HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. GEORGE BONIFACE SIMBACHAWENE (Mb.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2020/21

Thursday, April 23, 2020
 1. UTANGULIZI

 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka 2019/20 na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka 2020/21.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwasilisha Hotuba hii muhimu mbele ya Bunge lako Tukufu. Aidha, kwa namna ya kipekee namshukuru Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuanzia tarehe 23 Januari, 2020.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa dhati nampongeza Mhe. Rais kwa namna anavyoiongoza Serikali ya Awamu ya Tano inayosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM, ambapo mafanikio mengi yamepatikana katika sekta mbalimbali. Ni wazi kuwa mafanikio hayo yamepatikana kwa kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu nchini kupitia utendaji mzuri wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba nitoe Rai kwa wananchi na Waheshimiwa Wabunge wote bila kujali itikadi za aina yoyote, tuendelee kuyaenzi mafanikio haya makubwa na kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ninaishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Salum  Mwinyi Rehani (Mb.) na wajumbe wake wote kwa  kazi  nzuri  wanayoifanya ya kutoa ushauri wa kuboresha mambo mbalimbali katika Wizara ikiwemo kupitia na kuchambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2020/21.

 

 1. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, ninaomba kuwasilisha maelezo ya Mapitio ya Utekelezaji wa Majukumu na Kazi za Wizara katika Mwaka 2019/20 na Malengo ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2020/21.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Wizara iliidhinishiwa bajeti ya jumla ya Shilingi bilioni 921.24, kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 517.04 ni kwa ajili ya Mishahara, Shilingi bilioni 372.26 ni za Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni 31.93 ni fedha za Miradi ya Maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi, 2020 fedha zilizopokelewa na Wizara ni jumla ya Shilingi bilioni 731.55. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 7.91 zilikuwa ni za Miradi ya Maendeleo, Shilingi bilioni 373.61 ni Mishahara na Shilingi bilioni 350.74 zilikuwa ni za Matumizi Mengineyo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ukusanyaji mapato, hadi kufikia mwezi Machi, 2020 Wizara ilikuwa imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 248.40 ikilinganishwa na lengo la kukusanya Shilingi bilioni 471.89, sawa na asilimia 53. Miongoni mwa sababu ya kushuka kwa mapato ni upungufu wa vitendea kazi, kwa ajili ya ufuatiliaji wa mapato yanayotokana na shughuli za uhamiaji, ambazo zinachangia asilimia 70 ya mapato yote ya Wizara. Ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato hayo, Serikali katika mwaka 2021/21 imetenga Shilingi bilioni 1.17 kupitia Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya kununua magari sita (6) na pikipiki 20.
 2. Mheshimiwa  Spika,  katika  kutekeleza majukumu na kazi zilizopangwa mwaka 2019/20, Wizara imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo: kusajiliwa na kutambuliwa kwa watu 2,478,448 na hivyo kufanya jumla ya watu wote waliosajiliwa katika mfumo wa NIDA kufikia asilimia 86 ya lengo la usajili wa watu 25,237,954; kuwarejesha kwa hiari yao Wakimbizi 9,875 wa Burundi; kupunguza msongamano magerezani kwa kuwezesha wafungwa 2,973 kutumikia vifungo vyao nje ya magereza; kuokoa na kuwapa misaada wahanga 196 wa usafirishaji haramu wa binadamu; na kutolewa kwa pasipoti na hati nyingine za safari 395,903.

 

 1. Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni kukamilika kwa nyumba 431 za makazi ya Jeshi la Polisi katika mikoa mbalimbali; kukamilika kwa majengo 12 ya ghorofa katika Gereza Ukonga yenye uwezo wa kuchukua familia 172 za Askari Magereza; kukamilika kwa Ofisi ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dodoma. Wizara pia imefanikiwa kuwapandisha vyeo Maafisa, Wakaguzi na Askari 2,406 wa Jeshi la Polisi, 3,702 wa Jeshi la Magereza, 169 wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na 815 wa Idara ya Uhamiaji.

