HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. GEORGE BONIFACE SIMBACHAWENE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2021/2022

Monday, May 3, 2021

HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. GEORGE BONIFACE SIMBACHAWENE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA
MWAKA 2021/2022
UTANGULIZI
 
 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba   kutoa   hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2020/2021 na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka 2021/2022.

 1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia uzima na afya njema pamoja na kuniwezesha kuwasilisha Hotuba yangu katika Bunge hili la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, nchi yetu, ilimpoteza mwana mageuzi, mpendwa wa wananchi wa Tanzania na aliyekuwa mbeba maono mapana ya maendeleo, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyekuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Vyombo vyake vya Usalama imekuwa ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa miradi iliyojengwa na inayoendelea kutekelezwa kutokana na juhudi za Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ikiwemo ujenzi wa ofisi za Makao Makuu ya Vyombo hivyo na ujenzi wa makazi ya Askari. Wizara itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi inayoendelea kama ilivyokusudiwa ikiwa ni kumuenzi Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Mwenyezi Mungu ampumuzishe kwa amani!.  Amina.

 1. Mheshimiwa Spika, tarehe 19 Machi, 2021 Mhe. Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama. Nitumie nafasi hii kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kumpongeza kwa dhati kushika nafasi hii ya juu katika uongozi wa nchi yetu. Ninaomba Mwenyezi Mungu amwangazie baraka na neema zote ili aliongoze Taifa letu kwa amani, utulivu na mafanikio makubwa ya maendeleo. Hotuba za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alizozitoa tangu kushika Madaraka ya Rais zimempambanua na kumuonesha ni namna gani alivyo na Uzalendo, Umahiri, Ubunifu, Uadilifu, Ujasiri na Uwezo Mkubwa wa kuliongoza vema Taifa letu. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inatumia nafasi hii, kuahidi kutekeleza maelekezo na maagizo yake wakati wote.

 1. Mheshimiwa Spika, Pongezi zangu pia ninazitoa kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango kwa kupendekezwa na Mhe. Rais kushika nafasi hiyo. Pongezi nyingine ninazitoa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa ushindi wa kihistoria wa asilimia 76.27 alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba, 2020. Ushindi huo ni wa kihistoria na ameanza kuonesha nia na dhamira ya dhati ya kuibadilisha Zanzibar.

 1. TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2020/2021 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2021/2022

Mapitio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2020/2021
 
 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliidhinishiwa bajeti ya jumla ya Shilingi bilioni 902.63. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 481.50 ni kwa ajili ya Mishahara, Shilingi bilioni 382.84 ni za Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni 38.29 ni za Miradi ya Maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi, 2021 jumla ya Shilingi bilioni 707.16 zilipokelewa na Wizara, sawa na asilimia 78 ya bajeti yote iliyoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mafanikio yaliyopatika katika Mwaka 2020/2021
 
 1. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2020/2021 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imepata mafanikio mbalimbali yakiwemo: kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kiwanda cha Kuzalisha Bidhaa za Ngozi kilichopo Gereza Karanga – Moshi; kukamilika kwa Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza katika eneo la Msalato Jijini Dodoma; kukamilika kwa ujenzi wa nyumba 79 za makazi zenye uwezo wa kukaa familia 152 katika vituo vya magereza nchini; na kukamilika nyumba 19 za kuhudumia familia 38 za askari wa Jeshi la Polisi katika mikoa ya Arusha, Geita na Mwanza.

 1. Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni: kujengwa kwa Kiwanda Kipya cha Ushonaji wa Sare za Askari katika eneo la Kurasini – Dar es Salaam; kutekelezwa kwa asilimia 90 ya ujenzi wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Chamwino – Dodoma; kujengwa kwa kambi ya mafunzo ya Idara ya Uhamiaji iliyopo eneo la Boma Kichakamiba Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga; kuzalishwa na kusambazwa vitambulisho 925,342; kuokolewa kwa wahanga 165 wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu; na kupatikana kwa suluhisho la kudumu kwa wakimbizi, ambapo 1,047 walipelekwa katika mataifa mbalimbali. Mafanikio mengine kwa kirefu yapo katika kitabu changu cha hotuba.

