MAKAMU WA RAIS ASISITIZA USHIRIKIANO KATI YA JESHI LA POLISI NA WADAU WA UCHAGUZI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ni muhimu Jeshi la Polisi kuimarisha ushirikiano wa karibu na wadau wote wa uchaguzi, hatua ambayo itasaidia kuhakikisha kila mdau anatendewa haki, na kuondoa tofauti zinazoweza kusababisha migongano.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi uliofanyika katika ukumbi wa Chuo Cha Polisi (CCP) Moshi Mkoani Kilimanjaro Agosti 11, 2025
Mhe. Dkt. Mpango amesema kuwa baadhi ya maeneo muhimu ya ushirikiano ni pamoja na kuhakikisha mikutano ya kampeni inafanyika kwenye maeneo yaliyoruhusiwa na ndani ya muda uliopangwa sambamba na kuimarisha usalama wa wagombea na viongozi wa vyama vya kisiasa, bila kujali vyama vyao au itikadi zao.
Aidha, Makamu wa Rais amelitaka Jeshi la Polisi kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Taasisi nyingine za Serikali ili kujiandaa vyema kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufuatilia taarifa mbalimbali zenye mlengo wa uchochezi, zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari.
Naye, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amesema kuwa Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha Jeshi hilo linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia weledi, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.Pia, amepongeza jitihada za Jeshi hilo katika ufanisi wake wa kudumisha amani na kusimamia usalama wa raia na mali zao
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, amebainisha kuwa Jeshi hilo halitawavumilia watu wanaojificha chini ya mwamvuli wa siasa ambao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kufanya vitendo vya uhalifu wakiwa na dhamira ya kuvuruga amani ya nchi.