MAGEREZA KUFUFUA KIWANDA CHAKE CHA SUKARI NA KILIMO CHA MIWA MOROGORO

Tuesday, July 11, 2017

 
 
 
Na Christina R. Mwangosi
 
Jeshi la Magereza nchini limeanza kutekeleza mpango wake wa kufufua Kiwanda chake cha  Sukari na  Kilimo cha Miwa katika Gereza la Mbigiri mkoani Morogoro kwa lengo la kuongeza kiwango cha upatikanaji wa sukari hapa nchini ikiwemo kutoa fursa za ajira kwa watanzania.
Pamoja na kiwanda hicho kuongeza upatikanaji wa sukari hapa nchini lakini pia kufufuliwa kwa kiwanda hiki kutatoa fursa ya ajira Wananchi ambao watafanya kazi kwenye Kiwanda hicho kwa ujumla.
Katika kutekeleza mpango huo hatua za awali za Upembuzi yakinifu umeshafanyika na shughuli za kilimo tayari zimeanza katika eneo hilo kwa kutumia maktrekta matatu mapya ya kisasa ambayo hadi sasa yameshalima ekari 1000.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini Dk. Juma Malewa anasema kuwa katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda, Jeshi la Magereza limeainisha baadhi ya Miradi inayoweza kuiweka Tanzania katika Uchumi wa Viwanda ikiwemo ufufuaji wa Kiwanda hicho na Kilimo cha Miwa katika Gereza lake la Mbigiri Mkoani Morogoro.   
Dk. Malewa anasema kuwa  kwa kushirikiana na  Mifuko ya Hifadhi ya Jamii PPF na NSSF,  Jeshi la Magereza  limeanza zoezi  la kufufua  Kiwanda cha Sukari na  Kilimo cha Miwa katika Gereza la Mbigiri mkoa wa Morogoro.
Dk. Malewa anasema Kiwanda hicho kilisitisha shughuli zake za uzalishaji tangu mwaka 1996 kutokana na uchakavu wa miundombinu na teknolojia duni iliyokuwepo kwa wakati huo.
Anasema Ubia kati ya Jeshi la Magereza na Mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii utawezesha kujengwa kwa Kiwanda kipya cha kisasa ambacho kinategemewa kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa  kuzalisha sukari tani 30,000 kwa mwaka, kiwango ambacho kitasaidia kuongeza upatikanaji wa sukari hapa nchini.
 “Ni matumaini  yetu  hadi kufikia  mwisho wa mwaka huu kiwanda hiki kitaanza kufanya kazi… ufufuaji wa kiwanda hiki utawaneemesha  wakulima wadogo wadogo  wa miwa (Outgrowers)  waliopo  maeneo yanayolizunguka  gereza la Mbigiri mkoa wa  Morogoro na hivyo kuinua hali zao za kiuchumi kwa kuwa itakuwa ni fursa ya wakulima hao kupata soko la uhakika na karibu zaidi kwa ajili ya kuuza bidhaa zao baada ya kuvunwa kwenye mashamba yao’’. Dk.  Malewa  anasisitiza.
Dk. Malewa anasema kuwa pamoja na ardhi yenye rutuba ambayo kwa Jeshi la Magereza linaiona ni fursa ikitumiwa vizuri lakini pia ipo Miundombinu mbalimbali inayoweza kusaidia kuanzisha Viwanda na ardhi hii inaweza kutumika katika shughuli za kilimo na hivyo kuongeza uzalishaji wa chakula hapa nchini. 
Anasema wafungwa wengi na wa kutosha waliopo ndani ya Jeshi hilo watatumika   katika shughuli mbalimbali za uzalishaji utakaofanyika katika maeneo ya viwanda na mashamba makubwa ya uzalishaji wa chakula yaliyopo kwenye Magereza mbalimbali.
Dk. Malewa anasema kuwa katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda, Jeshi la Magereza tayari limeainisha baadhi ya Miradi inayoweza kuiweka Tanzania katika Uchumi wa Viwanda.
Jeshi la Magereza nchini lina fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza   kuwa na mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu na hivyo kufikia malengo yetu ya kuwa na uchumi wa viwanda. Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na ardhi nyingi yenye rutuba inayofaa kutumika kwa kushughuli za kilimo.
