Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

"TUZINGATIE MAADILI NA USIMAMIZI WA SHERIA KUUENZI MUUNGANO " WAZIRI MASAUNI



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amewataka Wananchi kuhakikisha wanaendelea kusimamia misingi ya Muungano kwa kujenga Taifa lenye maadili na usimamizi wa sheria.

Waziri Masauni aliyasema hayo Aprili 15, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kipindi cha miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

"Tangu  enzi za waasisi wa Muungano Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume walijenga Taifa lenye maadili hivyo hatuna budi kuendelea kufuata sheria za Nchi kwani Vyombo vya Usalama havita kuwa na simile kwa mtu yeyote yule."Alisema Mhandisi Masauni

Mhandisi Masauni amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano Wizara  inajivunia mafanikio mengi ikiwa ni  pamoja na maboresho ya muundo wa Jeshi la Polisi na Uhamiaji ambapo maboresho hayo yamesaidia kutanua wigo wa utoaji huduma kwa ufanisi,weledi na usasa na pia kuongeza  ushirikishwa wa jamii jambo ambalo limesaidia kubaini,kuzuia na kutanzua uhalifu.

Aidha, matumizi ya mifumo mbalimbali ya kidigitali  katika Vyombo vya Usalama  ni miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa ambayo yameleta usasa, urahisi, na ubora katika kutoa huduma kwa Wananchi.

Mifumo hiyo ni pamoja na  mfumo wa haki jinai, mfumo wa uhamiaji mtandao,usajili wa vitambulisho vya Taifa kupitia mtandao na kwa sasa kuelekea katika utekelezaji wa mradi wa ufungaji wa kamera(CCTV Camera) maalumu za kuzuia uhalifu kama vile  ujambazi, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani, wizi na matukio mengine.