Maeneo ya Kipaumbele kwa Mwaka 2021/2022
 
 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeweka kipaumbele katika kutekeleza maeneo yafuatayo: kuendelea kudumisha amani na usalama nchini; ujenzi wa ofisi na makazi ya askari; usajili na utambuzi wa watu 1,438,735; kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani; kuendelea kutekeleza Mkakati wa Mapinduzi ya Kilimo kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa na mahabusu; kukamilisha ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Ngozi katika eneo la Gereza Karanga – Moshi; kukamilisha uunganishaji wa Mfumo wa Udhibiti wa Mipaka (e-border) katika ofisi za uhamiaji za mikoa na wilaya. Maeneo mengine ya kipaumbele ni kama yalivyotajwa kwenye kitabu changu cha hotuba.

HALI YA USALAMA NCHINI
 
 1. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla nchi yetu imeendelea kuwa katika hali ya amani, utulivu na usalama na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii. Aidha, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo Vingine vya Usalama nchini viliwezesha kufanyika kwa amani na utulivu Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwezi Oktoba, 2020.

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Machi, 2021 jumla ya makosa makubwa ya jinai yanayojumuisha makosa dhidi ya binadamu, maadili ya jamii na kuwania mali yaliyotolewa taarifa katika Vituo vya Polisi nchini yalikuwa 37,230 ikilinganishwa na makosa 44,277 katika kipindi kama hicho mwaka 2019/2020. Hii inaonesha kuwa makosa 7,047 yamepungua sawa na asilimia 15.9. Kupungua kwa makosa hayo kumetokana na ushirikiano mzuri baina ya Jeshi la Polisi na Vyombo Vingine vya Ulinzi na Usalama, wananchi na wadau wengine.

 1. Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia makosa yaliyotolewa taarifa kwenye Vituo vya Polisi, jumla ya kesi 13,842 upelelezi wake ulikamilika na watuhumiwa 8,973 walifikishwa mahakamani, ambapo kesi 2,252 zilishinda na kesi 364 zilishindwa. Katika mwaka 2021/2022, Jeshi la Polisi litahakikisha kesi zinapelelezwa kwa haraka na litaboresha utendaji kwa kuwajengea uwezo wa kiutendaji Maafisa, Wakaguzi na Askari ndani na nje ya nchi.

HALI YA USALAMA BARABARANI
 
 1. Mheshimiwa Spika, hali ya usalama barabarani nchini imezidi kuimarika kutokana na usimamizi mzuri wa Jeshi la Polisi kuhusu Sheria za Usalama Barabarani, ushirikiano na wadau, kuongezeka kwa utii wa sheria bila shuruti kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara. Hivyo, kuwezesha kupungua kwa matukio ya ajali, vifo na majeruhi. Hadi kufikia mwezi Machi, 2021 jumla ya matukio makubwa ya ajali 1,228 yalitolewa taarifa katika Vituo vya Polisi ikilinganishwa na matukio 1,920 katika kipindi kama hicho mwaka 2020 ikiwa ni sawa na kupungua kwa matukio ya ajali kwa asilimia 36.04. Katika mwaka 2021/2022, Jeshi la Polisi litaendelea kutoa elimu kwa umma, kuchukua hatua kali kwa wanaokiuka sheria, kuanzisha kanzidata ya kuwatambua madereva wa bajaji na bodaboda na hivyo kuongeza ufanisi katika usimamizi wa usalama barabarani. Ninatoa wito kwa watumiaji wote wa barabara kuendelea kutii sheria za barabarani ili kuhakikisha usalama wao.

Operesheni za Kupambana na Uhalifu

 1. Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti na kupambana na uhalifu wa aina zote hapa nchini, Jeshi la Polisi limefanya operesheni mbalimbali kwa kushirikiana na taasisi nyingine. Katika operesheni hizo risasi 280 na silaha 134 zilikamatwa. Aidha, jumla ya watuhumiwa 138 walikamatwa na kufikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea. Vilevile, Nyara za Serikali 986 zenye thamani ya Shilingi bilioni 1.37 zilikamatwa na watuhumiwa 441 walifikishwa mahakamani. Jeshi la Polisi katika mwaka 2021/2022 litafanya ukaguzi kwa wamiliki wa silaha ili kujiridhisha kuwa wametekeleza kwa ukamilifu matakwa ya sheria husika pamoja na kudhibiti wizi wa Nyara za Serikali. Aidha, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine linaendelea kudhibiti vitendo vya uhalifu katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji.

