Tanzania logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

SERIKALI YARIDHIA OMBI LA KUJENGA KITUO CHA POLISI MATEMWE KUIMARISHA USALAMA


Serikali imeridhia kujenga Kituo cha Polisi katika eneo la Matemwe, Jimbo la Mkwajuni, Visiwani Zanzibar  kufuatia kukua kwa kasi kwa shughuli za Utalii na uwekezaji katika ukanda huo.


Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni, Mhe.  Ali Vwai Hamisi kuhusu Changamoto ya ukosefu wa Kituo cha Polisi eneo la Matemwe 


Naibu Waziri amesema hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo ni kupatikana kwa eneo rasmi la ardhi litakalotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, akibainisha kuwa kwa sasa bado hakuna eneo lililotengwa kwa matumizi hayo. 


Aidha, amemshauri Mbunge huyo kushirikiana na Kamisheni ya Ardhi Zanzibar kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kutenga eneo kwa ajili ya mradi huo.


Kuhusu hali ya usalama katika eneo hilo, amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha doria za kila siku katika ukanda wa huo wa Utalii unaojumuisha Matemwe, Pwanimchangani, Kiwengwa hadi Nungwi kupitia Kituo Kikuu cha Polisi Mkokotoni ili kuhakikisha usalama wa wageni na wananchi unaimarika wakati wote.


Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bumbwini, Mheshimiwa Mwinyi Jamal Ramadhan, kuhusu vigezo vinavyotumika katika ujenzi wa vituo vya polisi, Naibu Waziri amesema Serikali hutumia mfumo wa Security Audit (Ukaguzi wa Kiusalama) unaozingatia kiwango cha matishio ya kiusalama, viashiria vya uhalifu pamoja na umuhimu wa kimkakati wa eneo husika.