasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya chombo hiki muhimu.
 
Nihitimishe hotuba yangu kwa kurudia shukrani zangu kwa wale wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika kufanikisha kufanyika kwa mkutano huu.  Niwatakie mkutano mwema na wenye mafanikio.
 
Baada ya kusema hayo, sasa natamka kwamba Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza mwaka 2017 umefunguliwa rasmi.
 
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Back to Top