NAIBU WAZIRI SILLO AWAJULIA HALI MAJERUHI WA AJALI SAME

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, amefika katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Hospitali ya Mawenzi, na Hospitali ya Wilaya ya Same leo Juni 29, 2025, kwa ajili ya kuwapa pole na kuwajulia hali majeruhi wa ajali iliyotokea jana Juni 28, 2025, Wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.
Ajali hiyo iliyohusisha basi la Kampuni ya Chanel One na gari dogo aina ya Coaster (Rosa) imesababisha vifo vya watu 38 na kujeruhi watu wengine 30. Mhe. Sillo ameeleza masikitiko yake kutokana na tukio hilo na kutoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, huku akiwatakia majeruhi uponaji wa haraka.
Katika ziara hiyo, Mhe. Sillo ameambatana na Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, SACP William Mkonda, pamoja na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Awadhi Juma ambapo wametembelea pia eneo la tukio iliyotokea ajali hiyo
Aidha, Naibu Waziri Sillo ametoa wito kwa Madereva wote kuzingatia Sheria za usalama barabarani na kuwa waangalifu wakati wote ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Mhe. Sillo ameongeza kuwa Serikali kupitia Vyombo vya Usalama itaendelea kuchukua hatua kali kwa wote watakaokiuka Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa magari ya abiria pamoja na kutoa elimu kwa Madereva.