HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. KANGI ALPHAXARD LUGOLA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2019/20

Thursday, April 25, 2019

HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. KANGI ALPHAXARD LUGOLA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA
FEDHA KWA MWAKA 2019/20
 

 1. UTANGULIZI

 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa lipokee, lijadili na lipitishe Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka 2019/20.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo haya nitakayoyasoma naomba hotuba yangu yote iingie kwenye Hansad kama ilivyowasilishwa mezani kwako.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuwasilisha Hotuba hii kwa mara ya kwanza nikiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Vilevile, namshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniteua kusimamia Wizara hii nyeti inayoshughulikia amani, usalama wa raia na mali zao. Aidha, nampongeza Mhe. Rais kwa uongozi wake madhubuti ambao umefanikisha utekelezaji wa mambo mbalimbali ikiwemo miradi mikubwa ya kitaifa. Ni dhahiri kuwa wananchi wengi wana imani na matumaini makubwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayosimamia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 katika kuelekea kwenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, nawapongeza Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb.) kwa uongozi wao na miongozo ambayo imetoa dira katika kuboresha utendaji wa Wizara na Serikali kwa ujumla.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pia nakupongeza wewe binafsi na Naibu Spika kwa uongozi wenu mahiri katika uendeshaji wa shughuli za Bunge. Aidha, namshukuru Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb.) Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Wajumbe wa Kamati hiyo na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushauri wao unaolenga katika kuimarisha utendaji wa Wizara.

 

 1. UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA WIZARA KWA MWAKA 2018/19 NA MALENGO YA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2019/20

 
    Mapato na Matumizi ya Fedha
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara iliidhinishiwa bajeti ya jumla ya Shilingi bilioni 945.5 kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 521.5 ni kwa ajili ya Mishahara, Shilingi bilioni 385.7 ni za Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni 38.3 ni fedha za Miradi ya Maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi, 2019 fedha zilizopokelewa na Wizara ni jumla ya Shilingi bilioni 813.7. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 74 zilikuwa ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, Shilingi bilioni 368.8 ni Mishahara na Shilingi bilioni 370.9 zilikuwa kwa ajili ya Matumizi Mengineyo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara ilikuwa na lengo la kukusanya mapato ya Shilingi bilioni 297. Hadi kufikia mwezi Machi, 2019 jumla ya Shilingi bilioni 204.8 zilikuwa zimekusanywa sawa na asilimia 68.9 ya lengo.

 
    Mafanikio ya Wizara
 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kutekeleza kazi na majukumu yake, ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2019 imepata mafanikio mbalimbali yakiwemo: kuendelea kuwepo kwa amani, utulivu na usalama nchini kulikowezesha kuimarika kwa shughuli za uchumi na kijamii, ambapo hali ya uhalifu imepungua kwa kiasi kikubwa; kuimarisha usimamizi wa Sheria za Usalama Barabarani kulikosababisha kupungua kwa makosa ya barabarani kwa asilimia 38; kukamilika kwa Mkakati wa Kujitosheleza kwa Chakula wa Jeshi la Magereza na kuanza utekelezaji wake; kufungwa kwa mtambo na mashine mpya katika Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kilichopo Gereza Karanga Moshi; na kufanikiwa kuzima moto na kufanyika kwa uokoaji katika matukio 1,785.

 
 

 1. Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni kukamilika kwa jengo la kuanzia la ofisi za Makao Makuu ya Wizara eneo la Mtumba Jijini Dodoma; kuzinduliwa kwa mfumo wa kielektroniki wa kutoa vibali vya ukaazi (e-Permit) na Viza (e-Visa); kutunukiwa Tuzo kwa Pasipoti Mpya ya Tanzania ya Kielektroniki kuwa Pasipoti bora katika Ukanda wa Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika; kuanza utaratibu unaowezesha wananchi kupata nakala ya Kitambulisho cha Taifa  kupitia Tovuti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa; na kukamilika kwa mfumo wa kielektroniki wa usajili wa Jumuiya za Kijamii (Societies Management System).

 
      Maeneo ya Kipaumbele kwa Mwaka 2019/20
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Wizara imeweka kipaumbele katika maeneo yafuatayo: kuendelea kudumisha usalama wa raia na mali zao kwa kufanya doria, misako, operesheni mbalimbali; kuboresha mazingira ya ofisi na makazi ya Askari na watumishi raia; na kuwaongezea ujuzi watumishi raia na Askari kwa kuwapa mafunzo ya ndani na nje ya nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vipaumbele vingine ni kuendelea kutekeleza Mkakati wa Jeshi la Magereza wa Kujitosheleza kwa Chakula; kuendelea kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu kwa kuimarisha usimamizi wa Sheria husika; kuimarisha utendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza; kununua magari na vifaa vya kuzima moto na uokoaji; kuimarisha huduma za uhamiaji mtandao (e-immigration) kwa kuanzisha e-border management systerm na kuunganisha e-visa, e-permit na e-passport katika ofisi za kibalozi nje ya nchi; na kuongeza kasi ya utambuzi, usajili na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.

