Tanzania logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI AFUNGA MAFUNZO YA AWALI YA ASKARI WAPYA WA UHAMIAJI ZAIDI YA 500. ‎


‎Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ally Gugu jana tarehe 03 Oktoba 2025 amehitimisha mafunzo ya Awali ya Askari wapya wa Uhamiaji zaidi ya 500 Kozi Namba 04/2025 Katika Chuo Cha Uhamiaji Raphael Kubaga kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga.

‎‎Akitoa hotuba yake katika hafla hiyo Katibu Mkuu Bw. Gugu amesema askari hao wapya wamebahatika kupata nafasi hizo za ajira za kuitumikia Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji kuwa mafunzo waliyoyapata yakawasaidie kuwa watendaji wazuri na wenye kuzingatia maadili ya kazi na Utumishi wa Umma.

‎Aidha amewakumbusha  kuwa tarehe 29 Oktoba, 2025 ni siku ya Uchaguzi Mkuu; hivyo wanatakiwa kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu.

‎Pamoja na mambo mengine Bw. Gugu ameitaka Idara ya Uhamiaji Kuimarisha Doria na Misako hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu sanjari na

‎Kushirikiana na Tume ya Uchaguzi kutoa Elimu kwa Umma kuhusu masuala ya Uraia, Kutatua kwa haraka mapingamizi ya uraia kwa wagombea wa nafasi mbalimbali, Kuendelea kushirikiana na NIDA kutoa Vitambulisho vya Utaifa,Kudhibiti Uhamiaji haramu, Walowezi, Wakimbizi na raia wa kigeni kujipenyeza kushiriki uchaguzi mkuu.

‎Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Uhamiaji CGI Dkt. Anna Makakala ametoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuendelea kuipatia fursa mbali mbali Idara ya Uhamiaji ikiwemo fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukamilishaji wa majengo ya Ofisi na nyumba za makazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji. 

‎Mafunzo hayo yaliyofungwa yanajumuisha askari 554. Idadi hii ni chachu ya nguvu kazi mpya katika Idara ya Uhamiaji.