Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

KATIBU MKUU MMUYA AMELIAGIZA JESHI LA ZIMAMOTO KUONGEZA USIMAMIZI UJENZI WA NYUMBA ZA WATUMISHI KIKOMBO



Ni mwendelezo wa ziara ya siku mbili ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ndg. Kaspar Mmuya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Ujenzi kwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo miongoni mwa miradi iliyokaguliwa ni ujenzi wa nyumba za Askari wa zimamoto Kikombo na Majengo ya Vituo na Ofisi za Zimamoto Chamwino na Nzuguni Jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kupitia miradi hiyo Mmuya amesema kuwa katika Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za ghorofa sita za Askari wa Jeshi la Zimamoto zilizopo Kikombo Jijini Dodoma awali Serikali ilitoa kiasi cha shilingi Biliono 4.3 ambazo kwa sasa zimetumika. Serikali ya awamu ya sita imeongeza tena kiasi cha Shilingi Bilioni 2 ili kukamilisha ujenzi wa Majengo yote sita ya ghorofa ambapo ghorofa moja inauwezo wa kubeba familia kumi na kwa ghorofa sita jumla ya familia sitini za Askari zitanufaika na nyumba hizo za kisasa ambapo ghorofa nne zipo katika hatua ya mwishoni ya umaliziaji na ghorofa mbili zikiwa tayari kwenye hatua ya msingi.

 “Tumekubaliana na Kamishna wa Zimamoto kuhakikisha kuwa anaimarisha usimamizi wa fedha ili fedha iliyotolewa na Serikali iweze kuonekana kupitia mradi huo. Tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kulijali Jeshi la Zimamoto kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya kujenga Ofisi ikiwa ni kuboresha mazingira bora ya kazi kwa Askari, kuboresha makazi ya Askari kwa kujenga Nyumba bora na za kisasa na pia upatikanaji wa Vitendea kazi.”Alisema Mmuya.
Katika hatua nyingine Mmuya ametembelea katika eneo la Chamwino ambapo pamejengwa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Chamwino na kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.1 ambacho kimekamilika na kipo tayari kwa ajili ya matumizi na kukagua ujenzi wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Nzuguni ambacho kimegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.2 kwa sasa kikiwa kimekamilika.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali Jeshi la Zimamoto na Uokoaji CGF John Masunga amesema kuwa lengo la Jeshi ni kuongeza huduma kwa Watanzania na kwa sasa kunamkakati ambao unaelekeza kujenga vituo mpaka ngazi ya Wilaya ambapo mpaka sasa zipo fedha ambazo zimeshapokelewa kwa ajili ya kuanzisha vituo saba na Ofisi katika Mikoa saba ambayo ni Manyara, Simiyu, Songwe,Katavi,Kagera,Geita na Njombe.

 Wizara itaendelea kutunza Rasilimali zilizopo na pia kuangalia zinatumika vizuri kwa manufaa ya Askari. Matumaini ya Jeshi la Zimamoto ikiwa ni kulinda usalama wa Raia katika kuzuia majanga na kupunguza madhara pale majangwa yanapotokea na kutowaathiri Wananchi.Mategemeo ya Mheshimiwa Rais ni kuona Wananchi wakifanya kazi katika mazingira yenye amani na utulivu.
Wito umetolewa kwa Taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha wanapanda miti ya matunda ili kuimarisha afya za Watumishi na pia kutunza mazingira.