 
 
    JESHI LA POLISI
 
    Hali ya Usalama Nchini
 

 1. Mheshimiwa Spika, hali ya amani, utulivu na usalama nchini imeendelea kuimarishwa na kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kukua zaidi. Kwa ujumla hali ya uhalifu nchini imepungua kwa kiasi kikubwa. Katika kutimiza jukumu hilo Jeshi la Polisi limeimarisha misako, doria na operesheni kwa kutumia mbinu mbadala za kudhibiti uhalifu sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili jamii ibadilike na kuachana na uhalifu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019 jumla ya makosa makubwa ya jinai 45,574 yaliripotiwa katika Vituo vya Polisi nchini ikilinganishwa na makosa 47,236 yaliyotokea katika kipindi kama hicho mwaka 2017/18. Upelelezi wa makosa hayo umefanyika na kesi 17,631 zikiwa na watuhumiwa 37,267 zilifikishwa mahakamani. Katika kuhakikisha kesi zinapelelezwa kwa haraka, Jeshi la Polisi kwa mwaka 2019/20 litaongeza ufanisi katika utendaji wa Maabara ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai kwa kuongeza vifaa vya kisasa na kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Askari wapelelezi ndani na nje ya nchi. Aidha, Jeshi litakamilisha taratibu za kisheria ili maabara yake ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) isajiliwe na Mkemia Mkuu wa Serikali na kuiwezesha kufanya kazi sambamba na Maabara ya Uchunguzi wa Kikemia.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti uhalifu wa matumizi ya silaha, operesheni mbalimbali zimefanyika, ambapo jumla ya silaha 351 na risasi 4,844 za aina mbalimbali zilikamatwa. Aidha, kupitia operesheni hizo jumla ya watuhumiwa 239 walikamatwa na kufikishwa Mahakamani. Katika mwaka 2019/20 Jeshi la Polisi kupitia Shirika lake la Uzalishaji Mali litaanza kufanya mafunzo ya matumizi ya silaha za moto kwa Mashirika ya Umma, Kampuni Binafsi za Ulinzi na wamiliki binafsi wa silaha kwa lengo la kuimarisha matumizi sahihi na ulinzi wa maeneo yao. Natoa wito kwa wamiliki na watumiaji wote wa silaha za moto kushirikiana na Jeshi la Polisi kutekeleza matakwa haya ya kisheria.

 
    Hali ya Usalama Barabarani

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2018 hadi Machi, 2019 jumla ya matukio 2,593 yameripotiwa ikilinganishwa na matukio 4,180 yaliyoripotiwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2017/18. Aidha, takwimu zinaonesha kuwa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani vimepungua kwa asilimia 38.7. Kupungua kwa ajali na vifo kumetokana na usimamizi mzuri wa Sheria za Usalama Barabarani; ushirikiano na wadau, sambamba na kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuzingatia Sheria.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Jeshi litaendelea kusimamia Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Aidha, utaratibu wa kupata ridhaa ya Serikali kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 unaendelea. Muswada wa Sheria hiyo utawasilishwa Bungeni katika mwaka 2019/20.

 
 Miradi ya Ujenzi wa Makazi, Ofisi na Vituo vya Polisi
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya kazi na makazi ya Askari Jeshi la Polisi linatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba 400 kwa gharama ya Shilingi bilioni 10 zilizotolewa mwaka 2018 na Mhe. Rais. Hadi kufikia mwezi Machi 2019, awamu ya kwanza ya mradi unaojumuisha ujenzi wa nyumba 148 upo katika hatua ya umaliziaji katika mikoa nane (8) ya Dodoma, Katavi, Kaskazini Pemba, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Njombe, Pwani na Simiyu. Aidha, awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 252 upo katika hatua mbalimbali za ujenzi katika mikoa 24. Mradi huu umepangwa kukamilika mwezi Juni, 2019.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, kwa kutumia Mfuko wa Tuzo na Tozo Jeshi la Polisi linatekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 107. Kati ya nyumba hizo 100 zinajengwa mkoani Dodoma, ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 30 upo katika hatua ya umaliziaji na nyumba 70 zitajengwa baada ya awamu ya kwanza kukamilika. Aidha, ujenzi wa jengo moja la kuishi familia saba (7) Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita umekamilika. Pia, kwa kutumia Mfuko huo Jeshi la Polisi linaendelea na ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu ya Polisi Jijini Dodoma ambao umefikia hatua ya umaliziaji. Pia, wananchi na wadau wameendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika ujenzi wa nyumba za kuishi familia 13 na ujenzi wa Vituo vya Polisi 11 katika mikoa mbalimbali. 

