SILLO: JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI LINAENDELEA KWA BIDII KUOKOA MAFUNDI WALIOKWAMA MGODINI SHINYANGA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, ametembelea eneo la Mgodi wa Nyandolwa, katika Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Shinyanga, Agosti 16, 2025 kushuhudia juhudi za uokoaji wa mafundi waliokwama chini ya ardhi baada ya kuangukiwa na kifusi
Ajali hiyo ilitokea tarehe 11 Agosti 2025 katika eneo lenye leseni ya uchimbaji inayomilikiwa na kikundi cha wachimbaji wadogo maarufu kama Wachapakazi, ambapo mafundi wapatao 25 walikuwa wakifanya kazi ya ukarabati kwenye mashimo matatu tofauti ya uchimbaji dhahabu.
Akizungumza katika eneo la tukio, Mhe. Sillo ameeleza kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea kufanya kazi kwa bidii, usiku na mchana kuhakikisha kuwa mafundi wote waliokwama wanapatikana haraka iwezekanavyo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia taratibu za usalama kwenye migodi, akiwataka wamiliki wote wa migodi nchini kuhakikisha mazingira salama kwa wafanyakazi wao ili kuepusha majanga ya aina hii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ametoa ufafanuzi kuhusu mwenendo wa uokoaji akieleza kuwa hadi kufikia Agosti 16, 2025 jumla ya wafanyakazi watano wameokolewa ambapo watatu wako hai, mmoja alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu hospitalini na mwingine alikutwa tayari amefariki dunia ndani ya shimo, huku mafundi wengine 20 wakiendelea kutafutwa.
“Tuendelee kupambana hadi tuhakikishe tunawatoa watu wetu salama. Mhe. Rais ametoa maagizo mahsusi ambayo yameanza kutekelezwa kwa asilimia kubwa, ikiwemo kuongezwa kwa nguvu kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,” Aliongeza Mtatiro.