SERIKALI YATANGAZA MABADILIKO JESHI LA MAGEREZA
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,George Simbachawene amesema kuna haja ya kubadili Mfumo wa Magereza nchini ili kuendana na kasi ya dunia huku akigusia dhamira ya serikali kupitia baadhi ya sheria ambazo tumerithi kutoka kwa wakoloni na kuzifanyia mabadiliko ili kuweza kuboresha masuala ya utoaji haki katika vyombo mbalimbali vya haki jinai ikiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza.
Ametoa kauli hiyo
leo, jijini Dodoma baada ya kuapishwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Jeshi la
Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambayo kazi yake ni
Kumshauri Rais juu ya Utekelezaji wa majukumu aliyokabidhiwa Rais na ibara ya
36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sambamba na ujazaji wa
nafasi hizo katika Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza, kama Rais
atakavyotaka.
‘Ni lazima kweli
tutoke kwenye magereza ya kikoloni na sasa tuje kwenye magereza ya Jamhuri
ambayo ni watu huru wanaoishi katika nchi ya kidemokrasia inayotambua haki za
binadamu lakini pia kuna haja ya kufanya mabadiliko ya sheria maana dunia ya
sasa na kwa Uchumi tuliofikia lazima tufanye mabadiliko ziko sheria zetu
nyingine bado ni za kikoloni kwahiyo ipo haja ya kuzibadilisha na hilo
litashirikisha wadau wote waliopo kwenye mnyororo huu wa sheria na masuala ya
haki jinai.’ alisema Waziri Simbachawene
Akizungumza
Jaji Mfawidhi Kanda ya Dodoma,Mheshimiwa, Dkt. Juliana Masabo amepongeza
mabadiliko mbalimbali yanayoendelea kwenye vyombo vya usalama vilvyopo chini ya
wizara akikiri mabadiliko hayo yanasaidia mchakato wa utolewaji haki na
kupunguza badhi ya mambo ikiwemo masuala ya upelelzi kuchelewa.
‘Nakiri kuna
mabadiliko sana hasa magereza niliyotembelea masuala ya teknolojia ya Habari na
Mawasiliano yamesaidia kesi kuendeshwa kwa haraka kwa kesi kwa njia ya mtandao
jambo ambalo linasaidia ufanisi wa utendaji wa sekta ya mahakama lakini pia
kuna masuala ya haki za binadamu kuna mabadiliko makubwa sana katika magereza
yetu hali inayopelekea utu wa mtuhumiwa au mahabusu kuwa ni mzuri katika
magaereza yetu.’alisema Jaji Dkt.Masabo
