WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI YAENDESHA MAFUNZO ELEKEZI KWA WATUMISHI WAPYA.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bi. Miriam Mmbaga, amefungua mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa Wizara hiyo leo, Agosti 12, 2025, jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Bi. Mmbaga amewasisitiza washiriki kuwa na uelewa wa Sheria za Nchi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kulingana na idara na maeneo ya utendaji kazi.
"Baada ya mafunzo haya, tafuteni Sheria za Nchi na mzisome, kwa sababu katika Utumishi wa Umma hakuna kitu bora kama kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, sambamba na busara na hekima," alisema Bi. Mmbaga.
Washiriki wa mafunzo hayo wanatarajiwa kupata uelewa wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, elimu ya uwekezaji wa fedha kupitia hisa, maadili ya utendaji wa umma, kutunza siri na usalama wa nyaraka pamoja na huduma bora kwa wateja.
Kwa upande wake, mwenzeshaji wa mafunzo hayo, Bi. Katrina Makobwe, alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa waajiriwa wapya kwani yanawapa uelewa wa majukumu yao kazini.