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi litaendelea kushirikisha wadau mbalimbali katika ujenzi wa Vituo vya Polisi, ofisi na makazi ya Askari nchini kote. Hivyo, natumia fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika miradi hiyo ili kuweza kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika maeneo husika.

 
 
 
 
Uboreshaji wa Vyuo vya Polisi

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha Vyuo vya Polisi nchini, Jeshi la Polisi limefanya upanuzi wa miundombinu ya majengo ya Shule ya Polisi Tanzania (TPS) iliyopo Moshi. Ujenzi wa mabweni manne yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 320, majengo mawili (2) ya madarasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 612 na jengo moja (1) la ofisi umekamilika. Mradi huu umefadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa gharama ya Shilingi bilioni 20.4. Hivyo, natumia fursa hii kwa niaba ya Serikali kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuboresha Shule ya Polisi Moshi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Jeshi la Polisi limeanza ukarabati wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam kwa kutumia Shilingi milioni 700 zilizotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli.

 
                Kuongeza Rasilimaliwatu katika Jeshi  la Polisi
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Jeshi la Polisi limeajiri Askari wapya 812 kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kazi za Polisi. Askari hao wamehitimu mafunzo ya awali katika Shule ya Polisi Moshi tarehe 09 Aprili, 2019. Aidha, jumla ya Askari 3,725 wanatarajiwa kuajiriwa katika mwaka 2019/20.

 
Upatikanaji wa Vitendea Kazi kwa Jeshi la Polisi

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuboresha utendaji kazi, Jeshi la Polisi limepokea magari 144 na makasha (containers) matatu (3) ya vipuri kutoka Kampuni ya Ashok Leyland ya India. Jeshi pia limepata magari 18 na pikipiki 17 kupitia misaada ya taasisi na wadau mbalimbali.

 
Matukio ya Kutekwa na Kuuawa kwa Watoto
 

 1. Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba na Desemba, 2018 yaliibuka matukio ya mauaji na utekaji wa watoto katika Mikoa ya Njombe na Simiyu. Katika Mkoa wa Njombe watoto sita waliuawa na watatu walitekwa, ambapo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwapata watoto waliotekwa wakiwa hai. Kutokana na matukio hayo, watuhumiwa saba walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria. Vilevile, katika Mkoa wa Simiyu kulitokea mauaji ya watoto wanne, ambao waliuawa na kukatwa baadhi ya viungo. Kufuatia tukio hilo watuhumiwa 12 walikamatwa na kufikishwa Mahakamani. Taarifa za kiintelijinsia zilibainisha viini vya matukio hayo ni imani za kishirikina. Aidha, Wizara kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kutoa elimu kwa wananchi, hususan wazazi na walezi kuwa na uangalizi wa karibu kwa watoto wao wanapokwenda na  kurudi shuleni na wanapokuwa majumbani.

 
  Usimamizi wa Nidhamu za Askari
 

 1.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 hatua za kinidhamu zimeendelea kuchukuliwa kwa Maafisa, Wakaguzi na Askari Polisi waliobainika kujihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili mema ya Jeshi la Polisi. Jumla ya Askari 130 wa vyeo mbalimbali, Maafisa 28, Wakaguzi 14 na Askari 88 wamechukuliwa hatua za kinidhamu na za kisheria. Maafisa wawili, Wakaguzi saba na Askari 88 walishtakiwa kijeshi, Askari 35 walipewa adhabu ya kufukuzwa kazi, Askari watatu walifikishwa Mahakamani na Askari wawili walishushwa vyeo. Aidha, Maafisa 25 na Wakaguzi wanne waliandikiwa barua za onyo, kujieleza na tahadhari.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Wizara kupitia Jeshi la Polisi itaimarisha upekuzi wa Askari na vijana wanaoomba kujiunga na Jeshi ili kuwa na Askari wenye nidhamu na moyo wa dhati wa kulitumikia Jeshi na Taifa kwa ujumla. Aidha, Wizara itaendelea kuchukua hatua stahiki kwa Maafisa na Askari wasiozingatia maadili ya Jeshi vikiwemo vitendo vya kuomba na kupokea rushwa, kubambikiza kesi na kushiriki kwenye matukio ya uhalifu.

