Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

KAMATI YA NUU YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA UJENZI WA OFISI YA KAMANDA WA POLISI MKOA WA MANYARA



Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) imeeleza kuridhishwa na hatua ya utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara unaoendelea katika eneo la Komoto, Babati Mjini, ambapo hadi sasa umefikia asilimia 60 ya ukamilishaji wa mradi huo.


Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo Aprili 6, 2025, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vicent Mbogo (Mb), kwa niaba ya Kamati amepongeza Jeshi la Polisi kwa usimamizi mzuri na matumizi bora ya rasilimali katika kutekeleza mradi huo muhimu kwa uboreshaji wa mazingira ya utendaji kazi.


Mradi huo unaotekelezwa kwa mfumo wa Force Account unakadiriwa kugharimu Shilingi Bilioni 1.6 hadi kukamilika kwake, ambapo unalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara na Maofisa wake.


Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Kija Sweetbetus Mkoyi, amesema kuwa kazi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na ujenzi wa kuta za ndani na nje ufungaji wa mfumo wa maji safi na taka, umeme, pamoja na upakaji wa rangi.


Aliongeza kuwa kazi zilizobaki ili kukamilisha jengo hilo ni uwekaji wa Marumaru, ujenzi wa uzio, ufungaji wa madirisha ya vioo, mfumo wa mawasiliano na ulinzi pamoja na kukamilisha mandhari ya nje.


Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara limemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi hilo kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, sambamba na kutoa pongezi kwa Kamati hiyo ya Bunge kwa usimamizi thabiti na kusaidia upatikanaji wa fedha hizo.