KATIBU MKUU GUGU ATOA WITO KWA POLISI KUJIPANGA KUIMARISHA USALAMA WAKATI WA UCHAGUZI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu amesisitiza umuhimu wa Jeshi la Polisi kujipanga vizuri na kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika katika hali ya utulivu huku akihimiza Jeshi hilo kuendelea kubaini vishiria vya uvunjifu wa amani na uchochezi kwenye Mitandao ya Kijamii wakati wa Uchaguzi kwa kushirikiana na wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kudhibiti makosa ya Kimtandao.
Akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Agosti 15, 2025 Shule ya Polisi Tanzania, Moshi Katibu Mkuu Gugu amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia kwa umakini utekelezaji wa mikakati ya kiusalama kuelekea uchaguzi Mkuu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhuisha mipangokazi ya uchaguzi, kutoa mafunzo kwa Maafisa na Askari, na kuhakikisha doria na ulinzi wa misafara ya kisiasa unafanyika kwa ufanisi ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika katika mazingira ya amani na usalama.