 
Maeneo ya Kipaumbele kwa Mwaka 2020/21
 

 1. Mheshimiwa Spika, maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2020/21 ni pamoja na: kudumisha usalama wa raia na mali zao; kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu; kutoa mafunzo kwa Maafisa, Askari na Watumishi Raia na kuwapandisha vyeo; kununua vitendea kazi muhimu, hususan magari na pikipiki; kuendelea na ujenzi wa makazi ya Askari na ofisi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ni: kuendelea na usajili na utambuzi kwa lengo la kufikia idadi ya wananchi 27,796,983; kuandaa Sera na kufanya marekebisho ya baadhi ya Sheria zinazohusu Wizara; kupunguza msongamano magerezani; kutekeleza Mkakati wa Kujitosheleza kwa Chakula wa Jeshi la Magereza; na kusimamia utekelezaji wa shughuli za mashirika ya uzalishaji mali ya Jeshi la Polisi na Magereza ili yatimize malengo ya uanzishwaji wake.

 
JESHI LA POLISI
 

 1. Mheshimiwa Spika,   Jeshi la Polisi hushirikiana na jamii na wadau wengine ili kuhakikisha uhalifu wa aina zote unadhibitiwa. Ushirikiano huu umewezesha nchi yetu kuendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, uhalifu wa makosa makubwa ya jinai yanayojumuisha makosa dhidi ya binadamu, maadili ya jamii na kuwania mali umepungua na kufikia makosa 44,277 katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 ikilinganishwa na makosa 45,574 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19, sawa na asilimia 2.8. Jumla ya  kesi 12,736 upelelezi  wake ulikamilika na watuhumiwa walifikishwa mahakamani, ambapo kesi 2,783  zilishinda, kesi 478 zilishindwa, kesi 113 ziliondolewa, kesi 9,362 bado zipo mahakamani. Aidha, kesi 2,476 hazikufikishwa mahakamani zilifungwa katika Vituo vya Polisi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kesi zinapelelezwa kwa haraka, Jeshi la Polisi katika mwaka 2020/21 litaongeza idadi ya wapelelezi, kuwapa mafunzo wapelezi hao na kuongeza vitendea kazi vya kisasa vikiwemo vya Maabara zote za Uchunguzi wa Kisayansi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti uhalifu wa matumizi ya silaha, Jeshi la Polisi limefanya operesheni na kukamata silaha za aina mbalimbali 211 na risasi 531. Kupitia operesheni hizo, jumla ya watuhumiwa 156 walikamatwa na kufikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea. Vilevile, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo Vingine vya Dola lilifanikiwa kukamata nyara za Serikali 1,963 zenye thamani ya Shilingi bilioni 3.97. Watuhumiwa 997 walifikishwa mahakamani na kesi zao zipo kwenye hatua mbalimbali.

Hali ya Usalama Barabarani
 

 1. Mheshimiwa Spika, hali ya usalama barabarani imeendelea kuimarika kutokana na mikakati iliyowekwa na Jeshi la Polisi, ambayo imesaidia kupunguza matukio ya ajali, vifo na majeruhi. Katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 matukio makubwa ya ajali za barabarani yamepungua kwa asilimia 26 na ajali zilizosababisha vifo zimepungua kwa asilimia 10. Aidha, hatua kali zimechukuliwa kwa madereva waliokamatwa kwa makosa hatarishi, ambapo madereva 189 walifungiwa leseni na wengine kupelekwa mahakamani. Katika mwaka 2020/21 Wizara kupitia Jeshi la Polisi litaendelea kudhibiti ajali za barabarani kwa kushirikiana na wadau. Pia, elimu itaendelea kutolewa kwa umma juu ya matumizi sahihi ya barabara na utii wa sheria bila shuruti ili kuhakikisha barabara na watumiaji wanakuwa salama muda wote.

 
Kuboresha Makazi, Ofisi na Vituo vya Polisi
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Askari wanaishi katika mazingira bora, Serikali imekamilisha mradi wa ujenzi wa nyumba 400. Nyumba hizo zimejengwa katika mikoa mbalimbali na zilizinduliwa rasmi na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika Mkoa wa Geita tarehe 15 Julai, 2019 na Dodoma tarehe 22 Novemba, 2019. Aidha, katika kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais, wadau walijitokeza kuchangia ujenzi wa nyumba nyingine 31 katika mikoa ya Lindi, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Simiyu, Shinyanga na Songwe. Vilevile, Jeshi la Polisi kwa kutumia Mfuko wa Tuzo na Tozo limekamilisha ujenzi wa nyumba 31 za Askari na Ofisi ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Dodoma. Pia, ukarabati wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam umekamilika kwa kutumia fedha Shilingi milioni 700 zilizotolewa na Mhe. Rais.
 2.  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar Jeshi la Polisi limeshirikiana na wadau katika ujenzi wa nyumba nne (4) za Askari Kaskazini Pemba na nyumba mbili (2) Kusini Pemba, ambazo zimeezekwa na kazi za umaliziaji zinaendelea. Aidha, Kituo cha Polisi Nungwi Daraja “C” kilichopo Kaskazini Unguja kimejengwa upya. Ni matarajio ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuwa wadau wataendelea kusaidia ujenzi wa nyumba za kuishi Askari, Vituo vya Polisi na ofisi ili kupambana na uhalifu kikamilifu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21 Jeshi la Polisi limepanga kujenga Kituo cha Polisi Mkokotoni (Kaskazini Unguja) kitakachogharimu Shilingi milioni 500, ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari Buyekera unaokadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 1.40, kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbalizi kwa gharama ya Shilingi milioni 50 na kukamilisha ujenzi wa nyumba nne (4) za kuishi familia nane (8) za Askari wilayani Meatu kwa gharama ya Shilingi milioni 50. Aidha, Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wadau katika ujenzi wa nyumba nane (8) Kaskazini Pemba na 12 Kusini Pemba.

 
Usimamizi wa Nidhamu katika Jeshi la Polisi
 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linaendelea kuwatambua watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa nidhamu na ufanisi. Katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 jumla ya Askari 84 walipewa tuzo na zawadi kwa utendaji mzuri. Aidha, jumla ya watumishi 410 wamechukuliwa hatua za kinidhamu. Kati ya hao, Maafisa, Wakaguzi na Askari wamechukulia hatua na Mamlaka zao za kinidhamu, ambapo 78 wamefukuzwa kazi na 332 wamepewa barua ya onyo, barua ya tahadhari na kukatwa mshahara.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21 Wizara itaendelea kusimamia maadili na kuchukua hatua za kinidhamu kwa Askari watakaokwenda kinyume na mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi. Aidha, Askari watakaofanya kazi kwa ubora na uadilifu wataendelea kutambuliwa na kupongezwa kwa namna mbalimbali.

 
Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi
 

 1. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Agosti, 2019 Shirika lilianza kutoa mafunzo ya umahiri wa utunzaji na matumizi ya silaha za moto za kiraia kwa Kampuni Binafsi za Ulinzi Jijini la Dar es Salaam. Hadi kufikia mwezi Machi, 2020 jumla ya Askari 972 wa Kampuni hizo walipata mafunzo hayo. Vilevile, Shirika linakamilisha taratibu za kutoa mafunzo nchi nzima kwa kuandaa miundombinu wezeshi pamoja na kukamilisha mfumo wa TEHAMA utakaotumika kuratibu mafunzo husika. Hivyo, nichukue fursa hii kuwataka Wamiliki na Watumiaji wote wa silaha za moto za kiraia nchini kuwasiliana na Makamanda wa Polisi wa Mikoa ili kupata utaratibu wa kujisajili na kuhudhuria mafunzo katika maeneo yao.

 

 1. Mheshimiwa Spika, mafunzo haya hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Silaha za Moto ya mwaka 2015. Aidha, wamiliki na watumiaji wa silaha za moto za kiraia wasiozingatia sheria husika, hawataruhusiwa kuhuisha vibali vya umiliki na leseni za biashara zinazohusisha matumizi ya silaha hizo. Nitumie fursa hii pia kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kuwa kuanzia mwaka 2020/21 Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaanza kufanya ukaguzi wa vyeti vya umahiri kwa wamiliki wote wa silaha za moto za kiraia nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21 Shirika litajihusisha na kutoa ulinzi katika shughuli za usafirishaji wa fedha na vitu vingine vya thamani kwa Taasisi za Fedha na Kampuni za Madini. Utekelezaji wa shughuli hizi ni katika kuimarisha usalama na ulinzi katika eneo hili la kiuchumi.