 
 
 JESHI LA MAGEREZA
       
 Hali ya Ulinzi na Usalama Magerezani

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Jeshi la Magereza imeendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika magereza yote nchini. Katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019 kulikuwa na jumla ya wafungwa na mahabusu 38,501. Kati ya hao, wafungwa ni 19,395 na mahabusu 19,106. Idadi hii imekuwa ikisababisha msongamano wa wafungwa hasa katika magereza yaliyopo katika miji mikubwa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na msongamano wa wafungwa magerezani, Wizara inaendelea kutumia njia mbalimbali za kupunguza msongamano huo ikiwemo: msamaha wa Mhe. Rais, ambapo jumla ya wafungwa 4,477 walinufaika, wafungwa 91 walinufaika na utaratibu wa mpango wa Parole kupitia Sheria ya Bodi za Parole Sura ya 400 ya mwaka 2002; wafungwa 788 walinufaika na utaratibu wa kifungo cha nje; wafungwa 3,629 walihukumiwa kutumikia adhabu zao nje ya magereza kupitia Programu ya Adhabu Mbadala ya Kifungo cha Gerezani. Takwimu hizo ni kwa kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019. Vilevile, Jeshi limekamilisha ujenzi wa magereza mawili ya Mahabusu ya Chato – Geita na Ruangwa - Lindi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Wizara itaendelea kudhibiti msongamano wa wafungwa magerezani kwa kutumia njia zilizotajwa hapo juu. Aidha, Jeshi la Magereza limeongeza bajeti ya shughuli za Parole kutoka Shilingi milioni 116.5 mwaka 2018/19 hadi Shilingi milioni 241.3 mwaka 2019/20. Pia, Wizara inatarajia kuongeza Mikoa ya Katavi, Lindi na Ruvuma katika kutekeleza Programu ya Adhabu Mbadala ya Kifungo cha Gerezani na hivyo kufikia mikoa yote ya Tanzania Bara. Aidha, Wizara itaendelea kuharakisha uandaaji wa taarifa za uchunguzi ili kuhakikisha wahalifu na wafungwa wa vifungo vya muda mfupi usiozidi miaka mitatu wanatumikia adhabu mbadala nje ya magereza na hivyo kusaidia kupunguza msongamano magerezani.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi pia limeimarisha upekuzi ili kubaini vitu visivyoruhusiwa kuingizwa magerezani na kudhibiti vitendo viovu. Katika kufikia azma hiyo, utekelezaji wa mpango wa kufunga mfumo wa kisasa wa ulinzi wa kielektroniki umeanza kutekelezwa katika Magereza makubwa ya Mkoa wa Dar es Salaam (Ukonga, Keko na Segerea). Katika mwaka 2019/20 Jeshi litakamilisha kazi hii pamoja na kuanza kufunga mfumo huo katika Gereza Arusha na Gereza Isanga - Dodoma. Zoezi hili litaendelea kutekelezwa katika Magereza yote nchini kulingana na upatikanaji wa fedha.

 
Mkakati wa Kujitosheleza kwa Chakula
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais, Jeshi la Magereza limeandaa Mkakati wa miaka mitano (2018/19 – 2022/23) wa Kujitosheleza kwa Chakula cha Wafungwa na Mahabusu. Mkakati huo umejielekeza katika kuzalisha mazao muhimu ya chakula ambayo ni mahindi, mpunga na maharage. Mkakati husika umeanza kutekelezwa katika magereza kumi (10) ya Arusha, Idete, Kiberege, Kitai, Kitengule, Ludewa, Mollo, Nkasi, Pawaga na Songwe kwa kutenga jumla ya ekari 12,370.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, katika msimu wa kilimo 2018/19, Jeshi la Magereza limelima na kupanda eneo lenye jumla ya ekari 5,395 katika magereza hayo. Matarajio ni kuvuna tani 6,299 za mahindi, tani 3,228 za mpunga na tani 568 za maharage. Pamoja na Mkakati huo, magereza mengine yataendelea na shughuli za kilimo zikiwemo mbogamboga na matunda kwa utaratibu wa kuwekewa malengo ya uzalishaji. Hatua nyingine zilizochukuliwa katika kuboresha shughuli za kilimo ni ununuzi wa matrekta kumi (10) na zana zake ambayo yamesambazwa katika Magereza mbalimbali.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Jeshi la Magereza litaendelea kutekeleza Mkakati wa Kujitosheleza kwa Chakula cha Wafungwa na Mahabusu kwa kulima jumla ya ekari 8,150 za mazao mbalimbali.

 
Kuboresha Makazi ya Watumishi wa Jeshi la Magereza na Mabweni ya Wafungwa na Mahabusu
 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza linaendelea kujenga nyumba za makazi ya Askari katika vituo mbalimbali nchini. Jukumu hili linatekelezwa kupitia mpango unaoelekeza Wakuu wa Vituo kutumia nguvu kazi ya Askari, wafungwa na rasilimali zilizopo katika maeneo yao. Hadi kufikia mwezi Machi, 2019 jumla ya nyumba 129 zimekamilika na nyumba 264 zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Gharama za kukamilisha nyumba hizo ni Shilingi bilioni 1.8.

 
  Ajira kwa Jeshi la Magereza
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Jeshi la Magereza linatarajia kuajiri Askari 685. Pia, Jeshi litatoa mafunzo ya muda mfupi ya ndani ya Jeshi kwa lengo la kuboresha utendaji. Mafunzo hayo yatahusisha wataalam wa usimamizi wa rasilimali za Serikali, Kumbukumbu na Nyaraka za Serikali kwa lengo la kuboresha utendaji ndani ya Jeshi la Magereza.

     
 Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza
 

 1. Mheshimiwa Spika, Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza limekamilisha ujenzi wa majengo ya ofisi za kuanzia kwa ajili ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; na Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu katika eneo la Mtumba Jijini Dodoma. Aidha, ujenzi wa ukuta wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Jijini Dodoma unaendelea. Kazi zote zilizotajwa zina thamani ya Shilingi bilioni 3.5.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Shirika kupitia Kampuni ijulikanayo kama Karanga Leather Industries Company Limited limeboresha kiwanda cha viatu cha zamani kilichopo eneo la Gereza Karanga Moshi. Uboreshaji huo umefanyika kwa kuongeza mtambo na mashine mpya. Kwa sasa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha jozi 400 za viatu kwa siku ikilinganishwa na jozi 150 zilizokuwa zikilizalishwa awali.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza pia linatengeneza samani mbalimbali katika viwanda vyake vilivyopo Ukonga - Dar es Salaam, Uyui - Tabora na Arusha. Katika mwaka 2018/19 viwanda hivyo vimepokea zabuni za kutengeneza samani zenye jumla ya Shilingi 1,339,199,763.97. Zabuni hizo zilitoka katika Taasisi za Serikali na watu binafsi na zitakamilika kabla ya Juni, 2019.

 
 JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeshiriki katika kuzima moto na kufanya uokoaji katika matukio 1,785 nchi nzima. Jeshi pia limefanya ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto katika majengo 34,395 na magari 4,786. Kutokana na ukaguzi huo kiasi cha Shilingi bilioni 4.5 kilikusanywa. Katika mwaka 2019/20 Jeshi litaendelea na ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto ili kuzuia na kupunguza matukio ya moto nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika hatua za kudhibiti majanga ya moto elimu imeendelea kutolewa kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo vipindi vya runinga 45 na vipindi vya redio 331. Aidha, katika kukabiliana na matukio ya moto katika shule za Msingi na Sekondari, Jeshi limefungua jumla ya Vilabu vya Zimamoto 34 kwa ajili ya kutoa elimu katika shule za Msingi na Sekondari. Elimu hiyo itaendelea kutolewa kwa umma katika mwaka 2019/20. 

 
Hali ya Vitendea Kazi vya Kuzima Moto na Uokoaji
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na upungufu wa vitendea kazi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika mwaka 2018/19 limepata jumla ya magari 16. Vilevile, Jeshi limepokea msaada wa kontena lenye vifaa vya kuzima moto na uokoaji kutoka Ujerumani.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 jumla ya Shilingi bilioni 3.75 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa magari matano (5) ya kuzima moto. Hadi kufikia Machi, 2019 kiasi cha Shilingi bilioni 3 kimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa magari hayo, ambayo yataletwa nchini mwaka 2019/20. Aidha, jumla ya Shilingi bilioni 4.5 zimetengwa katika mwaka 2019/20, kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 3.75 ni kwa ajili ya ununuzi wa magari mengine matano (5) na Shilingi milioni 750 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kuzima moto na uokoaji.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kazi ya kuzima moto pia inahitaji uwepo wa visima vya kuhifadhia maji katika maeneo mbalimbali. Visima vilivyopo kwa sasa ni 2,042 nchi nzima ikilinganishwa na mahitaji ya visima 285,000. Kati ya visima vilivyopo, visima 692 vinafanya kazi na visima 1,350 ni vibovu.  Natumia fursa hii kutoa wito kwa Mamlaka za Maji katika mikoa mbalimbali, kutekeleza jukumu lao la kufanya matengenezo ya visima hivyo ili kuwezesha kazi ya kuzima moto kufanyika kwa wakati na ufanisi.

