Tanzania logo
United Republic of Tanzania

Ministry of Home Affairs

CGI DKT. ANNA MAKAKALA AWEKA ALAMA UJENZI WA KITUO CHA AFYA BOMA TANGA


Ujenzi wa Kituo kipya cha Afya Boma katika eneo la Chuo cha Uhamiaji Raphael Kubaga, Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga, umeanza rasmi ukiwa na lengo la kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, watumishi na askari wa Uhamiaji, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za kijamii.

‎Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania, CGI Dkt. Anna Makakala, ameweka alama ya kushiriki ujenzi kwa kubeba mawe na kuyapanga Katika Msingi wa mradi huo Novemba 13, 2026, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa ndani ya eneo la Chuo cha Uhamiaji Raphael Kubaga Katika Kata ya Boma, Wilaya ya Mkinga.

‎‎Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, CGI Dkt. Makakala ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa rasilimali fedha zinazowezesha Chuo cha Uhamiaji Raphael Kubaga na Idara ya Uhamiaji kwa ujumla kutekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya taasisi na wananchi wanaoizunguka.

‎‎Mradi huo unatekelezwa kwa mfumo wa (Force Account) chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, huku Serikali ikitoa zaidi ya Shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali itakayowezesha kituo hicho kutoa huduma bora za afya.

‎Miundombinu inayojengwa ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la huduma za mama na mtoto, maabara, jengo la kufulia (Laundry) pamoja na kichomea taka.

‎Kituo hicho kinatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Kata ya Boma na maeneo jirani, pamoja na watumishi na askari wa Chuo cha Uhamiaji Raphael Kubaga.

‎‎Ujenzi wa mradi huo ulianza Oktoba 29, 2026, ambapo jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ndilo lililoanza kujengwa na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu. Kwa ujumla, mradi mzima unatarajiwa kukamilika ifikapo Januari 31, 2027.

‎Utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali na Idara ya Uhamiaji katika kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma bora kwa Wananchi.