MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR, ATOA WITO WA KUKUZA MAADILI MEMA
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameiagiza jamii kuendelea kukuza maadili mema, mshikamano, na kupambana dhidi ya mmomonyoko wa maadili, kwa kutumia mwanga wa Qur’an Tukufu ili kujenga jamii yenye mshikamano wa kweli.
Mhe. Abdulla amesema hayo katika Hafla ya Uzinduzi wa Mashindano ya Kuhifadhi Qur’an Tukufu iliyofanyika jijini Dar es Salaam, leo Februari 1, 2026
Aidha, ametoa wito kwa wahitimu wa Qur’an Tukufu na jamii kuendelea kutenda matendo mema na kukatazana mabaya, ili kujenga jamii yenye malezi bora
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ayoub Mohammed Mahomud, amesema kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa jumuiya za kidini, bila kujali ukubwa au udogo wa Taasisi, ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, uwazi, uwajibikaji, na kwa kuzingatia kikamilifu sheria za nchi.
Pia, Mhe. Ayoub amesisitiza kuwa viongozi wa kiroho wanapaswa kutambua wajibu wao wa kulinda amani, mshikamano na umoja kwa kuhubiri maadili mema, upendo, na kukemea maovu yanayoweza kuhatarisha ustawi wa jamii, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho
Kadhalika, Mwenyekiti wa Taasisi ya Al - Hikma Foundation Sheikh Nudreen Kishk, ameeleza kuwa mashindano hayo yalianza rasmi mwaka 1998 ndani ya Madrasa ya Al-Hikma, Awali yalianza kama mashindano ya mtaa, yakaja wilaya, yakafuatia mkoa, yakawa ya kitaifa, na sasa ni mashindano makubwa zaidi ya Qur’an Tukufu ya Mabara yote ulimwenguni.
