Tanzania logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Maswali Yaulizwayo Mara kwa Mara

Mkimbizi ni mtu yeyote ambaye kutokana na hofu ya msingi ya kuteswa kwa sababu za rangi, dini, kabila, uanachama wa kundi la kijamii au maoni ya kisiasa, yuko nje ya nchi yake au nchi ya maskani yake ya kudumu na kwamba hawezi au hayuko tayari kuwa chini ya himaya ya Serikali hiyo ambayo ameikimbia.

Mhamiaji haramu ni raia wa kigeni aliye ndani ya Tanzania na asiye na kibali halali cha kuingia au kuishi Tanzania wakati Mkimbizi ni raia wa nchi ya kigeni aliyeomba na kupewa hifadhi kutokana na kuikimbia nchi yake kwa sababu za usalama wake

Waomba hifadhi wote wanapowasili nchini wanatakiwa kuripoti katika Ofisi zozote za Serikali ambako wataelekezwa kufika Idara ya Wakimbizi au kuonana na “Ofisa aliyeidhinishwa” ambaye atawapa utaratibu wa kufuata kufika Ofisi za Idara ambako watahojiwa na kusajiliwa.

Ifahamike kwamba maeneo wanayoishi wakimbizi ni maeneo tengefu, hivyo wageni wote wanaotaka kuingia katika maeneo haya kwa ajili ya kutoa huduma au sababu zozote zile; watapaswa kuandika barua ya kuomba kibali kwa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi. Hairuhusiwi kuingia maeneo tengefu bila kibali.

Usafirishaji haramu wa binadamu unahusisha kitendo cha kuajiri, kusafirisha, kuficha au kupokea mtu kwa njia ya vitisho, nguvu, udanganyifu au matumizi mabaya ya madaraka kwa lengo la unyonyaji. Unyonyaji unaweza kuwa wa kazi za kulazimishwa, ukahaba, kufanya kazi za ndani, kulazimishwa kuomba mtaani au kushirikishwa katika vitendo vya uhalifu.

Viini vinavyounda kosa la usafirishaji haramu wa binadamu ni;

·       Tendo Lenyewe: Kusajili, Kusafirisha, kuhamisha, kuhifadhi, kutoa au kupokea mtu kwa ajili ya kumtumikisha

·       Mbinu: kudanganya, kutisha au kutumia nguvu, kuteka na kutumia mikataba ya uongo

·       Nia/Kusudio: kutumikisha kingono, kufanyisha kazi ngumu, kulazimisha kuomba mitaani, kutoa viungo vya mwili na kufanyisha kazi za ndani

Ndiyo. Usafirishaji haramu wa binadamu ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Sura ya 432. Wahalifu hukabiliwa na adhabu kali ikiwemo kifungo cha maisha Gerezani.

Dalili ni pamoja na: haruhusiwi kuondoka sehemu ya kazi, kunyanganywa nyaraka binafsi, kufanya kazi kwa muda mrefu bila malipo au kwa malipo kidogo, anakula mabaki ya chakula kilichoachwa na mwajiri wake, ana makovu au vidonda ambavyo havijatibiwa kutokana na kuteswa, kuonyesha hofu au wasiwasi uliopitiliza, na kutumikishwa kwenye ukahaba au kazi za kinyonyaji.

Mtu yeyote anaweza kusafirishwa kiharamu, lakini makundi yaliyo hatarini zaidi ni wanawake, watoto, watu wenye ulemavu, maskini na wahamiaji wanaotafuta fursa.

Vichocheo ni pamoja na umaskini, ukosefu wa ajira, mahitaji ya nguvu kazi ya bei nafuu, ukahaba, migogoro ya kifamilia, ukosefu wa elimu, utandawazi, tamaa ya maisha mazuri na faida kubwa wanayoipata wahalifu wanaojihusisha na biashara hii.

Magendo kwa wahamaji yanahusisha kuvuka mipaka kinyume cha sheria kwa ridhaa ya mhusika, na mara nyingi huishia baada ya kuwasili eneo analokwenda. Usafirishaji haramu wa binadamu unahusisha unyonyaji, mara nyingi bila ridhaa, na huendelea hata baada ya kufika mwisho wa safari.

Kwa Waathirika: mateso, msongo wa mawazo, unyanyapaa, magonjwa, kupoteza uhuru na kifo. Kwa Familia: utengano, mzigo wa kifedha. Kwa Taifa: hasara ya kiuchumi, machafuko ya kijamii na kudhalilika kimataifa.

Kupitia Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu (Sura 432), kupitia Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirshaji Haramu wa Binadamu, kampeni za uelimishaji, mafunzo na ushirikiano na taasisi mbalimbali zikiwemo za kimataifa.

Ripoti mara moja katika kituo cha Polisi, piga simu kwenye namba ya dharura 195 ya Sekretarieti ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu, au toa taarifa kwa viongozi wa eneo husika.

Waathirika hupata msaada wa uokoaji, makazi salama ya muda, huduma za afya, ushauri, msaada wa kisheria, utafutaji wa familia, msaada wa kurejeshwa kwenye jamii, na ulinzi wa haki na utambulisho wao.

Kujielimisha, kuripoti matukio yanayotiliwa shaka, kusaidia familia zilizo hatarini, na kuelimisha jamii kupitia shule, makanisa, misikiti na mikutano ya kijamii.

Tembelea ofisi ya Sekretarieti au tovuti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, fuatilia kampeni za uelimishaji, au piga simu kwa namba ya dharura 195.