 
JESHI LA MAGEREZA
 

 1. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi, 2020 kulikuwa na jumla ya wafungwa na mahabusu 32,438 katika magereza yote nchini. Kati ya hao, wafungwa ni 14,464 na mahabusu 17,974 ambapo ni asilimia 9 zaidi ya uwezo uliopo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu 29,902. Jeshi la Magereza limeendelea kupunguza msongamano wa wafungwa kwa kutumia utaratibu wa Parole, ambapo wafungwa 92 waliachiwa huru. Pia, wafungwa 695 walitolewa magerezani ili kutumikia kifungo cha nje kwa utaratibu wa Extra Mural Labour. Aidha, wafungwa 5,533 waliachiwa huru kwa Msamaha wa Mhe. Rais na hivyo kufanya jumla ya wafungwa wote walioachiliwa huru hadi mwezi Machi, 2020 kufikia wafungwa 6,320.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Programu ya Adhabu Mbadala ya Kifungo cha Gerezani husaidia kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani na kuzipatia Taasisi za Serikali nguvu-kazi ya wafungwa badala ya kuajiri vibarua. Programu hii inasimamiwa na Wizara kupitia Idara ya Huduma za Uangalizi. Katika kipindi cha mwezi Julai, 2019 hadi Machi, 2020 jumla ya wafungwa 2,186 walinufaika na programu ya adhabu mbadala ya kifungo cha gerezani.

 
Kuboresha Makazi, Ofisi na Mabweni ya Wafungwa
 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa majengo 12 ya ghorofa katika Gereza Ukonga yenye uwezo wa kuchukua familia 172 za Askari Magereza na yameanza kutumika. Nyumba   hizo   zilizinduliwa   rasmi   tarehe 23 Januari, 2020 na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kwa dhati nimshukuru Mhe. Rais kwa juhudi kubwa alizozitumia katika kuhakikisha kuwa nyumba hizo zinakamilika na kuanza kutumika.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, Jeshi la Magereza linaendelea na ujenzi wa nyumba 482 katika magereza yote nchini na upo katika hatua mbalimbali. Aidha, bweni moja (1) la Gereza Kwitanga na mabweni manne (4) ya Gereza Segerea yamekamilika. Hivyo, kuongeza jumla ya nafasi 246 za kuhifadhi wafungwa. Pia, kwa kushirikiana na wadau, ujenzi wa mabweni 10 yenye uwezo wa kuhifadhi wafungwa 865 unaendelea katika magereza ya Kwitanga moja (1), Geita matatu (3), Sumbawanga matatu (3), Chunya moja (1), Kyela moja (1) na Kambi Mkwajuni mkoani Songwe moja (1).

 
Ujenzi wa Kiwanda cha Samani Msalato
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza sera ya uchumi wa viwanda, Serikali katika mwaka 2019/20 imetoa Shilingi milioni 820.41 kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha Samani Msalato Jijini Dodoma. Kiwanda hicho kitakapokamilika mwezi Julai, 2020 kitatengeneza samani kwa matumizi mbalimbali. Aidha, katika mwaka 2020/21 Jeshi la Magereza litaanza ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dodoma, ambapo jumla ya Shilingi bilioni 13.5 zimetengwa.

 
Mkakati  wa  Kujitosheleza kwa Chakula
 

 1. Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Kujitosheleza kwa Chakula unaendelea kutekelezwa ambapo katika mwaka 2019/20 jumla ya ekari 5,608 zimelimwa. Kati ya hizo, ekari 4,200 ni za mahindi, ekari 975 za mpunga na ekari 433 ni za maharage. Matarajio ni kuvuna mahindi tani 5,670, mpunga tani 1,463 na maharage tani 217. Kupitia Mkakati huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2018 umewezesha Magereza ya Arusha, Kitai, Kitengule na Songwe kujitosheleza kwa mazao ya mahindi na maharage kwa asilimia 100. Magereza hayo yameweza kuzalisha ziada na kulisha kwa mwaka mzima magereza mengine 43 yaliyopo katika Mikoa ya Geita manne (4), Kagera nane (8), Katavi mawili (2), Lindi matano (5), Mbeya matano (5), Mtwara matano (5), Rukwa matatu (3), Ruvuma sita (6), Shinyanga mawili (2) na Songwe matatu (3).