Dk. Malewa anasema pia Jeshi la Magereza lina Mpango wa kuanzisha shughuli za kilimo cha kisasa cha Umwagiliaji na kwa sasa lipo kwenye maandalizi ambapo umwagiliaji mkubwa unaandaliwa katika Gereza la Idete mkoani Morogoro ambapo kutokana na ukubwa wa eneo hilo lenye zaidi ya ekari 3000 zinazoweza kutumika kwa shughuli za kilimo litakuwa na uwezo wa kuzalisha tani za kutosha  za zao la Mpunga na hivyo kutosheleza mahitaji ya chakula cha wafungwa kwa wastani wa asilimia 50. Katika maandalizi ya awali tayari ekari 1000 zimeshaandaliwa ikiwa ni sehemu ya maandalizi hayo.
Anasema Mradi huo wa kuendesha kilimo cha kisasa na hivyo kulifanya Jeshi hilo kujitosheleza kwa chakula cha kulisha wafungwa wanaotumikia vifungo vyao kwenye Magereza mbalimbali hapa nchini ulioanza mwaka 2015 na kutarajiwa kukamilika mwaka 2020 utagharimu jumla ya shilingi bilioni 15 za kitanzania mpaka utakapokamilika na katika maandalizi ya awali upatikanaji wa mbolea, pamoja na matrekta ya kisasa 50 yatasaidia kuboresha shughuli za kilimo hicho cha kisasa.      
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini Dk. Juma Malewa anasema maboresho ya kilimo cha kisasa yanayoendelea ndani ya Jeshi hilo yatalifanya Jeshi hilo kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2020 wakati  shughuli za kilimo zinazofanyika kwa sasa katika maeneo mbalimbali ya Magereza nchini yanaliweza jeshi hilo kujitosheleza kwa asilimia 20 tu.
Dk. Malewa anasema mazao yatakayolimwa kwa wingi ni pamoja na Mpunga, Mahindi, Maharage pamoja na Alizeti kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta.
Anasema Magereza ambayo yatatumika kwa ajili ya shughuli za kilimo cha kisasa ni pamoja na Gereza la Kitai mkoani Ruvuma, Kitengule mkoani Kagera, Molo Sumbawanga, Idete na Mbigiri mkoani Morogoro, Kwitanga mkoani Dodoma na Gereza la Arusha.
Aidha katika kujitosheleza kwa chakula Jeshi la Magereza pia limejipanga kuendeleza ufugaji wa ng’ombe wa nyama, maziwa, kuku, nguruwe katika Magereza mbalimbali nchini likiwemo Gereza la Ubena- Morogoro, Pwani  Mugumu-Mara Kitengule-Kagera na Mbigiri-Morogoro pamoja na Gereza la KPF-Kingolwira Morogoro.
Kwa mujibu wa Dk. Malewa  Jeshi la Magereza limeweka  Mkakati  wa kupata Matrekta na Vyombo vya kisasa vya kilimo  ambavyo vitatumika kuboresha  shughuli za Kilimo katika jeshi hilo.
Kuhusu wataalamu Dk. Malewa anasema Jeshi la Magereza lina wataalumu wa kutosha waliobobea katika shughuli za kilimo cha kisasa ambao watatumika katika kufanikisha mpango huo.
Dk. Malewa anasema Jeshi la Magereza kwa sasa lina jumla ya hekta 130,000 na kati ya eneo hilo hekta 60,540  ndizo zinazoweza  zikatumika  kwa shughuli za Kilimo na ufugaji, eneo lililosalia ni eneo la  makazi ya askari, mawe pamoja na miamba.
Katika utekelezaji wa mpango huu wa miaka mitano Jeshi la Magereza litatumia wafungwa katika Nyanja mbili moja ni kwa upande wa uzalishaji na nyingine ni ile kuwafundisha wafungwa wenyewe kilimo cha kisasa ujuzi ambao watautumia mara watakapomaliza kutumikia vifungo vyao kwenye Magereza mbalimbali hapa nchini jambo litakalosaidia wafungwa hao kutorudia kujishughulisha na matukio ya uhalifu.
 

Back to Top