KONGAMANO LA QURAN LATAWALA UJUMBE WA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo (Mb), amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Octoba Mwaka huu 2025
Mhe. Sillo alitoa wito huo alipomwakilisha Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Doto Biteko, katika Kongamano la 30 la Kimataifa la Quran na Hadith lililoandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kwa kushirikiana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), lililofanyika jijini Dar es Salaam, Mei 20, 2025.
Katika hotuba yake, Mhe. Sillo amesema kuwa vitabu vitakatifu vya dini ni mwongozo wa maisha bora kwa waumini wa dini mbalimbali na kwa jamii kwa ujumla. Ameongeza kuwa kusoma na kusikiliza mafundisho ya vitabu hivyo ni ibada yenye malipo makubwa kwa Mwenyezi Mungu, hivyo alitoa pongezi kwa waumini wote walioshiriki kongamano hilo.
Aidha, Mhe. Sillo amesisitiza umuhimu wa kuwa na maadili mema, akiwahimiza wananchi kuishi kwa kufuata mafundisho ya vitabu vitakatifu vya dini, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
“Tukiweza kujijibu maswali kuhusu maadili yetu na vijana wetu, tutakuwa tumejenga Taifa lenye Raia wema, wazalendo na watiifu,” Amesisitiza Sillo.
Naye, Mwenyekiti wa JMAT Sheikh Alhad Mussa Salum, amesema kuwa vitabu vitakatifu vinaunganisha watu kwa kuwafundisha kupendana, kushirikiana na kuishi kwa amani licha ya tofauti zao za kiimani. Ameongeza kuwa mafundisho hayo yanapaswa kuwa msingi wa kujenga jamii yenye mshikamano, inayotanguliza maelewano badala ya migongano.