Miradi ya Ujenzi wa Makazi, Vituo vya Polisi na Majengo ya Ofisi

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na makazi ya askari, utekelezaji wa miradi ya ukarabati na ujenzi wa nyumba za makazi, Vituo vya Polisi na majengo ya ofisi unaendelea. Ujenzi wa majengo mawili (2) yaliyoko eneo la Mabatini Jijini Mwanza yenye uwezo wa kuhudumia familia 24 za Askari unaendelea, ambapo jengo moja limekamilika na jingine liko katika hatua za umaliziaji. Jumla ya Shilingi milioni 310.78 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani na fedha za wadau limekamilisha ujenzi wa nyumba 13 za kuishi familia 26 za Askari. Kati ya hizo, nyumba nne (4) zimejengwa eneo la Oljoro Jijini Arusha kwa gharama ya Dola za Marekani 100,000 na nyumba tisa (9) Mkoani Geita kwa gharama ya Shilingi milioni 562. Aidha, ujenzi wa nyumba 12 za kuishi familia 22 za Askari unaendelea katika maeneo ya Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Wilayani Rombo – Kilimajaro na Uyui - Tabora.

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 2.97 kwa ajili ya Vituo vya Polisi na majengo ya ofisi. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 1.50 zitatumika kujenga mabweni na hospitali katika Chuo cha Polisi Kurasini – Dar es Salaam, na kiasi kinachobaki cha Shilingi bilioni 1.47 kitatumika kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja “C’’ Mkokotoni – Kaskazini Unguja, ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja "A" katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja ‘A’ Wilaya ya Kigamboni, Mkoa wa Kipolisi Temeke na kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja ‘’B’’ Wilayani Mbalizi mkoani Mbeya. Aidha, vipo vituo vinne (04) vya polisi daraja c ambavyo vimekamilika vimetajwa kwenye kitabu changu cha hotuba.

Miradi ya Kipaumbele ya Jeshi la Polisi katika mwaka 2021/2022
 
 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Jeshi la Polisi limepanga kutekeleza miradi ya kipaumbele ambayo ni: kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja ‘A’ Lushoto Mkoani Tanga kwa Shilingi milioni 250; kumalizia ujenzi wa jengo la Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara kwa gharama ya Shilingi milioni 450; kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja ‘C’ Ludewa - Njombe kwa gharama ya Shilingi milioni 300; kuendelea na ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja “A” Mtumba katika Mji wa Serikali, Dodoma kwa gharama ya Shilingi milioni 601.10; kuanza ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja “A” Kigamboni, Dar es Salaam utakao gharimu Shilingi milioni 899.48; kuanza ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja “C’’ Nyakanazi, Kagera kwa gharama ya Shilingi milioni 60; na kukarabati jengo la ofisi Kikosi cha Polisi Anga kwa gharama ya Shilingi milioni 120. Vilevile, miradi iliyoanza kutekelezwa kwa nguvu za wananchi itakamilishwa ambapo Shilingi milioni 200 zimetengwa kwa ajili ya mradi wa nyumba 12 za makazi, Kaskazini Pemba na Shilingi milioni 200 zitatumika katika mradi wa nyumba 14 za makazi, Kusini Pemba.

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Jeshi la Polisi litaendelea kuwashirikisha wadau katika ujenzi wa Vituo vya Polisi, majengo ya ofisi na makazi ya Askari nchini kote, pamoja na kumalizia miradi ya ujenzi iliyosimama. Hivyo, ninatumia fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika ujenzi wa vituo vya polisi na nyumba za makazi ya Askari ili kuimarisha hali ya ulinzi na usalama nchini.

