Tanzania logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Nitafanya kazi kwa Uadilifu na Uaminifu-Katambi


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,  Patrobas Katambi, ameahidi kuwa Tume ya Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji itaendelea kufanya maamuzi kwa haki, uadilifu na kwa kuzingatia misingi ya kisheria, akisisitiza kuwa maamuzi yote yatakayofanywa yatatokana na kusikiliza pande zote na kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

Waziri Katambi amesema hayo leo,  baada ya uapisho wa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji uliofanyika jijini Dodoma ambapo  Naibu Waziri,Ayoub Mohamed Mahmoud pia aliapa kuwa Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo.

‘Tume hii haitatoka nje ya misingi ya utaratibu wa kufanya maamuzi, tutahakikisha wakati wote Tume inafanya wajibu wake kwa mujibu wa sheria na taratibu ili kusaidia Mahakama na Bunge katika utekelezaji wa majukumu yake ya kikatiba.’ Amesema Waziri  Katambi

 Waziri Katambi amebainisha kuwa Tume hiyo haitatoka nje ya misingi ya utaratibu wa kufanya maamuzi, huku ikihakikisha haki inatendeka kwa wakati wote kwa mujibu wa sheria, ili kusaidia Mamlaka za Mahakama katika utekelezaji wa majukumu yao ya kikatiba.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud, ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ana malengo makubwa na utashi wa dhati wa kuhakikisha wananchi wanaishi maisha bora kwa kuimarisha misingi ya utawala wa sheria na katiba

"Kuapishwa kwetu ni  kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Taifa linaendelea kuendeshwa kwa misingi ya Katiba, sheria na taratibu, ili kulinda maslahi ya wananchi’ Ameongeza Naibu Waziri  Ayoub

Akizungumza baada ya  uapisho huo, Mheshimiwa Jaji,Suleiman Haji Hassan amewapongeza kwa kiapo hicho na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, na misingi ya kikatiba. Pia, amewatakia heri katika nafasi zao za uwaziri na naibu uwaziri, na kuwaombea waweze kutimiza majukumu yao kwa uadilifu, hekima na uaminifu kwa maslahi mapana ya Taifa.