MHE. SILLO AISHUKURU SERIKALI KWA KUBORESHA MAZINGIRA YA KAZI

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha Sekta ya usalama na kuweka mazingira wezeshi ya kazi katika Wizara hiyo.
Mhe. Sillo ameyasema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, uliofanyika Aprili 29, 2025, katika Ukumbi wa Jeshi la Magereza jijini Dodoma.
Amesema kuwa chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia, bajeti ya Wizara imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, jambo lililochangia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Vyombo vya Usalama vilivyo chini ya Wizara hiyo.
Aidha, Mhe. Sillo amewataka Watumishi wote kuwa sehemu ya juhudi za kuendeleza usalama, amani na utulivu wa Taifa kwa kushirikiana, kuwajibika na kudumisha nidhamu ya kazi.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya Wizara hayawezi kufikiwa pasipo mshikamano wa viongozi na watumishi, ushirikiano kati ya Menejimenti na Watumishi, pamoja na moyo wa kujituma katika kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Ally Gugu, amesema kuwa Wajumbe wa mkutano huo watapata fursa ya kuchangia kwa kutoa maoni, mapendekezo na ushauri. Aliongeza kuwa hoja zilizojadiliwa katika kikao hicho zimewasilishwa kwa Mgeni Rasmi kwa ajili ya utekelezaji.
Naye Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, CGP Jeremiah Katungu amesema kuwa kikao cha Baraza ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Vyombo vya Usalama. Aidha, amebainisha kuwa msingi wa kikao hicho ni kuimarisha umoja, ushirikiano na utendaji kazi bora miongoni mwa Idara na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.