generica viagra

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Iliyotolewa na Msemaji wa Wizara Isaac Joel Nantanga Katika Kikao cha Waandishi wa Habari Kilichofanyika katika Ukumbi Wa Mikutano Ww Maelezo Jijini Dar Es Salaam Tarehe 11 Desemba, 2015

Friday, January 8, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeanza zoezi la kuhakiki Vyama vyote vya Kijamii vilivyopo hapa nchini, vilivyosajiliwa na Wizara Chini ya Sheria ya Vyama (Sura ya 337) iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002. Pamoja na kutaka kupata taarifa sahihi zaidi kuhusu vyama hivi, zoezi hili pia linalenga kuvifuta vyama vyote ambavyo vimeshindwa kutekeleza masharti ya kisheria kuhusu kulipa ada za mwaka, na kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa chama, na chama kuwasilisha taarifa za mapato na matumizi.
Vyama vya Kijamii vya Hiari vinavyosajiliwa chini ya Sheria ya Vyama ni pamoja na Vyama vya Hiari na Taasisi za Kidini.
Zoezi hili la kufanya uhakiki linavihusisha vyama 12,665 ambavyo vimesajiliwa katika Daftari la Msajili wa Vyama, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.  Tangu zoezi hili lianza mwezi Mei mwaka huu, vyama 1,268 vimeshafutwa na vingine 312 vimeridhia masharti ya Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO), chini ya Sheria Na. 24 ya mwaka 2002 yanayosimamiwa na iliyokuwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Aidha kwa sasa, vyama vingine 1,406 vimepewa kusudio la kufutwa na baada ya siku 21 kuanzia leo, kama vyama hivyo havitaonyesha sababu za msingi kwa nini visifutwe, vyama hivyo navyo vitafutwa.
Kifungu Na. 22 cha Sheria ya Vyama Sura 337, kikisomwa na Kanuni ya 6 ya Kanuni za Vyama zilizoundwa chini ya Kifungu Na. 38 cha Sheria ya Vyama, kwa pamoja kinazitaka Taasisi zote zilizosajiliwa chini ya Sheria hii kuwasilisha kila mwaka, kwa Msajili, taarifa za hesabu zilizokaguliwa, pamoja na taarifa za mapato na matumizi ya Taasisi husika.
Vilevile Taasisi husika inawajibika kulipa Ada ya mwaka kulingana na maelekezo ya Jedwali la 2 la Kanuni za Vyama.  Ili kurahisisha malipo haya ya ada, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imefungua Akaunti Maalumu yenye jina la MOHA Revenue Collection Na. 20110013811 ambapo Taasisi zinaweza kulipia ada zao katika Tawi lolote na NMB popote nchini.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inatoa angalizo kwa vyama vyote vya Kijamii kuendesha shughuli zake kwa kufuata Sheria na Kanuni zilizovianzisha, na kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani itaendelea kuvifuta vyama vyote vitakavyokiuka Sheria hii.
Wakati huohuo, Wizara imeanza msako wa Taasisii zinazofanya kazi zake nchini bila ya kuwa na usajili.  Msako huu umeanza baada ya kubaini kuwepo kwa Taasisi bubu nyingi hasa za kidini zinazoendesha shughuli zake kinyume  na Sheria ya Vyama.
Matokeo ya msako huu yatatolewa taarifa hapo baadaye.

Back to Top