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, Gereza Arusha limelisha kwa miezi sita (6) jumla ya magereza 14 yaliyopo Mikoa ya Arusha mawili (2), Kilimanjaro manne (4) na Tanga nane (8). Magereza ya Isupilo (Iringa) na Ludewa (Njombe) yamezalisha mahindi na kujitosheleza kwa asilimia 100 na kulisha magereza mengine matano (5) yaliyopo ndani ya mikoa hiyo. Aidha, Magereza ya Idete na Kiberege yaliyopo mkoani Morogoro yameweza kujitosheleza kwa zao la mpunga kwa asilimia 100 kwa mwaka mzima.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21 Wizara kupitia Jeshi la Magereza itaendelea kusimamia utekelezaji wa mkakati huo ili kuhakikisha lengo la kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa na mahabusu katika magereza yote linafikiwa. Aidha, matrekta mapya 26 yalinunuliwa na mawili (2) yalitolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Matrekta hayo yatasaidia kuongeza uwezo wa kulima katika magereza mbalimbali. Katika msimu wa mwaka 2020/21 Jeshi la Magereza litalima ekari 9,000, kati ya hizo mahindi ni ekari 5,750, mpunga ekari 2,000 na maharage ekari 1,250. Matarajio ni kuvuna wastani wa tani 7,785 za mahindi, tani 3,000 za mpunga na tani 625 za maharage.

 
Shirika la Magereza
 

 1. Mheshimiwa Spika, Shirika la Magereza lipo katika hatua za mwisho za ujenzi wa viwanda vitatu (3) vya Kampuni ya Kutengeneza Bidhaa za Ngozi. Viwanda hivyo vinajengwa katika eneo la Gereza Karanga Mjini Moshi kwa gharama ya Shilingi bilioni 9.63. Ujenzi huo umepangwa kukamilika kabla ya mwezi Juni, 2020. Aidha, Shirika limepata zabuni ya ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Ngozi ambacho ni sehemu ya viwanda vya Kampuni hiyo. Gharama za ujenzi zinakadiriwa kufikia Shilingi bilioni 18.18. Ujenzi utaanza mwezi Aprili, 2020 na utakamilika baada ya miezi nane (8).

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, Shirika limepata kandarasi ya kujenga majengo ya Kiwanda cha Sukari cha Kampuni Hodhi ya Mkulazi. Ujenzi huo unaendelea katika eneo la Gereza Mbigiri, ambapo ujenzi wa zahanati umefikia hatua ya kuezeka; majengo ya utawala na nyumba za makazi yapo katika hatua ya kujenga ukuta. Zabuni hiyo ina thamani ya Shilingi bilioni 2.34 na ujenzi utakamilika mwezi Juni, 2020.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Shirika pia limepokea jumla ya Shilingi bilioni 1.54 kutoka Taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia na watu binafsi kwa ajili ya kutengeneza samani. Samani hizo zimetengenezwa katika viwanda vilivyopo katika Magereza ya Arusha, Ukonga na Uyui na kukabidhiwa kwa wahusika. Katika mwaka 2020/21 Shirika litaendelea kutengeneza samani zenye ubora wa hali ya juu kwa ajili ya wadau.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Shirika limefanikiwa kuingiza miradi yake yote kwenye Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Mapato ya Serikali (GePG). Aidha, Shirika limeanzisha Mfumo wa Kielektroniki wa Kihasibu unaojulikana kwa jina la “Prisons Corporation Sole        Accounting System”. Mfumo huo unawezesha upatikanaji wa taarifa za mapato kutoka katika miradi yote ya Shirika. Natoa rai kwa wateja wanaopata huduma katika Miradi ya Shirika la Magereza kuhakikisha wanapewa stakabadhi za malipo za kielektroniki kwa kutumia mfumo huo.

 
 
 
 
JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI
 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 limefanya ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto katika maeneo 53,919 na magari 13,128. Kupitia ukaguzi huo, Shilingi bilioni 5.89 zilikusanywa kutokana na tozo za majengo na magari. Katika kukabiliana na majanga, Jeshi limeshiriki kuzima moto na kufanya uokoaji katika matukio 2,204 ambayo kama yasingedhibitiwa yangeweza kuleta madhara makubwa kwa jamii.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linakamilisha taratibu za ununuzi wa magari matano (5) ya kuzima moto pamoja na vifaa vya uokoaji kupitia bajeti ya mwaka 2019/20. Magari hayo yenye uwezo wa kubeba lita 5,000 za maji kila moja yatanunuliwa kutoka Shirika la Nyumbu Kibaha.  Katika  mwaka  2020/21 Wizara kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji imepanga kununua magari matatu (3) ya kuzima  moto  kwa  gharama  ya  Shilingi bilioni 2.25.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dodoma umekamilika. Aidha, ujenzi wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Chato mkoani Geita upo katika hatua za ukamilishaji. Katika mwaka 2020/21 Jeshi limetenga Shilingi bilioni 1.25 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Zimamoto na Uokoaji wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

