generica viagra

Masauni Aitaka NIDA Kusajili Watu 15 Milioni Ifikapo Mwezi Juni, 2016

Tuesday, January 19, 2016

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuhakikisha ifikapo mwezi Juni mwaka huu watu milioni 15 kuwa wamekwisha kusajiliwa kama alivyo agiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alipofanya ziara yake Desemba mwaka jana.
Mhandisi Masauni alizungumza hayo kwa Watendaji  Wakuu wa Mamlaka hiyo jijini Dar es salaam alipofanya ziara yake ya kwanza katika Makao Makuu ya NIDA ili kujionea shughuli mbalimbali wanazofanya katika kukamilisha majukumu yao.
Aidha, Masauni alisema kuwa ni vema watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu ili kuhakikisha fedha za walipa kodi zinatumiwa vizuri pasipo kutapanywa.
“Uadilifu ni muhimu kwa sababu zoezi hili linatumia fedha nyingi za walipa kodi hivyo ni vema watumishi wakafanya kazi kwa uadilifu mkubwa,” alisema Masauni.
Katika mazungumzo yake na viongozi hao wa NIDA, Mhandisi Masauni alisema kuwa vitambulisho hivyo vya taifa ni muhimu kwa taifa letu kwani vitasaidia katika usalama wa nchi yetu kwa kutambua raia wake pamoja na kuchangia katika ongezeko la mapato ya serikali.
Pia, Mhandishi Masauni ametoa rai kwa wanaojihusisha na kutengeneza vitambulisho feki vya taifa kuacha mara moja kwani atakayebainika kuwa na kitambulisho feki ama kutengeneza vitambulisho feki atachukuliwa hatua za kisheria.
“Yeyote atakaebainika kutengeneza ama kumiliki kitambulisho feki basi atachukuliwa hatua za kisheria hivyo awe tayari kukabiliana na matokeo ya vitendo vyake,” alisema Masauni.
Pamoja na hayo Naibu Waziri Masauni ameipongeza NIDA kwa kuandaa Mpango Kazi utakaowawezesha kufikia malengo waliyojiwekea katika kukamilisha majukumu yao kama alivyo agiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Charles Kitwanga alipofanya ziara katika ofisi hizo.
(Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali – 15 Januari, 2016)

Back to Top