WAFUNGWA KIFUNGO CHA NJE MKOA WA KAGERA WAZALISHA MICHE YA KAHAWA
Katika maadhimisho ya Siku ya Wakulima nchini Nanenane 2026, ambayo kwa mkoa wa Kagera yanafanyika kwenye viwanja vya Kyakairabwa, Bukoba, Ofisi ya Divisheni ya Huduma za Uangalizi Mkoa wa Kagera imekuwa mfano bora wa kazi zinazofanywa na wafungwa wanaotumikia adhabu mbadala chini ya Usimamizi wa Divisheni ya Huduma za Uangalizi mkoani humo.
Wafungwa hao wameonesha vitalu vya miche bora ya kahawa, miche bora ya miti ya mbao, na miche bora ya matunda itakayogawiwa bure kwa wananchi.
Aidha, kupitia maonesho hayo, wananchi wamepata fursa ya kujifunza utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo yao.
Hatua hiyo ya ugawaji wa miche, inakusudia kuwanufaisha wananchi kwa kutunza mazingira, kuimarisha ushirikiano kati ya Divisheni ya Huduma za Uangalizi na Jamii inayohudumiwa, kuwawezesha wafungwa wa vifungo vya nje kupata stadi, na ujuzi wa kuanzisha vitalu kwa ajili ya kujiingizia kipato mara wamazapo kutumikia adhabu, na kuwapa matumaini ya kurejea kwenye jamii wakiwa na mchango wa kuisaidia jamii inayowazunguka.
