MHE. AYOUB: USALAMA BARABARANI NI JUKUMU LA KILA MTANZANIA
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema usalama barabarani ni jukumu la kila Mtanzania, hivyo kila Taasisi na Mwananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuzuia ajali na kulinda maisha ya watumiaji wa barabara.
Mhe. Mahmoud amesema hayo jijini Arusha, wakati akifunga Wiki ya Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania (RSA) iliyobebwa na kaulimbiu ya “Zuia Ajali, Fanikisha Dira 2050,” ambapo amefafanua kuwa kuzuia ajali ni muhimu katika kulinda uhai, na afya ambayo ni msingi wa kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema barabara na huduma za usafiri zina nafasi kubwa katika maendeleo kwa kuwa zinawaunganisha wananchi na shule, hospitali, masoko, maeneo ya kazi na shughuli za uzalishaji. hivyo, amesema kuwa ajali zinapotokea huathiri familia, huduma za afya, waajiri na uchumi wa Taifa.
Kadhalika, amewataka madereva na waendesha pikipiki kuzingatia sheria za matumizi ya barabara, ikiwemo kuzingatia mwendo unaoruhusiwa, kutotumia simu wakati wa kuendesha, kuvaa kofia ngumu na kutumia mikanda ya usalama. Aidha amewataka abiria kutokubali vitendo vinavyohatarisha usalama wao na kutoa taarifa kupitia njia rasmi.
Pia, ametoa wito kwa RSA kuimarisha utawala na uwajibikaji wa shirika, kuweka viwango vya elimu inayotolewa, kutumia utaalamu uliopo ndani ya shirika na kuweka vipaumbele vinavyopimika.