JESHI LA MAGEREZA
 
Hali ya Ulinzi na Usalama Magerezani
 
 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza limeendelea kuwapokea, kuwalinda na kuwapatia huduma muhimu wahalifu wanaoletwa magerezani kwa mujibu wa sheria za nchi. Hadi kufikia Machi, 2021 jumla ya wafungwa na mahabusu 33,570 walikuwepo katika magereza yote nchini. Kutokana na msongamano wa wafungwa na mahabusu Magerezani, Jeshi la Magereza limeendelea kutumia utaratibu wa kifungo cha nje, ambapo katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Machi, 2021 jumla ya wafungwa 881 walitolewa magerezani kwa utaratibu wa kifungo cha nje. Aidha, wafungwa 3,319 waliachiliwa huru kwa Msamaha wa Mhe. Rais. Vilevile, kupitia Programu ya Huduma kwa Jamii na Huduma za Uangalizi, jumla ya wafungwa 2,253 walihukumiwa kutumikia adhabu zao kwenye jamii na hivyo kufanya jumla ya wafungwa wote waliotoka gerezani katika kipindi hicho kufikia wafungwa 6,453.

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza msongamano wa wafungwa. Kiasi cha Shilingi bilioni 1.24 kimetengwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Huduma kwa Jamii na Huduma za Uangalizi.

Kujitegemea kwa Chakula cha Wafungwa na Mahabusu
 
 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza linaendelea kutekeleza Mpango wa Mapinduzi ya Kilimo wa 2020/2021 – 2024/2025 kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa na mahabusu. Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 Jeshi la Magereza limefanikiwa kuvuna tani 4,720 za mahindi, tani 1,120 za mpunga, tani 298 za maharage na tani 43.6 za alizeti. Katika msimu wa mwaka 2020/2021, jumla ya ekari 11,185 zimelimwa, ambapo ekari 5,465 zimepandwa mahindi, 2,511 mpunga, 1,331 maharage na 1,490 zimepandwa alizeti kwa matarajio ya kuvuna tani 5,530.73 za mahindi, tani 1,478.63 za mpunga, tani 299.60 za maharage na tani 458.70 za alizeti. Katika mwaka 2020/2021 Shilingi Bilioni 6 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea kutekeleza Mkakati wa Mapinduzi ya Kilimo na kujitosheleza kwa chakula cha Wafungwa na Mahabusu.

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya kazi, Jeshi la Magereza limekamilisha ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu katika eneo la Msalato Dodoma ambayo ilizinduliwa na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 04 Februari, 2021. Aidha, jumla ya Shilingi bilioni 2.5 zilitolewa kwa ajili ya kuendelea na kazi zote zilizobaki. Aidha, Serikali ilitoa Shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa nyumba 173 zenye uwezo wa kukaa familia 326 zilizokuwa zimeanza kujengwa kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika maeneo ya magereza. Kati ya hizo, nyumba 79 zimekamilika na nyumba 94 zinaendelea kukamilishwa. Pia, mwezi Februari, 2021 Serikali ilitoa Shilingi bilioni 7.28 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za maafisa na askari 119 za kuishi familia 210 katika maeneo ya magereza nchini.

 1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2021/2022, Jeshi la Magereza linatarajia kujenga nyumba 129 za makazi ya maafisa na askari kulingana na rasilimali zinazopatikana katika magereza husika. Ujenzi huo utasaidia kupunguza changamoto ya nyumba za makazi ambapo kwa sasa zipo nyumba 5,057 ikilinganishwa na mahitaji ya nyumba 12,500 zinazohitajika.

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Magereza, Serikali imelipatia Jeshi hilo magari tisa (9) kwa ajili ya shughuli za utawala. Magari hayo yamesaidia kupunguza changamoto ya usafiri kwa Viongozi Waandamizi wa Jeshi la Magereza. Aidha, kwa mwaka 2021/2022, Shilingi bilioni 4.66 zimetengwa kwa ajili ya kununua magari 23 ya shughuli za Jeshi la Magereza.

Utekelezaji wa Lengo la Uchumi wa Viwanda

 1. Mheshimiwa Spika, katika kusaidia kufikiwa kwa lengo la uchumi wa viwanda, Jeshi la Magereza linakamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kiwanda cha Samani Msalato na ufungaji wa mashine, ambao umefikia zaidi ya asilimia 90 na utakamilika mwezi Juni, 2021.