 
 Ajira kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa rasilimaliwatu, mwaka 2019/20 Jeshi la Zimamoto na uokoaji linatarajia kuajiri Askari 500. Pia, Jeshi litawapandisha vyeo Maafisa na Askari 1,343 kwenye ngazi mbalimbali.

 
 
HUDUMA ZA UHAMIAJI
Utekelezaji wa Mradi wa Uhamiaji Mtandao
 

 1. Mheshimiwa Spika, tarehe 26 Novemba, 2018 Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alizindua mfumo wa kielektroniki wa kutoa vibali vya ukaazi (e-permit) pamoja na Visa (e-Visa). Mfumo huo unamwezesha mteja kutuma maombi yake kwa njia ya mtandao. Aidha, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kudhibiti watu wanaoingia na kutoka nchini (e-border Management Control System). Mfumo huu utaanza kutumika mwezi Julai, 2019 na utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka yetu pamoja na kuongeza udhibiti wa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali. Vilevile, katika mwaka 2019/20 Serikali itaunganisha e-visa, e-permit na e-passport katika ofisi za kibalozi nje ya nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, mfumo huo wa kielektroniki wa huduma za uhamiaji umeanza kuonesha mafanikio sio tu ndani ya nchi bali hata nje ya nchi. Katika kudhihirisha mafaniko hayo, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Pasipoti Mpya ya Tanzania ya Kielektroniki imetunukiwa Tuzo ya kuwa Pasipoti bora katika Ukanda wa Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika, kwa kukidhi viwango vya ubora wa kiusalama vinavyopendekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Usafiri wa Anga. Tuzo hiyo ilitolewa katika sherehe zilizofanyika katika Kisiwa cha Malta tarehe 26 Machi, 2019 na ilikabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji kwa niaba ya Serikali.

 
Hali ya Ulinzi na Usalama Mipakani
 

 1. Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama mipakani imeendelea kuwa shwari kutokana na kuimarisha udhibiti wa watu wanaoingia na kutoka nchini. Kazi hii inafanyika kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi wenye nia njema.

 
Misako, Doria na Ukaguzi
 

 1. Mheshimiwa Spika, misako, doria na ukaguzi umeendelea kufanyika katika sehemu mbalimbali ili kuwabaini wageni wanaoishi nchini kinyume cha sheria. Katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019 jumla ya watuhumiwa wa uhamiaji haramu 9,610 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria. Idadi hii imepungua kwa asilimia 28.2 ya wahamiaji haramu 13,393 waliokamatwa katika kipindi kama hiki mwaka 2017/18.

 

 1. Mheshimiwa Spika, tarehe 03 - 04 Aprili, 2019 Jijini Dar es Salaam ulifanyika mkutano wa kimataifa uliozikutanisha nchi tatu za Tanzania, Kenya na Ethiopia pamoja na Washirika wa Maendeleo. Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo uliokuwa na lengo la kutafuta mbinu mbalimbali za kukabiliana na wahamiaji haramu wanaoingia nchini. Kufuatia mkutano huo nilitoa agizo kwa Idara ya Uhamiaji kuhakikisha kwamba inawasaka madalali wa wahamiaji haramu ili waweze kukamatwa na kufunguliwa mashitaka. Majina ya madalali hao yameanza kupokelewa na yanafanyiwa kazi na Wizara.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Serikali itaendelea kusimamia Sheria na Kanuni za Uhamiaji ili kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu katika maeneo ya mipaka na vituo vya kuingilia nchini. Aidha, misako, doria na kaguzi zitaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwabaini na kuwadhibiti wahamiaji haramu pamoja na madalali, wasafirishaji, wanaowahifadhi na wote wanaoshiriki kwa namna moja au nyingine katika uhalifu huo.

 
 
 
VITA DHIDI YA BIASHARA HARAMU YA USAFIRISHAJI WA BINADAMU
 

 1.  Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Sekretarieti ya Kupambana na Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu imeokoa jumla ya wahanga 31 na kuwapatia misaada. Baadhi ya wahanga hao wameunganishwa na familia zao na wengine taratibu za kuwaunganisha na familia zao zinaendelea.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Wizara itakamilisha marekebisho ya Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu ya Mwaka 2008. Moja ya maeneo yanayopendekezwa kufanyiwa marekebisho katika sheria husika ni kuongeza wigo wa adhabu kwa wahalifu wa biashara hiyo.