 
IDARA YA UHAMIAJI
 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Idara ya Uhamiaji inaendelea kutoa huduma za pasipoti, viza na vibali vya ukaazi kupitia mfumo wa kielektroniki. Aidha, Mfumo wa Udhibiti wa Mipaka wa Kielektroniki umeanza kutumika kwenye Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vilivyopo Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar pamoja na Vituo vyote vya Mipakani vya Utoaji Huduma kwa Pamoja. Mfumo huu unasaidia kuimarisha usalama wa mipaka ya nchi yetu pamoja na kuongeza udhibiti kwenye ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

 

 1. Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Januari, 2020 Serikali iliziondoa rasmi pasipoti za zamani kwenye matumizi ili kuhakikisha kila Mtanzania anayehitaji kusafiri nje ya nchi anatumia pasipoti ya kieletroniki. Hadi kufikia mwezi Machi, 2020 jumla ya pasipoti 213,035 zilitolewa, kati ya hizo, pasipoti 15,598 zilitolewa kupitia ofisi za Balozi zetu nje ya nchi. Idadi ya pasipoti zote zilizotolewa imeongezeka kwa asilimia 189 ikilinganishwa na jumla ya pasipoti 73,416 zilizotolewa katika kipindi kama hiki mwaka 2018/19. Katika mwaka 2020/21 Wizara itaendelea kutumia mifumo ya kielektroniki kutoa huduma zake zote za uhamiaji.  Mifumo hiyo imeunganishwa na Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Mapato ya Serikali na itasaidia kudhibiti ukusanyaji wa mapato yatokanayo na huduma hizo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji imeendelea kuwawezesha wageni kuingia na kutoka nchini. Hadi kufikia mwezi Machi, 2020 wageni 1,158,022 waliingia nchini na Wageni 1,048,149 walitoka nchini. Aidha, jumla ya wageni 361 walizuiliwa kuingia nchini kutokana na sababu za kiusalama na kutokidhi vigezo vya uhamiaji.

 
Ujenzi wa Ofisi za Uhamiaji
 

 1. Mheshimiwa Spika,   katika mwaka 2020/21 Idara ya Uhamiaji itaendelea na ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu Jijini Dodoma na kukamilisha ujenzi wa ofisi katika Mikoa ya Geita, Lindi, Manyara na Mtwara. Vilevile, ujenzi wa Ofisi za Uhamiaji utaanza katika Wilaya za Chato, Kyerwa, Mlele, Mufindi, Simanjiro na Rorya.

 
VITA DHIDI YA BIASHARA HARAMU YA USAFIRISHAJI WA BINADAMU
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 Wizara imefanikiwa kuokoa na kuwasaidia Wahanga 196 waliokuwa wakitumikishwa katika maeneo mbalimbali. Kati ya hao, Wahanga 180 walikuwa wakitumikishwa ndani ya nchi na 16 nje ya nchi. Vilevile, watu na Kampuni zinazojihusisha na mtandao wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu zimeendelea kudhibitiwa, ambapo Wizara iliwasilisha ushauri katika mamlaka husika na Kampuni tisa (9) zilifutiwa leseni. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama iliwakamata jumla ya watu 102 wanaojihusisha na biashara hiyo na kuwafikisha kwenye Vyombo vya Sheria. Katika mwaka 2020/21 Wizara itaendelea na Mapambano Dhidi ya Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu kwa kufanya operesheni kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya mipaka ya nchi na njia zinazotumiwa na wahalifu wa biashara hiyo.

