Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 62 YA UHURU



Tarehe 09 Disemba, 2023 Taifa letu linaadhimisha Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Hili ni tukio la muhimu na la kihistoria kwa Taifa letu. Katika kuadhimisha sherehe hiyo, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania, ametumia Mamlaka aliyopewa chini ya Ibara 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa msamaha kwa wafungwa kwa masharti yafuatayo:-

 

1.  (i)         Wafungwa  wote wenye  sifa  stahiki   wamepunguziwa  robo  (1/4)  ya  adhabu baada ya kutoa punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58. Wafungwa hao ni wale  waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka miwili na kuendelea na ambao wametumikia robo (1/4) ya adhabu zao gerezani na ambao waliingia gerezani  kabla  ya  tarehe  12 Oktoba, 2023  isipokuwa  wafungwa walioorodheshwa katika sharti la 2(i – ix);

 

(ii)                Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu ambao wapo kwenye hatua ya mwisho (Terminal Stage). Ugonjwa na hatua hiyo  vimethibitishwa  na jopo la waganga  chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya;

 

(iii)               Wafungwa wa maisha ambao wametumikia vifungo vyao kwa muda wa miaka kumi na tano (15) na kuendelea. Aidha, kwa wafungwa wote waliobadilishiwa adhabu (commuted) hesabu zao zihesabike kuanzia tarehe ya kubadilishiwa adhabu;

 

(iv)              Wafungwa wa kunyongwa waliomaliza taratibu za Kimahakama na ambao wamekaa gerezani kwa muda wa miaka kumi (10) na kuendelea  kusubiri  utekelezaji wa adhabu ya kifo waliobadilishiwa kifungo kutoka cha kunyongwa kwenda kifungo cha maisha;

 

(v)               Wafungwa wenye makosa ya kujaribu kuua, kujaribu kujiua au kuua watoto wachanga (Attempt to Murder, Attempt Suicide or Infanticide) ambao wametumikia nusu ya adhabu zao na kwa waliohukumiwa kifungo cha maisha masharti ya aya ya 1(iii) hapo juu  yametumika;

(vi)              Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi ambao wametumikia robo (1/4) ya adhabu  zao, baada ya umri wao kuthibitishwa na jopo la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya;

 

(vii)            Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani au wenye watoto wanaonyonya na wasionyonya;

 

(viii)           Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio  na  uwezo  wa  kufanya  kazi, baada ya ulemavu wao kuthibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu  wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya;

 

(ix)              Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini (Under Presidential Pleasure) ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka kumi (10)  au zaidi;

 

2.         Aidha, msamaha huo haukuwahusisha wafungwa wafuatao:-

 

(iii)               Wafungwa wanaotumikia vifungo  vya  nje  chini ya Sheria ya Bodi za Paroli Sura ya 400 (R.E 2002), Sheria ya Huduma kwa Jamii Sura ya 291 (R.E, 2002) na Kanuni za kifungo cha nje {The Prisons (Extra Mural Penal Employment) Regulations, 1968};

 

(iv)              Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa mashauri/kesi za uhujumu uchumi na wale  wanaotumikia vifungo kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, rushwa, usafirishaji au  kujihusisha kwa namna yoyote ile na madawa ya kulevya ikiwemo bangi;

 

(v)               Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kujamiiana, utekaji au wizi wa watoto, kupoka, kuwapa mimba wanafunzi au makosa yoyote yale yanayohusiana na ukatili dhidi  ya  watoto na kujihusisha kwa namna yoyote ile na biashara haramu ya binadamu;

 

(vi)              Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo kwa makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu, unyang’anyi, unyang’anyi wa kutumia nguvu, unyang’anyi  wa kutumia silaha, kumiliki silaha, risasi, milipuko au  kujaribu  kutenda  makosa  hayo; 

 

(vii)            Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali au ujangili;

 

(viii)           Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhilifu wa fedha za Serikali;

 

(ix)              Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au  kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka kwa makosa hayo;

 

(x)               Wafungwa warudiaji;

 

(xi)              Wafungwa waliowahi kupata msamaha wa Mhe. Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania isipokuwa kwa wafungwa walioainishwa katika sharti la 1(iii),(iv) na

(xii)            Wafungwa wa Madeni (Civil Prisoners).

 

Wafungwa 2,244 wamenufaika na Msamaha huu ambapo wafungwa 263 wataachiliwa huru leo tarehe 09/12/2023, wafungwa 2 waliohukumiwa adhabu ya kifo wamebadilishiwa adhabu ya kifo na kuwa kifungo cha maisha na wafungwa 1,979 wamepunguziwa sehemu ya adhabu zao ambazo wataendelea kuzitumikia gerezani.  Ni matumaini ya Serikali kwamba wafungwa walioachiliwa huru leo tarehe 09/12/2023 watarejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa letu na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.