 1. Mheshimiwa Spika, kupitia Shirika la Magareza, Jeshi limefanikiwa kujenga kiwanda kipya Mjini Moshi cha kuzalisha bidhaa za ngozi kwa ubia na PSSSF. Ujenzi huo umegharimu Shilingi bilioni 9.63. Kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha jozi 3,000 za viatu kwa siku kilizinduliwa tarehe 22 Oktoba, 2020 na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Vilevile, ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza soli za viatu umekamilika na ufungaji wa mashine unaendelea. Aidha, ujenzi wa kiwanda kingine cha kuchakata ngozi katika eneo hilo umefikia asilimia 75 na umepangwa kukamilika mwezi Mei, 2021. Aidha, Shirika limekamilisha ujenzi wa majengo mbalimbali ya Kiwanda cha Sukari cha Kampuni Hodhi ya Mkulazi, yatakayogharimu jumla ya Shilingi bilioni 2.34.

JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI
 
 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea kutekeleza jukumu lake la msingi, ambapo limefanya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto katika magari na maeneo mbalimbali. Hadi kufikia mwezi Machi, 2021 jumla ya maeneo 36,703 yalikaguliwa, ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 5.25 kilikusanywa kutokana na ukaguzi huo. Aidha, Jeshi hilo lilifanikiwa kuzima moto na kufanya uokoaji katika matukio 2,172. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa huduma hizo, wadau wametoa msaada wa magari 10 ya utawala. Katika mwaka 2021/2022, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limepanga kununua magari nane (8) ya utawala na magari mawili (2) ya kuzima moto pamoja na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kuzima moto na uokoaji.

Miradi Inayotekelezwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Maafisa na Askari Eneo la Kikombo Jijini Dodoma, ambapo ujenzi wa majengo sita (6) yenye ghorofa tano (5) umekamilika na jumla ya Shilingi bilioni 2.9 zimetumika. Pia, Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Zimamoto Wilaya ya Chamwino – Dodoma umefikia asilimia 75. Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.19 zilizotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mfuko wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Jiji la Dodoma.

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Jeshi la Zimamoto na Ukoaji litakamilisha mradi wa ujenzi wa Nyumba za Maafisa na Askari katika eneo la Kikombo Jijini Dodoma, ujenzi wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji, Nzuguni Jijini Dodoma na kukarabati Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Ilala, Jijini Dar es Salaam.

IDARA YA UHAMIAJI

 1. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya utoaji wa huduma kwa wageni na raia kupitia mfumo wa kielektroniki. Kwa sasa usimikaji wa mfumo wa usimamizi na udhibiti wa mipaka (e-border system) unakamilishwa katika ofisi za Uhamiaji za Mikoa. Aidha, katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, zoezi la kuunganisha mfumo wa kieletroniki wa malipo ya Serikali (GePG) linaendelea katika ofisi za uhamiaji. Hadi kufikia mwezi Machi, 2021 mfumo huo umeunganishwa katika ofisi za uhamiaji za mikoa 29, vituo 16 vya kuingia na kutoka nchini na ofisi 44 za Ubalozi wa Tanzania. Katika mwaka 2021/2022 zoezi la uunganishaji wa mfumo huo litaendelea katika mikoa na vituo vya uhamiaji vilivyobaki.

Misako, Doria na Ukaguzi
 
 1. Mheshimiwa Spika, shughuli za misako, doria na kaguzi zimeendelea kufanyika katika maeneo ya mipakani, migodini, viwandani, hotelini na kwenye mashamba makubwa. Lengo ni kudhibiti wahamiaji haramu ikiwa ni pamoja na kuwabaini wageni wanaofanya kazi kinyume na sheria. Katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Machi, 2021 jumla ya watuhumiwa 15,786 wa makosa ya kiuhamiaji walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Katika kuimarisha shughuli za misako na doria Serikali imetoa magari 16 kwa Idara ya Uhamiaji. Aidha, ununuzi wa magari sita (6) umekamilika na hadi kufikia mwezi Juni, 2021 magari yote yatakua yamepokelewa.