 
MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA)
 

 1. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi, 2020 NIDA imefanikiwa kusajili jumla ya wananchi 2,478,448. Hivyo, kufanya wananchi waliosajiliwa kufikia 21,823,026 kati ya lengo la kusajili watu 25,237,954 ifikapo mwezi Juni, 2020. Aidha, NIDA imetoa Namba za Utambulisho wa Taifa 17,871,770 na imechapisha pamoja na kugawa kwa wananchi Vitambulisho vya Taifa 6,103,225. Vilevile, mashine mbili (2) zenye uwezo wa kuchapisha vitambulisho 144,000 kwa siku zimenunuliwa na tayari zimefungwa. Mashine hizo zitasaidia kufikia lengo la Serikali la kuwapatia wananchi Vitambulisho vya Taifa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, NIDA imesajili Wageni Wakaazi 26,794 na Wakimbizi 207,644 katika Kambi za Mtendeli, Nduta, Nyarugusu na Makazi ya Katumba, Mishamo, Ulyankulu pamoja na wakimbizi wenye vibali vya kuishi waliopo Jijini Dar es Salaam.  Pia, wafungwa 380 walisajiliwa katika Magereza ya Bagamoyo na Isanga na usajili huo utaendelea mwaka 2020/21 katika magereza yote nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, kwa kutumia mfumo wa usajili na utambuzi, Kampuni za Simu nchini zimefanikiwa kusajili laini zaidi ya 37,297,930 kwa kutumia alama za vidole. Zoezi hilo limefanikisha utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya kusajili laini za simu kwa kutumia Namba za Utambulisho wa Taifa na Vitambulisho vya Taifa. Usajili huo pia umechangia kuongezeka kwa mapato yanayokusanywa na NIDA kutoka lengo la Shilingi milioni 500 mwaka 2019/20 hadi kufikia makusanyo halisi ya Shilingi bilioni 1.38 mwezi Machi, 2020 sawa na asilimia 177. Ninatoa Rai kwa wananchi kuendelea kujisajili na pia nawaomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kuwahamasisha wananchi katika majimbo yao kujisajili na kutumia Namba za Utambulisho wa Taifa katika kupata huduma mbalimbali.

 

 1. Mheshimiwa  Spika,   kupitia  Bunge  hili nawaomba wananchi, hususan waliopo katika mikoa  ya  pembezoni  na  mipaka ya nchi wawe na subira kutokana na kuchelewa kupata Namba za Utambulisho wa Taifa. Hali hii inatokana na kuwepo kwa utaratibu  maalumu  wa  kufanya  upekuzi wa maombi yao kwa sababu ya kuwepo kwa mwingiliano mkubwa wa watu kutoka nchi jirani. Upekuzi huo unafanyika kwa nia njema ili vitambulisho vyetu visitolewe kwa watu wasiostahili.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Wizara kupitia NIDA itaendelea na zoezi la usajili na utambuzi wa watu, ambapo jumla ya watu 6,076,666 wanatarajiwa kusajiliwa. Lengo ni kufikia idadi ya wananchi 27,796,983 watakaofikia umri wa miaka 18 mwezi Juni, 2021.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi taasisi 69 za umma na binafsi zimeuunganishwa na mfumo wa usajili na utambuzi wa watu. Katika mwaka 2020/21 mifumo ya taasisi 39 za umma na binafsi itaunganishwa na mfumo wa Vitambulisho vya Taifa. Aidha, NIDA itaanza kutoza tozo kwa taasisi za umma na binafsi zinazotumia taarifa kutoka kwenye  mfumo  wa  usajili  na  utambuzi kwa kuzingatia mikataba kati ya taasisi hizo na NIDA. Fedha zilizotengwa kwa mwaka 2020/21 kwa ajili ya kazi za NIDA ni jumla ya Shilingi bilioni 10.86. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 10 ni fedha za ndani na Shilingi milioni 861.81 ni fedha za nje.

