NAIBU WAZIRI SILLO AKUTANA NA VIONGOZI WA USALAMA BARABARANI, AAHIDI USHIRIKIANO KUIMARISHA USALAMA BARABARANI

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, amekutana na Viongozi wa Usalama Barabarani kwa lengo la kutambulishwa kwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, SACP William Mkonda.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Februari 10, 2025, katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto jijini Dodoma, Naibu Waziri Sillo aliwapongeza viongozi hao kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha usalama barabarani unaimarika.
Aidha, alisifu juhudi zao za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya barabara, hatua ambayo inachangia kupunguza ajali zinazosababisha vifo, majeraha, na uharibifu wa miundombinu.
“Ninawapongeza kwa utekelezaji wa majukumu yenu ya kuhakikisha hali ya usalama barabarani inaendelea kuimarika, hasa kupitia utoaji wa elimu kwa Watanzania, jambo linalosaidia kupunguza ajali nchini,” alisema Sillo
Mhe. Sillo aliwahakikishia viongozi hao kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea kushirikiana nao katika kutekeleza majuku yao ya kusimamia Usalama barabarani sambamba na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zitakazojitokeza.
Pia, aliwasisitiza Viongozi hao dhamira ya Serikali ya kupunguza ajali barabarani na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara unaimarika zaidi.