Miradi na Maeneo ya Kipaumbele ya Idara ya Uhamiaji katika Mwaka 2021/2022
 
 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji itaendelea na: ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Jijini Dodoma; ujenzi wa majengo ya ofisi zilizopo katika Mikoa ya Geita kwa gharama ya Shilingi milioni 813.49; Mtwara Shilingi milioni 878.66; na Lindi Shilingi milioni 297.32. Aidha, makazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji yataboreshwa kwa kufanya ukarabati wa nyumba katika Mikoa ya Tabora na Pwani, ambapo jumla ya Shilingi milioni 300 zimetengwa. Vilevile, ununuzi wa nyumba 12 za makazi katika eneo la Msamala mkoani Ruvuma utafanyika kwa gharama ya Shilingi milioni 250; kuanza ujenzi wa madarasa katika Kambi ya Mafunzo ya Uhamiaji Boma Kichakamiba mkoani Tanga utakaogharimu Shilingi milioni 900; na ununuzi wa magari sita (6) kwa gharama ya Shilingi milioni 960.

MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA)
Usajili na Utambuzi wa Watu
 
 1. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2021 usajili wa wananchi umefikia watu 22,345,948 ikilinganishwa na lengo la kusajili watu 25,237,954.  Pia, Namba za Utambulisho 18,762,822 zimezalishwa na kugawiwa kwa wananchi. Aidha, NIDA imezalisha na kusambaza vitambulisho 925,342 na hivyo kufanya idadi ya vitambulisho vilivyozalishwa na kusambazwa hadi Machi, 2021 kufikia 7,028,567 katika wilaya 34 za Tanzania Bara na Zanzibar. Kazi ya uzalishaji vitambulisho katika wilaya 116 zilizobaki inaendelea na inatarajiwa kukamilika Julai, 2021.

 1. Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, NIDA imeendelea kuunganisha taasisi za umma na binafsi katika Kanzidata yake. Lengo ni kuwawezesha wadau kuhakiki taarifa za watu wanaopata huduma na hivyo kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa jamii na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi. Kuanzia Julai, 2020 hadi Machi, 2021 Mikataba 45 ya ushirikishanaji taarifa imesainiwa na maombi mengine 22 ya wadau yanashughulikiwa. Kupitia mikataba hiyo, NIDA iliweza kuvuka lengo kwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 10.37 ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya Shilingi bilioni 8.16 sawa na asilimia 127.

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, NIDA itaendelea na zoezi la usajili na utambuzi katika wilaya na mikoa yote nchini na jumla ya Shilingi bilioni 10.08 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za hizo.

USAJILI NA USIMAMIZI WA JUMUIYA ZA KIDINI NA ZISIZO ZA KIDINI

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya ina jukumu la kusajili Jumuiya za Kidini na zisizo za Kidini, kufuatilia utendaji, uendeshaji na kushiriki katika utatuzi wa migogoro ya jumuiya zilizosajiliwa. Kwa kipindi cha Julai, 2020 hadi Machi, 2021 jumla maombi ya usajili wa jumuiya 331 yalipokelewa. Jumuiya 124 zilisajiliwa, ambapo 10 ni za kidini na 114 zisizo za kidini. Maombi matatu (3) yamekataliwa kwa kutokutimiza vigezo vya kusajiliwa na 104 yanaendelea kufanyiwa kazi. Aidha, migogoro tisa (9) imesuluhishwa kati ya 11 iliyokuwepo.

 1. Mheshimiwa Spika, uhakiki wa takwimu umefanyika kwa jumuiya zote zilizosajiliwa kuanzia mwaka 1955 hadi 2021 na hadi kufikia mwezi Machi, 2021 jumla ya jumuiya 9,836 zilikuwa zimesajiliwa, zikiwemo 992 za Kidini na 8,844 zisizo za Kidini.. Ninatoa wito kwa vikundi ambavyo havijasajiliwa vifike Ofisi ya Msajili wa Jumuiya kwa ajili ya kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337.

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itafungua ofisi nne (4) za Msajili wa Jumuiya katika Kanda ya Mashariki kwenye Mkoa wa Dar es Salaam, Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza, Nyanda za Juu Mkoa wa Mbeya na Kanda ya Kaskazini Mkoa wa Kilimanjaro kwa lengo la kurahisisha utoaji huduma kwa jamii. Aidha, elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kusajili vikundi na vyama mbalimbali vya kijamii itaendelea kutolewa.