 
HUDUMA KWA WAKIMBIZI
 

 1. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi, 2020 Tanzania ilikuwa inahifadhi waomba hifadhi na wakimbizi 293,710. Kati ya hao, Warundi walikuwa 216,900, Wakongo 76,384 na 426 kutoka nchi nyingine. Kwa kuwa tatizo la ukimbizi sio la kudumu, Wizara kwa kushirikiana na Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNHCR na IOM imeendelea kuwatafutia suluhisho la kudumu wakimbizi wanaohifadhiwa hapa nchini. Hadi kufikia Machi, 2020 jumla ya wakimbizi 9,875 kutoka Burundi walirejeshwa kwa hiari yao nchini kwao. Idadi hiyo inafanya wakimbizi waliorejeshwa nchini humo tangu kuanza kwa zoezi hilo mwezi Septemba, 2017 kufikia 82,299. Aidha, jumla ya wakimbizi 1,901 walihamishiwa katika nchi ya tatu za Australia, Canada, Ireland, Marekani na Uholanzi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge hili, ninaomba kutumia fursa hii, kukanusha shutuma zinazotolewa na makundi mbalimbali kuwa Serikali ya Tanzania inawarejesha wakimbizi nchini kwao kwa lazima. Aidha, ninapenda kuuhakikishia umma wa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuwa, Serikali ya Tanzania katika kutekeleza zoezi la kuwarejesha wakimbizi, imekuwa ikiheshimu uhiari wa wakimbizi katika kuamua kurejea nchi zao au kuendelea kubaki Tanzania ikiwa wanaona bado hawana uhakika wa usalama nchini kwao. Aidha, zoezi hilo linatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana kikamilifu na Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNHCR, IOM na WFP pamoja na wadau wengine wa kimataifa na ndani ya nchi. Ushiriki wa wadau hao ni ushahidi tosha kuwa zoezi husika linafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Haki za Binadamu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Serikali itaendelea kuwahifadhi wakimbizi na kuwatafutia suluhisho la kudumu. Aidha, usalama utaendelea kuimarishwa katika maeneo yote yanayohifadhi Wakimbizi.

Upandishwaji Vyeo na Ajira
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Maafisa, Wakaguzi, Askari na Watumishi Raia walipandishwa vyeo kama ifuatavyo: Jeshi la Polisi 1,821; Jeshi la Magereza 3,702; Jeshi la Zimamoto na Uokoaji 169; na Idara ya Uhamiaji 991. Pia, Serikali imeajiri Askari 400 wa Idara ya Uhamiaji na kuwapangia kazi katika vituo mbalimbali baada ya kuhitimu mafunzo ya awali. Katika mwaka 2020/21 Serikali imepanga kuajiri Askari 2,725 wa Jeshi la Polisi, Askari 685 wa Jeshi la Magereza, Askari 501 wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Askari 495 wa Idara ya Uhamiaji.  Askari hao watapewa mafunzo ya awali ndani ya nchi kabla ya kupangiwa vituo vya kazi.

 
C. SHUKURANI
 

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni (Mb.) kwa ushirikiano anaonipa katika kusimamia majukumu ya Wizara. Aidha, nawashukuru kwa dhati Katibu Mkuu Ndugu Christopher D. Kadio na       Naibu Katibu Mkuu Ndugu Kailima Ramadhan kwa kusimamia vema utekelezaji wa kazi za Wizara. Pia, nawashukuru Wakuu wa Vyombo vya Usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Ni dhahiri kuwa Wakuu wa Vyombo hivi wametoa mchango mkubwa katika kusimamia maeneo yao na kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kuwepo nchini. Vilevile, nawashukuru Wenyeviti wa Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi na Shirika la Magereza na watumishi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuendelea kutekeleza shughuli za Wizara kwa weledi na ufanisi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ninaishukuru familia yangu kwani imekuwa msaada mkubwa katika kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu ya kiofisi. Aidha, nawashukuru wananchi wote wa Jimbo langu la Kibakwe kwa kuendeleza umoja na mshikamano katika kushiriki kwenye maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya jimbo letu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwashukuru Mhe. Rais, Viongozi wote wa Kitaifa, Mhe. Spika, Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wa dini, Watumishi wa Serikali, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi ambao mmeshirikiana na mimi katika kunipa faraja wakati wa Msiba mzito wa Marehemu Baba yangu.

 
D. HITIMISHO
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21 Wizara inatarajia kukusanya mapato ya jumla ya     Shilingi 488,569,880,319. Aidha, mapato yanayokusanywa na NIDA kupitia ada        ya utambulisho yataanza kutolewa taarifa na Msajili wa Hazina badala ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kama ilivyokuwa awali.

 

 1. Mheshimiwa Spika,  naomba sasa Bunge lako  Tukufu  liidhinishe  Bajeti  ya  jumla ya  Shilingi  899,170,293,000  kwa  ajili ya  Wizara  ya  Mambo  ya  Ndani  ya  Nchi kwa mwaka 2020/21. Kati ya fedha hizo, Shilingi 863,734,431,000  ni  kwa  ajili ya Matumizi ya Kawaida, ambapo Shilingi 382,229,678,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 481,504,753,000 ni Mishahara. Fedha za Miradi ya Maendeleo ni Shilingi 35,435,862,000 kati ya fedha hizo Shilingi 34,540,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 895,862,000 ni fedha za nje.

 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja.

 

Back to Top