KATAMBI AMWAKILISHA RAIS SAMIA MRADI WA BILIONI 4
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Hafla ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Skuli ya Mafunzo ya Amali,iliyoko Kijiji cha Kangagani,Kaskazini Pemba.
Uwekaji jiwe la msingi wa Skuli hiyo ni muendelezo wa jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha Sekta ya Elimu ambapo leo Mheshimiwa Rais Samia ameweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Amali Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Waziri Katambi ameweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa skuli hiyo, ambao utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 4.1 huku mradi huo ukijumuisha Ujenzi wa Maabara,Kituo cha Teknolojia ya Habari,Nyumba za Walimu, Ufundi Umeme,Ufundi Bomba,Ushonaji, Karakana za Ubunifu, Ukumbi na nyumba za kulala wanafunzi.
Mradi huo unajengwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Taasisi ya Rais Samia (Samia Foundation) ambao unagharimu kiasi cha Tanzania Shilingi Bilioni 4.1 ambapo Taasisi ya Rais Samia imechangia kiasi cha Shilingi Bilioni 2.5 na Mamlaka ya Elimu Tanzania imechangia kiasi cha Shilingi Bilioni 1.6.
