WAZIRI KATAMBI AHIMIZA WATANZANIA KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII WA NDANI
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Protabas Katambi, ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi za taifa na mbuga za wanyamapori zilizopo hapa nchini, ili kukuza uchumi wa taifa.
Ameyasema hayo, Februari 26, 2026 alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro iliyopo mkoani Arusha, akiwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Zambia, Mhe. Jack Mwiimbu pamoja na wajumbe wengine walioshiriki Mkutano wa Nne wa Kamati ya Wataalamu wa Kamisheni ya Kudumu ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama (JPCDS) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Katambi amesema vivutio vya kipekee vilivyopo Ngorongoro ni tunu adhimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni fahari kwa Taifa, huku akisisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kujivunia rasilimali hizo na kuzitumia kama fursa ya kujifunza, kuburudika na kuchangia maendeleo ya nchi.
Aidha, Mhe. Katambi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuhamasisha utalii kupitia filamu ya kimataifa ya The Royal Tour, ambayo imeitangaza Tanzania duniani na kuvutia idadi kubwa ya watalii kutoka mataifa mbalimbali.
“Taarifa nilizozipata hapa getini zinaonesha kuwa jumla ya watalii takribani elfu tatu kwa mwezi hutembelea hifadhi hii, hii ni idadi kubwa inayochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa pato la taifa,” alisisitiza Mhe. Katambi.
Kwa upande wake, Mhe. Jack Mwiimbu amepongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Zambia, akieleza kuwa ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza namna ambavyo Tanzania imefanikiwa kuhifadhi rasilimali zake za asili huku ikiendeleza sekta ya utalii kwa manufaa ya wananchi wake.
Ziara hiyo ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, sambamba na kutembelea na kujionea vivutio vya utalii vinavyoitangaza Tanzania Kimataifa.
