NAIBU WAZIRI AYOUB ACHANGIA MILIONI 9 UJENZI WA KITUO CHA POLISI CHAANI
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Chaani, Ayoub Mohammed Mahmoud, amechangia shilingi milioni Tisa (9,000,000) kwa ajili ya malipo ya fidia ya ardhi itakayowezesha ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi katika Wilaya ya Chaani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza leo baada ya kukabidhi fedha hizo katika eneo la kituo hicho, Mhe. Ayoub amesema mchango wake utaungana na shilingi milioni moja (1,000,000) zitakazotolewa na Jeshi la Polisi, na hivyo kufanya jumla ya shilingi milioni kumi (10,000,000) kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi waliokuwa wakidai stahiki zao.
Hatua hiyo imewezesha wananchi hao kuridhia kuachia eneo hilo rasmi kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho katika jitihada zao za kushiriki katika kuimarisha usalama wa wananchi wa Chaani katika jimbo hilo
Aidha, Mhe. Ayoub ameeleza kuwa maandalizi ya ujenzi huo yanatarajiwa kuanza ndani ya wiki mbili zijazo. Ameongeza kuwa Serikali imekusudia kukipandisha hadhi kituo hicho na kuwa Kituo cha Polisi cha Daraja C, ambapo ujenzi wake unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 220.
Katika hatua nyingine, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi, kwa kuendelea kusimamia kwa karibu mikakati ya kuimarisha Amani, Usalama na Utulivu nchini
