Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

USAJILI WA JUMUIYA ZA KIRAIA ZISIZO ZA KIDINI UMEANZA JIJINI DAR ES SALAAM LEO



MSAJILI wa Jumuiya za Kiraia nchini Emmanuel Kihampa amefungua zoezi la usajili wa jumuiya za kiraia zisizo za kidini Jijini Dar es Salaam, kuanzia leo Aprili 2, hadi Aprili 11 mwaka huu ambapo zoezi hilo litakuwa linaedeshwa kwenye ofisi za Wakuu wa Wilaya wa maeneo husika.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ndogo ya Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam, amesema usajili huo unahusisha vyama na vikundi visivyo vya kidini kuanzia vile vya kiuchumi kama vya wafanyabishara, wavuvi, wakulima, pia vyama vya kufa na kuzikana, kusaidiana kwenye shida na raha, ujirani mwema, umoja wa watu wanaoishi kwenye makazi, vyama vya kitamaduni kama vyama vya kiukoo, vyama vya kikabila, na vyama vya kikanda vyote vinatakiwa visajiliwe ili vitambulike kisheria.

Kihampa pia amesema usajili huo unahusisha vyama vya kitaaluma kama vyama vya waandishi wahabari, vyama vya madaktari, mafundi selemala na vyama vya wahitimu wa shule au vyuo.

Msajili alibainisha umuhimu kwa jamii kusajili vikundi hivi ni ikiwa ni pamoja na kuongeza tija kwenye vyama na vikundi husika.

"Utakuja kugundua kwamba kuna vyama na vikundi vinavyokutanisha wajasiriamali mbalimbali mfano wanaozalisha bidhaa za ngozi lakini usalishaji huo haupo kwenye kiwango cha ushindani katika soko la ndani au nje ya Nchi lakini kupitia usajili wa vyama hivi sekta husika wanaweza kufika kwenye vyama husika na kuwapatia mafunzo ya kuboresha bidhaa zao ili kuongeza tija kwenye usalishaji wao" alisema Kihampa

Katika hatua vyingine Msajili amevitadharisha vyama au vikundi ambavyo havitafanya usajili kwani kutofanya hivyo ni kosa kisheria kwani hatua za kijinai zinaweza zikachukuliwa kwa wale ambao wanaendesha vyama na vikundi bila kuwa na usajili kwa hiyo ni vyema wakachukua hatua stahiki kuvisajili ili waendeshe shughuli zao katika mazingira yenye usalama ya kuzingatia sheria za nchi yetu ili wasipate matatizo yoyote. Pia amebainisha mchakato wa kusajili chama au kikundi ni shilingi laki mbili mpaka kukamilika kwake.