UDHIBITI WA BIASHARA HARAMU YA USAFIRISHAJI WA BINADAMU
 
 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2020/2021, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kuwaokoa na kuwasaidia jumla ya wahanga 165 waliokuwa wanatumikishwa kufanya kazi kinyume na sheria. Kati yao, wahanga 163 walikuwa wanatumikishwa hapa nchini na wahanga wawili (2) walikuwa nchini Iraq na Malaysia. Wahanga wote walipewa huduma muhimu kama chakula, matibabu, msaada wa kisheria na wa kisaikolojia. Vilevile, Wizara iliratibu zoezi la kutambua familia za wahanga 77 Raia wa Tanzania na kuwaunganisha na familia zao. Katika kipindi hicho, wahalifu 26 wanaojihusisha na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu walikamatwa na jumla ya kesi saba (7) zilifunguliwa mahakamani.

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara kupitia Sekretariati ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu imepanga kufanya kazi za kipaumbele zikiwemo: kukamilisha uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu (2021 – 2024) na kuanza utekelezaji wake; kuimarisha ulinzi, usalama na uhifadhi wa wahanga (Victims Protection); kuendelea kuandaa na kutekeleza miongozo (Standard Operating Procedures) kwa ajili ya kutambua wahanga na kuwawezesha kupata huduma mbalimbali; kuandaa utaratibu wa kitaifa wa kutoa rufaa kwa wahanga; na kuandaa mfumo wa kitaifa wa uratibu wa masuala ya biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

HUDUMA KWA WAKIMBIZI

 1. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi, 2021 Serikali ilikuwa ina waomba hifadhi na wakimbizi 273,252. Pia, huduma za kijamii zinaendelea kutolewa kwa wakimbizi na waomba hifadhi kwa kushirikiana na UNHCR, WFP pamoja na mashirika ya hisani ya kimataifa na ya ndani ya nchi. Katika kuwatafutia suluhisho la kudumu wakimbizi, Serikali kwa kushirikiana na UNHCR na IOM imewahamishia nchi ya tatu (resettlement) jumla ya wakimbizi 1,047, ambao walipelekwa Australia, Canada, Ireland, Marekani, Ubelgiji na Ufaransa. Aidha, Wakimbizi 31,432 walirejeshwa kwa hiari nchini Burundi.
 2. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kuwahudumia wakimbizi na kuwatafutia suluhisho la kudumu, kushughulikia maombi ya waomba hifadhi na kusimamia ulinzi na usalama katika kambi za wakimbizi. Aidha, itaendelea na programu za utunzaji wa mazingira katika kambi za wakimbizi na maeneo yanayozunguka kambi hizo. Fedha zilizotengwa kwa kazi hizo ni jumla ya Shilingi milioni 640.96.

 1. SHUKURANI

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mhe. Samia Suluhu Hassan – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuiongoza Wizara hii, pamoja na maelekezo na miongozo yake kwangu na kwa Wizara ninayoiongoza. Mwenyezi Mungu amjalie Rais wetu Neema ya Uhai na Afya njema ili aweza kusimamia utekelezaji wa Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020, kwa mafanikio makubwa huku Nchi ikiwa na Amani na Utulivu.

Mheshimiwa Spika, namshukuru pia Mhe. Dr. Philip Isdor Mpango – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo na miongozo yao wanayotupatia katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara yetu.
Mheshimiwa Spika, Nakushukuru wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Mhe. Mussa Azan Zungu (Mb.) na Wajumbe wa Kamati hiyo kwa kutoa ushauri wa kuboresha mambo mbalimbali katika Wizara ikiwemo kupitia na kuchambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2021/2022. 
 
 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, ninatoa shukrani zangu za dhati kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Khamis Hamza Khamis (Mb) Jimbo la Uzini, Kusini Unguja kwa kunisaidia kusimamia majukumu ya Wizara ikiwemo kujibu maswali ya Wabunge na kutoa ufafanuzi wa hoja zinazowasilishwa hapa Bungeni. Aidha, ninawashukuru Katibu Mkuu Ndugu Christopher Derrick Kadio na Naibu Katibu Mkuu Ndugu Ramadhan Kombwey Kailima kwa usimamizi wao madhubuti wa utekelezaji wa kazi za Wizara.