 
Mradi wa Vitambulisho vya Taifa
 

 1.  Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea na zoezi la usajili, ambapo hadi kufikia Machi, 2019 jumla ya watu 19,934,708 walikuwa wamesajiliwa sawa na asilimia 82 ya lengo la kusajili watu 24,295,468. Aidha, Mamlaka imetoa Namba za Utambulisho wa Taifa kwa Wananchi 11,133,095. Mamlaka pia imechapisha vitambulisho 4,850,724 na kugawa kwa wananchi 4,503,769. Hata hivyo, ili kuongeza kasi ya kuchapisha vitambulisho, Mamlaka ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za ununuzi wa mashine mpya mbili (2) zenye uwezo wa kuchapa vitambulisho 9,000 ikilinganishwa na vitambulisho 750 kwa saa vinavyochapishwa na mashine zilizopo sasa.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia NIDA imeanzisha utaratibu wa kuvipeleka Vitambulisho vya Taifa katika ofisi za Watendaji wa Kata kwa ajili ya kuongeza kasi ya ugawaji wa vitambulisho kwa wananchi. Pia, Mamlaka inashirikiana na taasisi nyingine kutumia Namba za Utambulisho wa Taifa katika kutoa huduma.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa NIDA imeanzisha utaratibu unaowezesha wananchi kupata nakala ya Kitambulisho cha Taifa kupitia Tovuti ya Mamlaka hiyo (www.nida.go.tz). Sambamba na utaratibu huo, wananchi wanaweza kupata Namba ya Utambulisho wa Taifa kupitia simu zao za viganjani kwa kupiga namba *152*00# halafu kuchagua namba 3 na kufuata maelekezo. Kupitia namba hiyo ya Utambulisho wa Taifa wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali zikiwemo: usajili wa kampuni ya biashara; usajili wa laini za simu; huduma za fedha zitolewazo na benki; ulipaji wa kodi za Serikali; kupata mikopo ya elimu ya juu; na kupata pasipoti.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Wizara kupitia Mamlaka hiyo itaendelea na zoezi la usajili ili kufikia wananchi 25,237,954. Pia, NIDA itakamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa ofisi 25 za usajili za wilaya, Ofisi ya Makao Makuu ya Mamlaka Jijini Dodoma pamoja na mifumo ya TEHAMA. Kati ya ofisi hizo 22 zitajengwa Tanzania Bara na tatu (3) zitajengwa Zanzibar (Wilaya ya Micheweni - Kaskazini Pemba, Wilaya ya Mkoani - Kusini Pemba na Wilaya ya Magharibi - Mjini Magharibi). Kazi hizo zitatekelezwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea ambapo Shilingi 9,645,489,600 zimetengwa katika mwaka 2019/20.

 
HUDUMA KWA WAKIMBIZI
 

 1.  Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeendelea kupokea na kuhifadhi wakimbizi na waomba hifadhi kutoka nchi mbalimbali. Hadi kufikia mwezi Machi, 2019 Tanzania ilikuwa inawahudumia waomba hifadhi na wakimbizi 321,642. Aidha, katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019 jumla ya wakimbizi 28,662 kutoka Burundi walirejeshwa nchini mwao kwa hiari yao. Idadi hiyo inafanya wakimbizi waliorejeshwa nchini mwao tangu zoezi hilo lilivyoanza mwaka 2017 kufikia 63,167 kati ya 83,676 waliojiandikisha sawa na asilimia 73.3.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea na zoezi la kuwahamishia katika nchi ya tatu wakimbizi waliopo nchini. Hadi kufikia Machi, 2019 jumla ya wakimbizi 2,583 walihamishiwa katika nchi za Marekani, Canada, Australia na Uholanzi. Serikali inatekeleza majukumu hayo kwa kushirikiana na Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNHCR na IOM.

