KATAMBI AFUNGUA MAFUNZO YA CPX IMARISHA UWEZO 2026
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amefungua zoezi la Command Post Exercise (CPX) Imarisha Uwezo 2026, linalolenga kuimarisha uratibu, ushirikiano na utayari wa pamoja wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo uliofanyika Novemba 23, 2026, katika Shule ya Kijeshi ya Ulinzi wa Anga jijini Tanga, Katambi alisema mazingira ya sasa ya kiusalama yanahitaji vyombo husika kuwa tayari wakati wote na kutumia teknolojia na maarifa yanayoendana na wakati.
Alisisitiza kuwa usalama wa nchi hauwezi kujengwa na chombo kimoja pekee, bali unahitaji ushirikiano wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi za Serikali zinazohusika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda, alisema maandalizi ya zoezi hilo yamekamilika na washiriki wako tayari kuanza utekelezaji.
Alisema zoezi hilo litawajengea washiriki uelewa wa pamoja katika kupanga na kutekeleza operesheni zinazohitaji ushirikiano wa vyombo mbalimbali vya usalama.
Zoezi la CPX Imarisha Uwezo 2026 linashirikisha Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na taasisi za Serikali zinazohusika na masuala ya usalama.
