DKT. MWIGULU AZINDUA KITAMBULISHO CHA TAIFA KILICHOBORESHWA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua kitambulisho cha Taifa kilichoboreshwa, toleo la mwaka 2026, akisisitiza kuwa uwekezaji huo unapaswa kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza usumbufu kwa wananchi.
Katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Stendi ya Zamani ya Mailimoja, Kibaha, mkoani Pwani, Waziri Mkuu pia amezindua teknolojia mpya ya uzalishaji wa vitambulisho, programu tumizi ya NIDA Wallet na magari 10 ya huduma za usajili.
Amesema maboresho hayo yanafungua fursa ya kuunganisha huduma mbalimbali kupitia utambulisho mmoja, hivyo kupunguza ulazima wa wananchi kubeba vitambulisho vingi katika shughuli zao za kila siku.
Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa kila Mtanzania anayestahili kupata kitambulisho cha Taifa anapaswa kukipata kwa wakati, bila usumbufu wala urasimu.
Amempongeza Rais Dkt. Samia kwa kuwezesha uwekezaji huo, akisema matumizi ya teknolojia yanapaswa kuboresha huduma, kuimarisha utawala bora na kupanua fursa za wananchi katika shughuli za kiuchumi.