 
Masoko ya Pamoja kati ya Wananchi na Wakimbizi

 1.  Mheshimiwa Spika, Wizara imetekeleza agizo la Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuyahamishia ndani ya makambi masoko ya pamoja. Katika kutekeleza agizo hilo Wizara imehamishia masoko mawili ndani ya Kambi za Nduta na Mtendeli  yanayotumiwa na wananchi pamoja  na Wakimbizi ili kuimarisha usalama na kudhibiti utoro wa wakimbizi.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Wizara itaendelea kuwahifadhi wakimbizi waliopewa hadhi hiyo kwa mujibu wa Sheria za nchi yetu, kuwatafutia suluhisho la kudumu ikiwa ni pamoja na kuwarejesha katika nchi zao za asili kwa hiari na kuwahamishia nchi ya tatu. Aidha, Wizara itaendelea kuimarisha udhibiti na kudumisha hali ya usalama katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuhifadhi wakimbizi.

 
 
USAJILI NA USIMAMIZI WA JUMUIYA ZA KIJAMII

 1.  Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019 jumla ya maombi ya usajili ya jumuiya 150 yamepokelewa, ambapo 77 ni ya Jumuiya za Kidini na 73 ni Jumuiya za Kijamii. Kutokana na maombi hayo, jumla ya Jumuiya 69 zilisajiliwa, kati ya hizo 38 ni za Kijamii na 31 ni za Kidini. Maombi ya Jumuiya 81 yanaendelea kushughulikiwa.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, sambasamba na shughuli za usajili, Wizara imekamilisha mfumo mpya wa usajili wa Jumuiya za Kijamii ujulikanao kama Societies Management System. Mfumo huo utawezesha shughuli za usajili kufanyika kwa ufanisi zaidi ikiwa ni pamoja na kuboresha ukusanyaji wa mapato.

 

 1. SHUKURANI

 

 1.  Mheshimiwa Spika, natoa shukurani kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni, Mbunge wa Kikwajuni - Zanzibar kwa msaada wake anaonipa katika kusimamia majukumu ya Wizara. Vilevile, nawashukuru kwa dhati Katibu Mkuu Meja Jenerali Jacob G. Kingu na Naibu Katibu Mkuu Ramadhan K. Kailima kwa uongozi wao madhubuti katika kusimamia utekelezaji wa kazi na majukumu ya Wizara.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, pia natoa shukurani zangu za dhati kwa Wakuu wa Vyombo vya Usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Vilevile, nawashukuru Makamishna; Makamishna Wasaidizi; Wakuu wa Idara na Vitengo; Askari na watumishi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuendelea kutekeleza shughuli za Wizara kwa weledi na ufanisi.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa shukurani kwa nchi wahisani zikiwemo Austria, Belgium, Egypt, Jamhuri ya Watu wa China, India, Japan, Korea Kusini, Morocco, Urusi, Ujerumani pamoja na Taasisi na Mashirika ya Kimataifa ya ASA, EU, RESA, IOM, UNDP, UNHCR, UN-Women, UNICEF, WFP, Vyombo vya Habari, Jumuiya za Kijamii na wananchi kwa ujumla. Wadau wote hawa wamekuwa nguzo muhimu katika kutoa misaada ikiwemo ya ujenzi wa ofisi, vituo vya Polisi na makazi ya Askari, vitendea kazi pamoja na kutoa taarifa mbalimbali ambazo zinasaidia kubaini na kuzuia uhalifu.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, kipekee naishukuru familia yangu, ndugu, marafiki na wananchi, hususan wa Jimbo langu la Mwibara kwa ushirikiano wao katika kuchangia maendeleo ya jimbo letu.

 

 1. HITIMISHO

 

 1.  Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kulinda amani na usalama kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola nchini pamoja na wadau mbalimbali. Kuwepo kwa utulivu nchini kutaendelea kuwezesha utekelezaji wa shughuli za maendeleo na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, Wizara imepanga kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Shilingi 297,014,614,300 mwaka 2018/19 hadi Shilingi 471,893,927,000 mwaka 2019/20 sawa na ongezeko la asilimia 58.8. Ili kufikia lengo hilo Wizara itatumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kuimarisha matumizi ya mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato ya Serikali (GePG); kuendelea kuhuisha viwango vya tozo na ada mbalimbali ili viendane na wakati; kuendelea kufanya ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto katika maeneo mbalimbali nchini; na kuimarisha huduma za uhamiaji mtandao.

 

 1.  Mheshimiwa Spika, naomba sasa Bunge lako Tukufu liidhinishe Bajeti ya jumla ya Shilingi 921,247,033,279 kwa ajili ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2019/20. Kati ya fedha hizo, Shilingi 889,308,619,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, ambapo Shilingi 372,268,278,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 517,040,341,000 ni Mishahara. Fedha za Miradi ya Maendeleo ni Shilingi 31,938,414,279 kati ya fedha hizo Shilingi 21,500,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 10,438,414,279 ni fedha za nje.

 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja.
Back to Top