Sisi ni Nani?

Wizara ya Mambo  ya Ndani ya Nchi ni moja ya Wizara za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ina jukumu la kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na amani na utulivu.
Majukumu yake makuu ni:-

 1. Kulinda usalama wa raia na mali zao.
 2. Kuhifadhi na kuwarekebisha wafungwa.
 3. Kuwezesha na kusimamia utokaji na uingiaji nchini wa raia na wageni.
 4. Kusimamia masuala ya Zimamoto na Uokoaji.
 5. Kutoa huduma kwa wakimbizi waliopo nchini.
 6. Kusimamia Programu ya Huduma Kwa Jamii.
 7. Kujenga na kusimamia Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu na kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia na wageni wenye miaka 18 na kuendendea.

Muundo wa Wizara:
Kufuatana na Muundo uliopitishwa mwaka 2013,Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaundwa na Idara, na Vitengo vifuatavyo:

 1. Idara ya Jeshi la Polisi (Jeshi la Polisi);
 2. Idara ya Huduma za Magereza (Jeshi la Magereza);
 3. Idara ya Huduma za Uhamiaji (Idara ya Uhamiaji);
 4. Idara ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (Jeshi la Zimamoto na Uokoaji);
 5. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA);
 6. Idara ya Probesheni na Huduma za Jamii;
 7. Idara ya Kushughulikia Malalamiko;
 8. Idara ya Huduma za Sheria;
 9. Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu;
 10. Idara ya Sera na Mipango;
 11. Idara ya Usimamizi wa Manunuzi;
 12. Kitengo cha Fedha na Uhasibu;
 13. Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani;
 14. Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali;
 15. Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Dira
Dira ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kuwa Wizara ambayo itaifanya nchi yetu kuwa na amani na utulivu, mahali ambapo sheria zinaheshimika.
Dhamira
Dhamira ya Wizara ya mambo ya ndani ya Nchi ni kulinda maisha na mali, kuwezesha na kuthibiti utokaji na uingiaji nchini kwa raia na wageni, kuwarekebisha wafungwa na kutoa huduma kwa wakimbizi waliopo nchini.
Majukumu ya Idara na Vitengo:
 

 1. Jeshi la Polisi

Jukumu kubwa la Jeshi la Polisi ni kuhakikisha usalama na ulinzi wa raia na mali zao kwa kutunza amani na usalama, kutunza sheria na utulivu, kuzuia na kutambua uhalifu, kukamata na kutunza wahalifu na kulinda mali.
 
Idara za Jeshi la Polisi ni pamoja na:

 1. Divisheni ya Operesheni;
 2. Divesheni ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai;
 3. Devisheni ya Intelijensia.
 4. Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu.

Jeshi la Polisi linaongozwa na Inspekta Jenerali wa Polisi akisaidiwa na Naibu Kamishna Jenerali wa Polisi wakisaidiwa na Makamishna wa Divisheni, Kanda, Vitengo, Makamanda wa Vikosi mbalimbli na wa Mikoa, Wilaya na Vituo.
 
 

 1. Jeshi la Magereza

Jukumu kubwa la Jeshi la Magereza ni kutunza katika hali salama aina zote za wafungwa na kusimamia urekebishwaji wao.
Divisheni za Jeshi la Magereza ni:

 1. Divisheni ya Sheria na Shughuli za Magereza;
 2. Divisheni ya Huduma ya Urekebishaji;
 3. Divisheni ya Fedha na Utawala.

Vitengo vya Jeshi la Magereza ni pamoja na Kitengo cha Intelijensia na Operesheni na Kitengo cha Ukaguzi wa Magereza.  Jeshi la Magereza pia lina Shirika la Uzalishaji na Ofisi za Magereza za Mikoa na Wilaya.
Jeshi la Magereza linaongozwa na Kamishna Jenerali wa Magereza akisaidiwa na Makamishna wa Divisheni mbalimbali na Vitengo.

 1. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji

Majukumu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni kukinga na kupunguza idadi ya vifo, majeraha kwa watu, na uharibifu wa mali kutokana na moto, mafuriko, matetemeko, ajali za barabarani na majanga mengine.
Idara na Vitengo vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni pamoja na:

 1. Divisheni ya Usalama wa Moto;
 2. Divisheni ya Operesheni;
 3. Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu;
 4. Kitengo cha Sheria;
 5. Ofisi za Zimamoto na Uokoaji Mikoa;
 6. Ofisi za Zimamoto na Uokoaji Wilaya;
 7. Vituo vya Zimamoto na Uokoaji na;
 8. Chuo cha Zimamoto na Uokoaji.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaongozwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji akisaidiwa na Naibu Kamishna Jenerali, Makamishna na Makamanda wengine.
 

 1. Idara ya Uhamiaji

Jukumu la Idara ya Uhamiaji ni kuwezesha na kudhibiti utokaji na uingiaji nchini wa raia na wageni kufuatana na Sheria Na. 7 ya 1995, Sheria ya Uraia wa Tanzania Na. 6 ya 1995 na Sheria ya Pasi na Nyaraka za Kusafiria Na. 20 ya mwaka 2002 na Kanuni zinazoambatana na Sheria hizo.
Divisheni, Vitengo na Ofisi za Idara za Uhamiaji ni pamoja na:

 1. Divisheni  ya Pasi, Uraia na Utaifa;
 2. Divisheni ya Visa, Pasi na Vibali;
 3. Divisheni ya Usimamizi na Uthibiti wa Mipaka;
 4. Ofisi ya Zanzibar;
 5. Divisheni ya Utawala, Fedha na Uhasibu;
 6. Kitengo cha Sheria;
 7. Chuo cha Taaluma za Uhamiaji Tanzania; na
 8. Ofisi za Uhamiaji za Mikoa.

