Tanzania logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

KATAMBI AITAKA MAGEREZA KUWEKA KIPAUMBELE UJUZI KWA WAFUNGWA


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesisitiza umuhimu wa kuwapatia wafungwa mafunzo ya ufundi stadi yatakayowawezesha kujenga ujuzi, kujitegemea na kuwa na uwezo wa kushiriki katika shughuli za maendeleo mara baada ya kumaliza vifungo vyao.

Katambi ameyasema hayo Novemba 25, 2026, katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya ushirikiano kati ya Jeshi la Magereza na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), iliyofanyika katika viwanja vya Gereza Kuu la Karanga, Moshi mkoani Kilimanjaro, ikiwa na lengo la kuimarisha mafunzo ya ufundi na utambuzi wa ujuzi kwa wafungwa.

 Ameeleza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuboresha mfumo wa marekebisho ya tabia kwa wafungwa, kwa kuwapatia fursa ya kujifunza stadi mbalimbali zitakazowasaidia kujipatia kipato, kupunguza utegemezi na kuwa raia wenye mchango chanya katika jamii baada ya kurejea uraiani.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo kutekeleza makubaliano yaliyosainiwa kwa vitendo ili mafunzo yatakayopatikana yawe na tija, yakilenga kuwajengea wafungwa uwezo, kuimarisha urekebishaji wa tabia na kuongeza fursa za ajira na kujiajiri baada ya kutoka gerezani.

Hafla hiyo imekwenda sambamba na zoezi la kuwatunuku vyeti wafungwa 481 waliohitimu Programu ya Urekebu wakiwa Gerezani ambao wamepata ujuzi wa fani mbalimbali ikiwemo mapishi, ufundi bomba, ushonaji na nyinginezo.