 1. Mheshimiwa Spika, pia, shukrani zangu za dhati ninazitoa kwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, nikianza na Inspekta Jenerali wa Polisi - Bw. Simon Nyankoro Sirro; Kamishna Jenerali wa Magereza – Meja Jenerali Seleman Mzee; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji - Dkt. Anna Makakala; Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji – Bw. John Masunga; ambao wamewezesha kupatikana kwa mafanikio makubwa katika Wizara pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na Amani na Utulivu Nchini. Vilevile, ninamshukuru Prof. Suffian H. Bukurura Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Wajumbe wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi na Meja Jenerali Mstaafu Raphael M. Muhuga Mwenyekiti wa Bodi na Wajumbe wa Shirika la Uzalishaji Mali Jeshi la Magereza.

Aidha, nashukuru kwa dhati, Wakurugenzi, Wakurugenzi Wasaidizi, Makamishna, Makamishna Wasaidizi, Wakuu wa Vitengo, Maafisa, Askari na watumishi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuendelea kutekeleza vema shughuli za Wizara. Kwa namna ya pekee, ninazishukuru Jumuiya za Kidini na zisizo za Kidini, Vyombo vya Habari na Wananchi wote wa Tanzania kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
 
 1. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutoa shukrani za dhati kwa wadau wa maendeleo zikiwemo nchi za Botswana, Burundi, Ethiopia, Jamhuri ya Kenya, Jamhuri ya Korea Kusini, Malaysia, Seychelles, Ujerumani pamoja na Mashirika ya Kimataifa ya UNDP, UNHCR, UNICEF, IOM, UN – Women, RECSA pamoja na Taasisi ya TRI na Kampuniya GGML kwa kuendelea kutoa misaada ya kifedha, kijamii na kiufundi kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 

 1. Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini si kwa umuhimu, ninamshukuru sana mke wangu mpenzi Mariana William Naano, ndugu na jamaa kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu. Aidha, kwa namna ya pekee sana na kwa uzito mkubwa ninawashukuru wananchi wa Jimbo langu la Kibakwe kwa kuendelea kuniamini na kunipa ushirikiano katika kuendeleza umoja na mshikamano na kuchangia shughuli za maendeleo ya Jimbo letu. Nawashukuru sana na tuendelee kushikamana kwa ajili ya ustawi wa jimbo letu.

 1.    HITIMISHO
 1. Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa hoja ya kuomba fedha, ninaomba nikiri kuwa, Maafisa, Wakaguzi, Askari na Watumishi wa Vyombo vya Usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi walio wengi wanaishi kwenye makazi yasiyoridhisha na yasiyotosheleza. Aidha, katika wilaya nyingi kuna changamoto ya kutokuwepo kwa Vituo vya Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Ofisi za Uhamiaji. Kwa kutambua changamoto hii, Wizara iko mbioni kuandaa Mpango Kabambe wa Ujenzi wa Nyumba, Ofisi na Vituo kwa ajili ya Vyombo Vyote vya Usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Mpango huu umeanza kufanyiwa kazi katika ngazi ya wataalam na utakapokamilika utawasilishwa katika mamlaka husika ili kupata mwongozo kwa ajili ya kuendelea na hatua ya utekelezaji.

Makadirio ya Ukusanyaji Mapato kwa Mwaka 2021/2022
 
 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara imepanga kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi 494,917,473,000 kutoka vyanzo mbalimbali. Ili kufikia lengo hili Wizara itatekeleza mikakati mbalimbali ya ukusanyaji mapato ikiwemo ununuzi wa vitendea kazi kama magari na pikipiki na kuendelea kuunganisha na kutumia mifumo ya kieletroniki katika kutoa huduma.

Maombi ya Fedha kwa Mwaka 2021/2022

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba sasa Bunge lako Tukufu liidhinishe Bajeti ya jumla ya Shilingi 939,089,045,000 kwa ajili ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2021/2022. Kati ya fedha hizo, Shilingi 389,750,394,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo, Shilingi 521,868,651,000 ni Mishahara na Shilingi 27,470,000,000 ni fedha za Miradi ya Maendeleo. Kati ya Fedha za Maendeleo zinazoombwa, Shilingi 27,390,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 80,000,000 ni fedha za nje.

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa Hoja.

MHESHIMIWA SPIKA, NINAOMBA HOTUBA YANGU YOTE KAMA ILIVYOWASILISHWA KWA KATIBU WA BUNGE IINGIE KATIKA KUMBUKUMBU RASMI ZA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.
 
Back to Top