Tanzania logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

AYOUB:AJIRA 500 KUZALISHWA KUPITIA UWEKEZAJI WA UTALII ZANZIBAR


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema zaidi ya ajira 500 zinatarajiwa kuzalishwa kupitia uwekezaji unaoendelea Visiwani Zanzibar katika sekta ya utalii huku zaidi ya ajira 300 zisizohitaji utaalamu mkubwa zikitengwa kwa wananchi wa jimbo la Chaani na Wilaya kwa ujumla 


Mhe. Ayoub ameyasema hayo Aprili 12, 2026 aliposhiriki Mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Jimbo la Chaani, ambapo ameleza kuwa Serikali na viongozi wa eneo hilo wanaendelea kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unawanufaisha wananchi moja kwa moja kupitia fursa za ajira na ukuaji wa uchumi Visiwani humo


Amebainisha kuwa uwekezaji mkubwa unaoendelea katika eneo la Pwanimchangani, ikiwemo uwepo wa zaidi ya hoteli 10 za nyota tano pamoja na hoteli ndogondogo 30, umefungua fursa pana za ajira na biashara kwa wananchi wa eneo hilo.


Kadhalika, amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 zimebeba ujumbe muhimu unaoeleza kuwa dhamana ya kuleta maendeleo ni wajibu wa kila mwananchi, huku akisisitza kuwa kauli mbiu hiyo inapaswa kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo nchini.


Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Wazo Mwang'onda amewapongeza wawekezaji na wakandarasi wanaotekeleza miradi katika eneo hilo kwa uaminifu na uzingatiaji wa viwango vya ujenzi, huku akiwataka kuhakikisha wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na huduma na fursa zitokanazo na miradi hiyo kwa wakati.


Mwenge wa uhuru 2026 umebeba kauli mbiu isemayo "Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo"