LINDI YATOA SOMO UTATUZI WA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, ameupongeza Mkoa wa Lindi pamoja na wananchi kwa mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti migogoro kati ya wakulima na wafugaji
Akizungumza katika Maadhimisho ya Nane Nane mkoani Lindi, Mhe. Ayoub amesema mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali, vyombo vya Usalama pamoja na wananchi katika kutafuta suluhu ya changamoto hizo.
Amesema awali mkoa huo ulikuwa ukishuhudia watu kati ya 27 hadi 30 wakipoteza maisha kila mwaka kutokana na migogoro ya wakulima na wafugaji, hali ambayo imebadilika kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wananchi.
Kadhalika, amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, pamoja Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi ACP John Imori kwa kuhakikisha wakulima na wafugaji wanaishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji badala ya kutumia nguvu katika migogoro.
Ameeongeza kuwa mafanikio hayo hayawezi kupatikana kwa juhudi za Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa wananchi ambao wamekuwa tayari kushirikiana na vyombo vya Usalama katika kutafuta suluhu za migogoro hiyo
Naibu Waziri ametoa rai kwa mikoa mingine nchini kuiga mfano wa Lindi kwa kuimarisha ushirikiano kati yao na viongozi, ili kumaliza kabisa migogoro ya wakulima na wafugaji katika jamii zao