Idara ya Uhamiaji inaongozwa na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akisaidiwa na Makamishna na Wakuu wa Vitengo.

 1. Idara ya Wakimbizi

Jukumu la Idara ya Wakimbizi ni kusimamia masuala ya wakimbizi kufuatana na Sheria ya Wakimbizi ya mwaka 1998 na Sera ya Taifa ya Wakimbizi ya mwaka 2003.
Sehemu za Idara ya Wakimbizi ni:

 1. Sehemu ya Operesheni na Usalama;
 2. Sehemu ya Sheria na Ulinzi; na
 3. Sehemu ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu.

Idara hii inangozwa na Mkurugenzi akisaidiwa na Wakurugenzi Wasaidizi.
 
 

 1. Idara ya Probesheni na Huduma kwa Jamii

Jukumu la Idara ya Probesheni na Huduma kwa Jamii ni kusimamia adhabu mbadala katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Sheria ya Probesheni ya Wahalifu (Kifungu. 247 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002), Sheria ya Huduma kwa Jamii Na. 6/2002, Kanuni ya Kifungo cha Nje ya mwaka 1968 (EML) na Sheria ya Bodi za Paroli Na. 25/1994.
Sehemu ya Idara hii ni:

 1. Sehemu ya Probesheni
 2. Sehemu ya Huduma za Utunduizi

Idara hii inaongozwa na Mkurugenzi akisaidiwa na Wakurugenzi Wasaidizi.

 1. Idara ya Kushughulikia Malalamiko

Jukumu ya Idara ya kushughulikia Malalamiko ni kupokea na kushughulikia malalamiko yanayohusu utendaji wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Taasisi nyingine zilizo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Taasisi Binafsi za Ulinzi.
Sehemu za Idara za Malalamiko ni:

 1. Sehemu ya kushughulikia Malalamiko;
 2. Sehemu ya Sheria na Utafiti.

Idara hii inaongozwa na Mkurugenzi.

 1. Idara ya Huduma za Sheria

Jukumu la Idara ya Huduma za Sheria ni kutoa huduma za kisheria kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Sehemu ya Idara ya Huduma za Sheria ni:

 1. Sehemu ya Usajili wa Vyama vya Kijamii;
 2. Sehemu ya Huduma za Kisheria.

Idara hii inaongozwa na Mkurugenzi.
 

 1. Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu

Jukumu la Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu ni kutoa utaalamu wa huduma za utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu kwa Wizara.
Sehemu za Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilmaliwatu ni:

 1. Sehemu ya Utawala;
 2. Sehemu ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu.

Idara hii inaongozwa na Mkurugenzi akisaidiwa na Wakurugenzi Wasaidizi.

 1. Idara ya Sera na Mipango

Jukumu la Idara ya Sera na Mipango ni kutoa huduma za kitaalamu kuhusu masuala ya uandaaji wa Sera na utekelezaji wake, na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya Sera na Mipango ya Wizara.  
Sehemu za Idara ya Sera na Mipango ni:

 1. Sehemu ya Sera;
 2. Sehemu ya Mipango;
 3. Sehemu ya Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji Taarifa za Utekelezaji.

Idara hii inaongozwa na Mkurugenzi akisaidiwa na Wakurugenzi Wasaidizi.

 1. Idara ya Ununuzi na Ugavi

Jukumu la Idara ya Ununuzi na Ugavi ni kutoa huduma za kitaalamu kuhusu shughuli za ununuzi, utunzaji na ugavi wa vifaa na huduma kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Sehemu za Idara ya Ununuzi na Ugavi ni:

 1. Sehemu ya Ununizi;
 2. Sehemu ya Ugavi.

Idara hii inaongozwa na Mkurugenzi akisaidiwa na Wakuu wa Sehemu.
 

 1. Kitengo cha Fedha na Uhasibu

Jukumu la Kitengo cha Fedha na Uhasibu ni kutoa huduma kuhusu usimamizi wa fedha na utunzaji wa vitabu wa hesabu kwa Wizara.
Kitengo cha Fedha na Uhasibu kinaongozwa na  Mhasibu Mkuu.

 1. Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani

Jukumu la Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani ni kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Afisa Masuhuli (Katibu Mkuu) kuhusu usimamizi mzuri wa rasilimali za Wizara.
Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kinaongozwa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu.
 

 1. Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano

Jukumu la Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Wizara.
Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kinaongozwa na Mchambuzi wa Mifumo ya Kompyuta Mkuu.

 1. Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali

Jukumu la Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali ni kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu huduma za habari, elimu, mawasiliano na mijadala kwa umma na vyombo vya habari kwa Wizara.
Kitengo hiki kinaongozwa na Afisa Mkuu mwenye uelewa na uzoefu mpana wa shughuli za Wizara.
 
 
 

Back to Top